logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumapili, 10 septemba 2006
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1
Si uadilifu kuchanganya dini na siasa katika dola mseto
Deusdedit Jovin


JUMAPILI iliyopita tuliona urefu na upana wa ukuta unaotenganisha dini na siasa katika dola yenye raia walio na dini mseto kama vile Tanzania.

Swali lililo mbele yetu leo ni: Je, katika nchi ile ile moja kama vile Tanzania, au nchi nyingine yoyote yenye Serikali Kuu moja na inayokaliwa na raia wamoja, lakini raia wenye dini mseto, ni upuuzi kujenga ukuta wa sheria zinazotenganisha ofisi za kidini kwa upande mmoja na ofisi za kiserikali kwa upande mwingine?

Msimamo wa makala hii ni kwamba katika dola yenye raia wenye dini mseto si upuuzi kujenga ukuta unaotenganisha dini na siasa. Utetezi unafuata bila kuchelewa.

Hatuwezi kuifanya Sharia iwe mizani yetu ya maisha kama wanavyofanya Waislamu, kwa sababu si watu wote wanaamini kama wanavyoamini wao kwamba ndoa za mitala ruksa; kwamba Mungu anayo nafsi moja; na kwamba Mungu hazai. Tukifanya hivyo, wasio Waislamu wataporwa uhuru wao wa kuabudu.

Hatuwezi kuifanya Torati ya Musa iwe mizani yetu ya maisha, kama wanavyofanya Wayahudi, kwa sababu si watu wote wanaamini kama wanavyoamini wao kwamba talaka katika ndoa ruksa; na kwamba mzinzi apigwe kwa mawe hadi kufa au sharti akatwe ulimi ili asipate fursa ya kumtongoza mtu tena. Tukifanya hivyo, wasio Wayahudi wataporwa uhuru wao wa kuabudu, na watu wengi wanaweza kukatwa ndimi.

Hatuwezi kuzifanya sheria za Kanisa ziwe mizani yetu ya maisha, kama wanavyofanya Wakatoliki, kwa sababu si watu wote wanaamini kama wanavyoamini wao kwamba Mungu mmoja anazo nafsi tatu; kwamba kila nafsi ya Mungu huyu ni Mungu pia; kwamba nafsi ya pili ya Mungu huyu ilizaliwa bila kuumbwa; na kwamba Yesu ni Mungu-Mtu. Tukifanya hivyo, wasio Wakatoliki wataporwa uhuru wao wa kuabudu.

Hatuwezi kuzifanya sheria za dini ya Kihindu ziwe mizani yetu ya maisha, kama wanavyofanya Wahindu, kwa sababu si watu wote wanaamini kama wanavyoamini wao kwamba kuna mamilioni ya miungu wa kike huko angani; kwamba kuna mamilioni ya miungu wa kiume huko angani; na kwamba miungu hawa wanaoana na kuzaliana. Tukifanya hivyo, wasio Wahindu wataporwa uhuru wao wa kuabudu.

Hatuwezi kuzifanya dini za ‘kipagani’ ziwe mizani yetu ya maisha, kama wanavyofanya wao, kwa sababu si watu wote wanaamini kama wanavyoamini wao kwamba kufanya mapenzi shambani wakati wa mwezi mwandamo kunaongeza rutuba shambani na hivyo kuongeza mazao; na kwamba mwanamke mwenye mimba akila mayai anazaa mtoto asiye na nywele. Tukifanya hivyo, wasio wapagani wataporwa uhuru wao wa kuabudu.

Aidha, kwa sababu hizo hizo, hatuwezi kuzifanya dini nyingine ziwe mizani yetu ya maisha. Lakini liko jambo mbadala tunaloweza kufanya kwa faida ya watu wote. Tunaweza kutumia matilaba ya binadamu (human goods) kama mizani huru ya maisha yetu sote!

Matilaba ya binadamu ni kitu chochote kizuri kwa ajili ya ustawi wa binadamu na jamii kwa ujumla. Mifano ya matilaba ya binadamu ni pamoja na uhai, ndoa, mali, ukweli, raha, madaraka, urafiki, ukweli, elimu bora, amani na hasa amani ya moyo, afya njema, uhuru wa utashi, uhuru wa kuabudu au tuseme ibada yenyewe, urembo, udugu, mshikamano, uaminifu, mazoezi ya viungo, burudani, raha, furaha, na kadhalika.

Tangu misingi ya ulimwengu ilipoumbwa, watu wote katika sehemu zote za ulimwengu wanakubali kwamba hivi ni vitu vizuri na huwa wanavifukuzia. Kwa hiyo matilaba ya binadamu ni mizani huru kwa ajili ya maisha ya watu wote katika jamii mseto. Sasa tuone jinsi mizani hii inavyotumika. Nitajieleza kwa njia ya mzunguko na hasa kwa njia ya mifano.

Katika mfano wa kwanza, tutazame kitendo cha kuua, kusitisha uhai wa mtu kwa makusudi, kwa kumpiga risasi ya moyo kutokana na chuki binafsi (murder). Watu wote wenye akili timamu, wanakubali kwamba mauaji hayo ni kitendo kibovu kimaadili kwa sababu tatu.

Kwanza, lengo la mtendaji (finis operantis) ni baya. Anakusudia kuhujumu uhai wakati uhai wa binadamu ni aina mojawapo ya matilaba ya binadamu yanayopaswa kuheshimiwa na watu wote, siku zote, na katika sehemu zote.

Pili, madhara ya tendo lenyewe hata kama lingefanyika kwa bahati mbaya (finis operis) ni mabaya. Kwa mujibu wa kanuni za baiolojia, mtu akipigwa risasi ya moyo, lazima atapoteza uhai jambo ambalo ni baya.

Tatu, tukiangalia kimefanyika lini na wapi, kimefanywa na nani, na kwa vipi, tutagundua kwamba mazingira yanayokizunguka kitendo (circumstances) ni mabaya. La muhimu katika mfano huu ni kwamba aliyeuawa ni mtu asiye na hatia, kwa maana kwamba hakuuawa kwa sababu alikuwa anataka kuua, bali kutokana na chuki binafsi.

Kwa ujumla, katika mfano huu, lengo la mtendaji ni baya, matokeo ya kitendo ni mabaya, na mazingira ni mabaya. Kwa sababu haya matatu yana uhasama na matilaba ya binadamu, kila mtu mwenye akili timamu, bila kujali dini, itikadi au utamaduni, atakwambia kwamba kumuua mtu asiye na hatia kwa makusudi, na hasa kutokana na chuki binafsi, ni kitendo kibaya kimaadili.

Mfano wa pili ni kitendo cha kuiba. Katika makala hii, kuiba ni kitendo cha mtu mmoja kuchukua mali bila ridhaa ya mmiliki wakati mchukuaji hana mahitaji yanayoyazidi ya mmiliki na wala hajashindwa kuipata mali hiyo vinginevyo. Kwa kuzingatia maana hii, watu wote wenye akili timamu, watakubali kwamba kuiba ni kitendo kibaya kimaadili kwa sababu zile zile tatu.

Lengo ni baya, matokeo ni mabaya na mazingira ni mabaya. La muhimu hapa ni kwamba mtu mmoja anachukua mali ya mwingine bila ridhaa, wakati mwenye mali anaihitaji zaidi kuliko anayeichukua, tena wakati ambapo anayeichukua hajashindwa kuipata vinginevyo.

Kwa ujumla, katika mfano huu, lengo la mtendaji ni baya, matokeo ya kitendo ni mabaya, na mazingira ni mabaya. Kwa sababu haya matatu yanao uhasama na matilaba ta binadamu, kila mtu mwenye akili timamu, bila kujali dini, itikadi au utamaduni, atakwambia kwamba kuiba ni kitendo kibaya kimaadili.

Mfano wa tatu ni kitendo cha kudanganya. Katika makala hii, kudanyanga ni kitendo cha mtu kusema maneno anayojua kuwa si kweli kwa lengo la kumlaghai mtu mwenye haki ya kuujua ukweli. Kwa msingi wa maana hii, watu wote wenye akili timamu, watakubali kwamba kudanganya ni kitendo kibaya kimaadili kwa sababu zile zile tatu.

La muhimu hapa ni kwamba mtu anasema maneno ambayo anajua kuwa si kweli kwa mtu mwenye haki ya kuujua ukweli huo.

Kwa ujumla, katika mfano huu, lengo la mtendaji ni baya, matokeo ya kitendo ni mabaya, na mazingira ni mabaya. Kwa sababu haya matatu yana uhasama na matilaba ya binadamu, kila mtu mwenye akili timamu, bila kujali dini, itikadi au utamaduni, atakwambia kwamba kudanganya ni kitendo kibaya kimaadili.

Tungeweza kuendelea kwa kuzingatia mantiki hii hii tukifanya tathmini ya uadilifu wa matendo kama vile: ngono katika ndoa, ngono nje ya ndoa, uzinzi, ngono wakati wa dirisha la rutuba katika tumbo la mwanamke, ngono wakati wa dirisha lisilo na rutuba katika tumbo la mwanamke.

Pia tunaweza kufanya tathmini ya uadilifu wa matendo kama vile: ngono kwa kondomu wakati wa dirisha la rutuba katika tumbo la mwanamke, ngono kwa kondomu wakati wa dirisha lisilo na rutuba katika tumbo la mwanamke, biashara ya kuwapambanisha wasichana warembo majukwaani, biashara ya utumwa, ukeketaji na kadhalika.

Hata hivyo ukurasa huu hautoshi. Lakini, kwa mifano hiyo mitatu hapo juu tunaweza kufanya majumuisho muhimu yatakayotuwezesha kubaini kanuni ya jumla katika mchakato wa kufanya tathmini ya kimaadili kwa msingi wa matilaba ya binadamu.

Kwa kuzingatia mifano hii mitatu hapo juu, ukweli ni huu. Katika kufanya tathmini ya kimaadili kuhusiana na kitendo chochote cha binadamu, mambo matatu lazima kuzingatiwa kabisa: lengo la mtendaji; tamati ya kitendo chenyewe hata kama kimefanyika kwa bahati mbaya; na mazingira yanayokizunguka kitendo husika.

Na sasa inaonekana kwamba ili kitendo chochote cha binadamu kiitwe kitendo kizuri kimaadili lazima lengo la mtendaji liwe zuri, lazima tamati ya tendo lenyewe iwe nzuri, na lazima mazingira ya tendo yawe mazuri. Kwa hapa, hii tutaiita mafiga matatu ya tendo adilifu.

Kwa mujibu wa kanuni hiyo, kabla tendo lolote la binadamu halijaitwa zuri kimaadili, lazima wanachama wote watatu katika mafiga haya matatu wawe ‘wazuri’.

Katika mchakato huu ‘uzuri’ unapimwa dhidi ya matilaba ya binadamu ambayo ni mizani huru. Hujuma yoyote kwa matilaba yoyote ya binadamu inaharibu uzuri wa mwanachama katika utatu huo, na hivyo kuharibu uzuri wa kitendo kimaadili.

Hapa mantiki ni kwamba kila binadamu, siku zote na sehemu zote analo jukumu la kujizuia kuhujumu matilaba ya binadamu kwa makusudi. Nafikiri mifano hapo juu inatosheleza kuliweka hili bayana.

Kwa hiyo basi, kwa kuzingatia kanuni hii, sasa tuko tayari kuitumia mizani ya matilaba ya binadamu katika kupima ubora wa mfumo wa sheria zinazoshabikia ubia kati ya dini na siasa katika dola yenye raia walio na dini mseto kama vile Tanzania.

Tuanze na mazingira (circumstances). Hapa mazingira ni dola kama vile Tanzania ambako kuna raia wanaoamini katika dini mseto, kama vile Ukristo, Uyuda, Uislamu, Uhindu, Ubudha, Ujeni, Upagani na kadhalika, huku kila jumuiya ikiwa na mizani yake ya maisha iliyo na misingi yake katika misahafu, mafundisho ya waanzilishi wa dini na tamaduni zenye nasaba na mahali ambako dini hizo zilianzia.

Haya ndiyo mazingira yanayotuhusu sasa hivi. Na mazingira haya kama tulivyoyakuta tangu tupate uhuru hatujayabadilisha, wala si rahisi kuyabadilisha. Kwa hiyo, ni bora kuyachukulia kama mazingira mazuri kwa ajili ya tathmini hii.

Sasa tuone lengo la mtendaji (finis operantis). Katika dola yenye raia walio na dini mseto, ikiwa sheria za nchi zitatungwa kwa kuegemea dini mojawapo, serikali katika nia njema kabisa ya kutimiza wajibu wake, itaanza kuzitekeleza. Lengo hili ni zuri kwa sababu kutimiza wajibu ni jambo jema kimaadili.

Hatimaye sasa tuone tamati ya kitendo chenyewe (finis operis). Katika dola yenye raia walio na dini mseto, ikiwa sheria za nchi zitatungwa kwa kuegemea dini mojawapo, katika serikali kutekeleza majukumu yake, mambo yafuatayo yatatokea, tutake tusitake:

Mosi, serikali yenye mamlaka turufu katika nchi nzima itajikuta inatekeleza amri zenye msingi wake katika dini moja, kwa maana ya kuwalazimisha wale wasioamini dini hiyo kuiamini kwa nguvu.

Pili, serikali yenye mamlaka turufu katika nchi nzima itajikuta inazilazimisha jamii za kiraia, kama vile familia na asasi zisizo za kiserikali kama vile makanisa na misikiti kuendesha shughuli zake kwa kufuata maagizo ya serikali, kinyume cha taratibu walizo jiwekea.

Tatu, kwa sababu dini moja itakuwa imekwezwa dhidi ya nyingine, viongozi wa kiroho katika dini hiyo watajikuta wana sauti juu ya serikali, wakielekeza ifanye lipi na iache lipi. Matokeo ya hili ni udikteta kwa jumuiya nyingine za waamini wasioamini katika dini rasmi ya dola.

Hivyo basi, katika mazingira haya, kwa kuwa lengo la mtendaji (finis operantis) ambaye ni serikali ni zuri; kwa kuwa kitendo cha serikali kutekeleza sheria za nchi kina tamati (finis operis) mbaya, kwa maana kwamba inahujumu matilaba ya raia; na kwa kuwa mazingira ni mazuri; inafuata kimantiki kwamba mafiga haya yana dosari hapa! Kwa hiyo, si jambo adilifu kuchanganya dini na siasa katika dola yenye raia walio na dini mseto.

Mizani ya matilaba ya binadamu kama msingi wa haki na majukumu katika jamii ni mwamba imara wa jamii yenye amani! Hii ni kweli kwa sababu, watu wote makini, katika zama zote, na katika sehemu zote duniani wameunga mkono mizani hii.

Mwanafalsafa Aristotle, aliposema kwamba “kila binadamu hufukuzia kitu anachokiona kuwa ni kizuri kwa ajili ya ustawi wake” alikuwa anazungumzia mafiga haya.

Mgriki aitwaye Marcus Tullius Cicero aliposema kwamba “akili timamu ndiyo sheria mama” alikuwa anazungumzia mafiga yale yale.

Mjerumani Emmanuel Kant aliposema “mara zote mtumie binadamu kufikia malengo yako lakini bila kuhujumu akili na utashi wake huru kwani kufanya hivyo ni kumtumia kama kitu kisicho binadamu” alikuwa anazungumzia kitu kile kile.

Mkatoliki aitwaye Thomas Aquinas aliposema kwamba “sheria mbaya si sheria kamwe” alikuwa anazungumzia mafiga yale yale.

Myahudi aitwaye Martin Buber alikuwa anazungumzia mafiga yale yale pale alipolaani mifumo ya kibaguzi inayowafanya wanadamu wawe na uhusiano wenye sura ya “mimi na kitu hiki” badala ya kuwa na sura ya “mimi na mtu huyu”.

Mhindu aitwaye Mahatma Gandhi aliposema “Mungu hana dini” alikuwa anazungumzia kitu kile kile.

Vilel vile, Mtume Paulo aliposema kuwa “mbinu mbaya haziwezi kufanikisha malengo mazuri” na Julius Nyerere aliposema: “nchi yetu haina dini lakini watu wake wana dini.”

Ni msingi ule ule uliosukuma Yesu Kristo kusema “mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe,” na bila shaka ndiyo ilikuwa nia ya Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaaban Simba, aliposema: “Baraza la Ulamaa Taifa kwa heshima na taadhima kubwa kabisa linaiomba Serikali pamoja na Bunge letu tukufu limpe kila Mtanzania haki yake (ya kuabudu) bila kuitikia shinikizo la mtu au kikundi kinachotaka kwa dhana tu kumzuia mtu au kikundi kingine kutekeleza ibada au kudai na kupata haki yake.”

Lakini kama kanuni hii ya mafiga matatu ya tendo adilifu ni mbovu, basi tukubali kuwa kina Aristotle, Cicero, Aquinas, Kant, Buber, Gandhi, Paulo, Nyerere na Yesu walikosea sana. Na kama walikosea hivyo, basi dunia nzima inaogelea katika matope ya makosa yao. Lakini si rahisi watu hawa wakosee hivyo na dunia nzima isigunde hivyo hadi leo. Kwa hiyo hawakukosea.

Kwa kuhitimisha basi, ina maana kama kuna mtu anapinga kanuni ya mafiga matatu ya tendo adilifu, anawapinga wote hawa, ama kwa sababu ana mawazo potofu! Historia ya ulimwengu inasema nini kuhusu hili? Tukutane Jumapili ijayo.

Mwandishi wa makala hii ni mkazi wa Dar es Salaam, anapatikana kwa simu 0713 - 425579 na barua pepe: deusjovin@hotmail.com

h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2006 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa mkwepu na makunganya, slp 15261, dar es salaam, tanzania
simu +255-22-2120604  •  faksi +255-22-2126234