KESI za ubakaji katika Mahakama za Watoto nchini zimeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Hayo yalibainishwa na Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Kinondoni, Hamisa Kalombola kwenye semina ya siku moja iliyokuwa ikizungumzia mada ya ndoa katika umri mdogo na ubakaji, iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA).
Hamisa alisema ingawa hana takwimu za matukio ya ubakaji, lakini ni mengi ambayo anashindwa kuelewa chanzo chake.
Aliwashauri waandishi wa habari kuripoti habari za Mahakama ya Watoto ambapo kuna matukio mengi ya ubakaji, ili jamii ielewe matatizo wanayoyapata watoto.
Pia aliwashauri waandishi hao kuripoti taarifa kwa usahihi na bila upendeleo.
Mmoja wa washiriki wa semina hiyo, Pudensiana Temba, ambaye alikuwa katika utafiti wa kujua chanzo cha watoto kuolewa katika umri mdogo alisema ni umasikini wa baadhi ya wanachi wa vijijini.