NASIKITIKA kwamba Tanzania inakuwa nchi ya giza. Ndani ya nchi ya giza kuna taifa la giza. Katika taifa la giza kutakuwa na mateka wa giza.
Nchi ya giza, taifa lililokumbwa na giza na mateka wa giza, wote ni mahabusu katika giza nene ambamo ama wamebakia kulalama, kupiga ramli au kuishi kwa matumaini ya kukombolewa na wengine.
Giza limeweka kufuli kwenye akili za watu – watawala na watawaliwa. Na kadiri miaka inavyokwenda, vijukuu na vitukuu vya giza ndivyo vinachukuliwa kuwa matatizo, badala ya ‘giza baba.’
Katika mkanganyiko na mkengeuko – penye vurugu kichwani na kupotea kwa dira – si tu nchi na taifa na watu wake wanadumaa. Hapana. Bali wanadidimia pia. Wanamong’onyoka kiakili.
Hapana. Katika giza, wanaangamia. Wanateketezwa na moto usioleta nuru. Vifuu visivyotoa moshi. Wanakuwa mkaa usioweza kupika chochote na jivu lisiloweza kuonekana ndani ya giza nene.
Ni hapo nchi ya Tanganyika, taifa la Tanzania na Watanzania walipofikia; miaka zaidi ya 40 tangu kupatikana kwa uhuru.
Watu wa kileleni – watawala – wamebaki na fikra dhaifu. Nuru yao ni jua lijalo kwa miujiza mradi kumekucha. Nuru yao ni mbalamwezi kutoka kisahani cha kioo kizungukacho kwa awamu. Nuru yao ni vibatari – urithi wa watu wa ujima.
Nasema hiyo ndiyo Tanzania katika giza ambalo ni matunda ya ukosefu wa mwanga. Tunajadili ukosefu wa nishati muhimu: Umeme.
Giza lilipofunga akili za watu wa kileleni, wakabaki kuona kwamba mahitaji ya nishati ya umeme ni mwanga tu. Wakabaki kufikiri kwamba kinachohitajika ni kumulika majumba yao na njia zao. Basi.
Hata walipoambiwa kuwa nishati ya umeme inahitajika kwa uzalishaji katika viwanda, akili zao zilikimbilia eneo moja la kuzalisha nishati hiyo: Mabwawa mawili au matatu nchi nzima.
Hata hivyo, katika giza lililofunika akili zao, hakuna aliyefikiria uwezekano wa kupanuka kwa matumizi ya umeme nchini. Kwani wengi waliishi kama watalii – wako mbioni kuondoka ili waende kutumbua walichokwanyua.
Katika hali ya kawaida giza huzaa giza na matunda ya giza ni giza. Akili iliyokumbwa na giza haichochei uwezo wa kufikiri. Hata uwezo wa wachache na akili zao haviwezi kupenya kuta nene za giza lililofunika nchi.
Watu wa kileleni wakawa hawawezi kuona kuwa kila mto usiokauka unaweza kuwa chanzo cha nishati umeme. Wakawa vipofu. Kama hawana uwezo wa kuwekeza, basi wahimize wenye uwezo wafanye hivyo. Hawakufikiri hivyo.
Watu wa kileleni wakawa hawawezi kuona kwamba jua litokalo kila siku ni chanzo muhimu cha nishati. Hawakujua au walipuuza uvunaji nishati umeme kutoka mionzi ya jua, ambao gharama yake ni ndogo.
Wakawa hawaangalii vyanzo vingine kama vile gesi na makaa ya mawe. Gesi na makaa ya mawe ‘vikaozea’ ardhini na wa kileleni wakaendelea kulalama, huku wakiorodhesha wale waliowaita maadui wakuu wa nchi.
Zaidi ya miaka 40 sasa tangu nchi ipate uhuru, watu wa kileleni ndio wanakimbia huku na kule kutafuta vyanzo vya umeme.
Katikati ya mahangaiko haya ambayo hakika siyo makini, lolote linaweza kutendeka. Mikataba dhaifu kama ule wa IPTL ndiyo inaweza kuangamiza nchi ya giza kwa kasi isiyokuwa ya kawaida.
Leo hii nchi imeingia katika uzalishaji wa ainaaina ambao unahitaji nishati umeme. Nishati hiyo haipo. Hata kinachofanyika ni kujaribu kupoza hali mbaya iliyopo lakini si kuweka misingi ya ufumbuzi wa tatizo kwa muda mrefu.
Giza lililokumba akili limeleta giza lenyewe ambalo ni ukosefu wa mwanga na nishati kwa ajili ya uzalishaji katika maeneo mbalimbali.
Giza limesababisha kusimamishwa kwa uzalishaji na pengine kutoanzishwa kwa miradi ambayo ingekuwa muhimu kwa wananchi.
Giza limeleta upungufu mkubwa katika utoaji elimu shuleni na vyuoni. Mafunzo kwa njia ya mazoezi yamesimama na wanafunzi na walimu wamekuwa ‘kijiweni.’
Giza limekuza giza la akili na watu wa kileleni wanaendelea kufanya hali hii kuwa gumzo kuu la kisiasa badala ya kuhakikisha kwamba mgogoro huu unaondoka.
Nasikitika kwamba madhara ya giza yamekuwa makubwa mno. Haitakuwa ajabu kuamka asubuhi na kukuka mitaa inapiga miayo – haina magazeti – na baadhi ya vituo vya redio na televisheni vikiwa kimya – vimetekwa na giza.
Nasikitika kwamba, kwa mwendo huu, na iwapo hali haitabadilika, maeneo yote yanayotegemea nishati yatakwama na kizazi kipya kinachozaliwa gizani hakitaishi kuona nuru na uhuru wa akili zake.
Na hapo ujinga utakuwa umetukuzwa. Utakuwa umeapishwa kuchukua madaraka yote nchini. Utakuwa umeasisi udhibiti mkali zaidi kwa kizazi chote na vingine vijavyo.
kankugambile@yahoo.com