CHAMA cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha na Huduma za Ushauri nchini (TUICO), kimeanza mikakati ya kuwapiga msasa viongozi na wanachama wake kote nchini kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya sheria za kazi zinazotarajiwa kuanza kutumika hivi karibuni.
Akizungumza na Tanzania Daima mjini Morogoro wakati wa mafunzo hayo kwa makatibu wasaidi 35 wa chama hicho mkoani hapa, Katibu Mkuu wa TUICO, Boniface Nkakatisi, alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kubaini kuwa mabadiliko ya sheria hizo yanaweza kuleta changamoto kubwa katika utendaji wao hivyo wameamua kuwaandaa mapema viongozi na wanachama wao katika kukabiliana na changamoto hizo.
Alisema uchunguzi uliofanywa na TUICO kuhusu mabadiliko hayo umebaini kuwa utendaji wa viongozi na wanachama wao unapaswa kubadilika, ili kwenda sambamba na sheria hizo zinazotarajiwa kuanza kutumika Oktoba mwaka huu.
Katika mabadiliko hayo, jumla ya sheria mbili zimeingizwa katika mfumo wa wafanyakazi nchini ambazo ni sheria ya Asasi na sheria ya Ajira na Uhusiano kazini.
Katibu Mkuu huyo wa TUICO alisema kubadilishwa kwa sheria hizo kunatokana na kupitwa na wakati, hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya sasa ya ajira, ikiwamo utoaji wa fidia kwa wafanyakazi wanaoathirika na utendaji wao wakiwa kazini pamoja na kutotoa fursa nzuri ya haki na uhuru kwa wafanyakazi.