MKUU wa Mkoa (RC) wa Kigoma, Joseph Simbakalia, amesema kuwa uchakavu wa miundombinu ya barabara na reli kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, ni kikwazo kikubwa cha maendeleo kwa kuufanya mkoa huo kuwa kama kisiwa.
Alibainisha hayo baada ya ziara yake ya siku moja ya kujifunza na kutambua mambo mbalimbali yanayoukwamisha mkoa huo kiuchumi. Amegundua udhaifu na ubovu wa miundombinu ya reli na barabara kuwa chanzo kikuu cha kudumaza uchumi wa Kigoma.
Alisema hata bandari ya Kigoma imekuwa ikikosa tija na kusababisha wateja wake kuikimbia kutokana na mizigo yao inayosafirishwa kwa njia ya reli kufika ikiwa imechelewa na ikiwa katika mafungu mafungu, jambo linalosababisha hasara kubwa kwa wamiliki wa mizigo na bidhaa husika.
Alisema wateja wengi wanaotoka nje ya nchi, hususan Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Rwanda na Burundi wamelazimika kubadili njia za usafirishaji ambako wameanza kutumia bandari ya Mombasa nchini Kenya na kupitia Uganda kabla ya kuingia katika nchi zao.
Simbakalia alisema ili mkoa wowote upate tija na kupiga hatua katika maendeleo, ni lazima uboreshe mahitaji ya chakula, miundombinu na nishati ambapo kwa mkoa huo una hazina ya kutosha ya chakula jambo ambalo limeufanya kuwa mkoa pekee ambao haujawahi kuomba chakula serikalini tangu uhuru.
Alisema miundombinu na nishati vikiboreshwa, ni wazi mkoa utapiga hatua kubwa kiuchumi na kuishinda mikoa mingi nchini inayoonekana imeendelea jambo ambalo pia litapunguza mfumuko wa bei unaoendelea kupanda kiholela.