WATALAAMU nchini wametakiwa kuwa macho na baadhi ya kampuni binafsi zinazotaka kutumia utaalamu wao kuombea fedha katika mashirika ya kimataifa.
Tahadhari hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Dk. Abel Gibbe alipokuwa akizungumza katika Ofisi za Tanzania Daima, Dar es Salaam.
Dk. Gibbe ambaye anadai kutapeliwa na Kampuni ya ED-Consult (T) Ltd. ya jijini Dar es Salaam, alisema alifuatwa na watendaji watatu wa kampuni hiyo ambao walimtaka awape cheti cha maelezo yake binafsi (CV) ili wayatumie kushindania mradi wa kimataifa wenye thamani ya dola 100,000.
“Walinifuata nyumbani kwangu Mbezi, wakaniomba CV yangu, ati waitumie kushindania mradi wa kuendesha utafiti na kutoa mafunzo ya kuimarisha elimu katika programu ya Education II Project Zanzibar.
“Walidai mradi huo utafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia African Development Bank, wakaniahidi kunilipa sh milioni 3 kila mwezi kwa vile mimi ndiye ningeendesha mradi huo, nikakubaliana nao, niliwapa CV yangu, na nimefanya kazi katika mradi huo, lakini wamenitapeli,” alilalamika Dk. Gibbe.
Alisema kwa kutumia CV yake, kampuni hiyo kwa kushirikiana na kampuni moja ya India ya Education Consultants India Ltd walifanikiwa kuupata mradi ambao ulianza kufanya kazi Oktoba 2000.
Alisema alifanya kazi Zanzibar kwa muda wa miezi saba kwa gharama zake baada ya Ed- Consult kutoa malalamiko ya mara kwa mara kwake kuwa haina fedha.
“Kwa muda wote niliofanya kazi Zanzibar walinipa sh 930,000 fedha nyingine wananizungusha wakati ninajua wamekwishalipwa.
“Hawa ni watu hatari, wametumia CV yangu na elimu yangu katika mradi wao, badala ya kunilipa stahili yangu wamenitapeli, wananizungusha, shida yao ilikuwa kunitumia kama chombo cha kupatia fedha kisha wanitelekeze.
“Kibaya zaidi, kwa sababu niliwaamini, nilitumia fedha zangu nyingi katika kukamilisha mradi huo, akiba yangu imebakia kidogo na nina familia inanitegemea, ninachanganyikiwa,” alisema Dk. Gibbe.
Alitoa tahadhari kwa wataalamu wengine kuwa makini na kampuni zinazoendesha mambo yake kiujanja janja kwa sababu zinaweza kuwaita na kutumia vyeti vyao katika njia mbaya au kuwatapeli.