logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumatatu, 11 septemba 2006
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1
MARSH: Lulu iliyoibuliwa ‘machimboni’ na Ndolanga
Deodatus Mkuchu


ANA jina la kisoka hasa, majina yake yote matatu, yaani la kwanza, la pili na hata la ukoo, ni majina ambayo yako kwenye medani ya soka.

Huyo si mwingine, ni Marsh Marcia Sylvestre. Jina lake kwa sasa, si jipya masikioni na hata machoni mwa Watanzania hususan kwa wale wapenzi na mashabiki wa soka.

Wengine watakuwa wamemsikia au kumwona wakati akicheza soka katika timu mbalimbali nchini na wapo pia waliomwona au kumsikia akiwa na timu ya Tanzania ya vijana wa chini ya miaka 17, - Serengeti Boys, kama msaidizi wa Kocha Mkuu, Abdallah ‘King’ Kibaden.

Marsh ni mwanasoka halisi kutokana na mchango wake katika mchezo huo akiwa mchezaji na sasa ni kocha ambaye yuko Burundi, akiwa na timu ya Tanzania inayoshiriki michuano ya Challenge kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes).

Mbali ya kufundisha klabu kadha wa kadha za madaraja mbalimbali, Marsh kwa sasa ni kocha mkuu wa timu ya Kagera Sugar iliyoko Ligi Kuu ya Vodacom.

Huko Kagera amemwachia jahazi msaidizi wake, Mrage wa Kabange, akiendeleza yale yote ya Marsh, ikiwa ni siku chache tu tangu walipoibebesha Kagera Sugar ubingwa wa michuano ya Tusker, akiifunga Simba katika mechi ya fainali.

Alichokifanya Marsh na Kabange si kutwaa ubingwa pekee, bali kuweka rekodi mbili, kwanza kuipokonya Simba kwa mara ya kwanza taji hilo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001.

Pili, kuweka rekodi ya kipekee ya Kagera Sugar kushiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo na kutwaa ubingwa.

Mbali ya Simba iliyolambishwa mabao 2-1 katika fainali, nyingine zilizoshiriki ni ZANACO ya Zambia, na Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Polisi ya Uganda.

Nyingine ni Yanga na Moro United ambazo zilifungashwa virago baada ya kushindwa kuhimili kishindo cha michuano hiyo.

Kagera Sugar ilianza kuonyesha matumaini baada ya kuinyuka ZANACO na Polisi Uganda kabla ya kuwaduwaza wengi kwa kuitandika Simba katika fainali.

Ingawa wapo wanaomfahamu Marsh kutoka kitambo, wapo pia waliomfahamu akiwa na kikosi cha Serengeti Boys ambacho mwaka 2004, kilipata nafasi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika nchini Gambia, ingawa hakikwenda.

Hiyo ilitokana na kukumbwa na mkasa kiutawala baada ya mchezaji wake Nurdin Bakari kuonekana amezaliwa katika miaka miwili tofauti. Kwa kifupi kulikuwa na utata wa umri.

Katika fomu za Simba zilizokwenda Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ajili ya ushiriki wa Ligi ya Mabingwa, zilionyesha amezaliwa mwaka 1983 na zilizotumwa kwa ajili ya ushiriki wa michuano ya vijana, zilionyesha amezaliwa mwaka 1988.

Kosa Hili la kiutawala, lilitosha kuiadhibu Serengeti Boys kutoshiriki fainali hizo licha ya kufuzu na kuifungia nchi kwa miaka miwili kutoshiriki michuano hiyo ili kuwa funzo.

Baada ya mkasa huo, Marsh bado akabaki na kofia mbili za kitaifa ambazo ni kocha msaidizi wa Serengeti Boys na Ngorongoro Heroes na wakati huohuo, Kagera Sugar, wakamchukua na kuwa kocha mkuu.

Akiwa na Kagera Sugar, Marsh amefanikiwa kusuka kikosi cha wachezaji wasio na majina makubwa, lakini wenye vipaji, moyo na ari kubwa katika majukumu waliyonayo na hii ni kati ya siri kubwa ya mafanikio ya timu hii.

Licha ya ugeni wake katika michuano ya Tusker, Kagera Sugar imeonyesha soka ya hali ya juu na kuacha gumzo kubwa, si kutokana na kutwaa ubingwa tu, bali kiwango cha kutisha kilichoonyeshwa na timu hiyo.

Ushujaa huo wa kutwaa taji la Tusker ambalo lilizoea kutua Mtaa wa Msimbazi kila mwaka tangu mwaka 2001, umeifanya Kagera Sugar kuheshimika kisoka baada ya kutafuna mfupa uliomshinda Yanga, Mtibwa na Moro United ambazo kwa nyakati tofauti zimeshiriki michuano hiyo.

Katika mahojiano na Tanzania Daima yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Marsh anasema, siri kubwa ya mafanikio kwa timu yake, ni nidhamu binafsi na ile ya uchezaji iliyoko kwa wachezaji wa timu hiyo.

Anasema, hiyo ni silaha kubwa ya mchezaji kwani chini ya msingi huo, mchezaji ama timu ni lazima ipate mafanikio, kwani kila mmoja huzingatia kilichomfanya awepo katika timu.

Marsh, kocha asiye na makuu anasema, chini ya mwamvuli huo, wachezaji wameweza kujituma kwa nguvu zote na uadilifu mkubwa katika mashindano hayo.

Anasema silaha hiyo pamoja na ushirikiano mkubwa kutoka kwa uongozi wa timu hiyo, kumewafanya wachezaji waone mafanikio ya timu ni yao pia.

Alikotokea Marsh:

Akiwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbugani, jijini Mwanza, kati ya mwaka 1972 hadi 1977, aliweza kuwamo katika kikosi cha shule na kushiriki mashindano ya ngazi mbalimbali ya shule za msingi (UMITASHUMTA).

Marsh anawakumbuka baadhi ya wachezaji aliokuwanao katika mashindano hayo, ni Athumani Juma Chama aliyewahi kuwika na timu ya Tanzania (Taifa Stars) pamoja na Yanga.

Wengine ni Halfan Ngassa aliyewahi kuwika na Pamba, Jumanne Ntambi ambaye kwa sasa ni Kocha Mkuu wa Kahama United ya Shinyanga, Isaac Mwakatika, Abbas Magongo na Thobias Nkoma.

Marsh alipata elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Lake, na akiwa hapo, aliweza kuwamo katika kikosi cha shule kilichoshiriki mashindano mbalimbali ya shule za sekondari (UMISETTA).

Kati ya wachezaji aliokuwa nao ni Rwemaho Mkama, Ibrahim Magongo, Ahmed Amasha, Venance Mwamoto na alipohitimu kidato cha nne, alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa Mafinga.

Kutokana na kipaji chake cha soka, alipofika Mafinga, siku iliyofuata kukawa na mechi, alipopewa namba, alionyesha kiwango kikubwa na siku ya tatu akahamishiwa Makao Makuu ya JKT, Dar es Salaam.

Akiwa JKT Dar es Salaam, mwaka 1984, alikuwa ni kati ya wachezaji waliounda kikosi cha soka Makao Makuu akiwa na wachezaji kama Dennis Mdoe liyewahi kukipiga Yanga kabla ya kutimkia Botswana. Pia alikuwa naye Selemani Mateleka. Kama si kuwekewa ngumu na Jeshi, angeweza kuichezea Simba, kwani Simba ilimwita yeye na Adolf Kondo.

“Tuliitwa na Simba kwa ajili ya kusajiliwa, binafsi niliwekewa ngumu na uongozi wa jeshi, hivyo Simba kufanikiwa kumtwaa Adolf Kondo,” anasema Marsh.

Anasema, Simba iliwaona katika Kombe la Taifa mwaka huo akiwa katika kikosi cha Mkoa wa Dar es Salaam, Mzizima United, iliyokuwa chini ya Nahodha, Ramadhani Lenny.

Baadhi ya wachezaji anaowakumbuka katika kikosi cha Mzizima ni Yassin Abuu Napili, Athanas Michael, Saleh Umbopa, Aboubakar Salum ‘Sure Boy’, Muhidin Sisso, Moses Mkandawile, Omar Pazi na wengineo.

Kutokana na kipaji chake, mwaka 1886 hadi 1988, alikuwa mfanyakazi na mchezaji wa Kampuni ya Biashara Mkoa (RTC), akiwa Mara na kuwa kati ya wachezaji mahiri wa timu hiyo.

Kutokana na kipaji chake, Marsh alihamishiwa katika kikosi cha timu ya RTC Kagera na kuwa kati ya wachezaji wa timu hiyo iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu wakati huo ikiitwa Daraja la Kwanza.

Marsh anasema baada ya kung’ara na timu hiyo kwa siku kadhaa, alirejeshwa tena Mara ambako alikaa kwa muda na mwaka 1997 alikwenda nchini Kenya kuichezea klabu ya Breweries.

Anasema alikaribishwa na Kocha James Siang’a ambaye kwa sasa anainoa Mtibwa Sugar ya Morogoro. Kabla ya Kujiunga na Mtibwa Sugar, Siang’a aliifundisha kwa mafanikio makubwa Simba kuanzia mwaka 2001 hadi 2004.

Mbali ya kuibebesha Simba mataji ya Ligi Kuu Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kwa vipindi tofauti, pia aliiwezesha Simba kuingia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003.

Pamoja na mafanikio hayo, Siang’a aliondoka huku bado akiwa kipenzi kwa wanachama na wapenzi wa Simba na kujiunga na Moro United kabla ya kwenda Mtibwa Sugar.

Marsh anasema, hakuweza kukaa muda mrefu Breweries kwani mwaka 1998, alirejea jijini Mwanza na kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Toto Afrika iliyokuwa Ligi Kuu.

Kati ya mechi anayoikumbuka akiwa na Toto Afrika ni dhidi ya Yanga katika Uwanja wa Taifa ambapo timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

“Mechi hii ilikuwa ni baada tu ya Yanga kucheza na Kwara United ya Nigeria katika michuano ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, nakumbuka wakati huo Yanga ilikuwa na mgogoro,” anasema.

Msimu uliofuata, akajiunga na timu ya Kahama United ya Shinyanga wakati huo ikiitwa 82 Rangers na kufanikiwa kuipandisha kutoka Ligi Daraja la Kwanza hadi Ligi Kuu.

Anawakumbuka baadhi ya wachezaji waliokuwamo katika kikosi cha timu hiyo ni Karume Songolo, Madata Lubigisa, Joseph Mwanakusha, Ally Mrisho na wengineo.

Mwanzoni mwa mwaka 2002, akajiunga na timu ya Geita Gold Mine iliyokuwa Ligi Daraja la Nne na aliipandisha hadi daraja la kwanza, na kuweza kuing’arisha timu hiyo na kuishia chupuchupu kwenda Ligi Kuu ya Vodacom.

Anakumbuka mechi ya kuamua timu ipi iende Ligi Kuu, ilizikutanisha Kahama Gold Mine FC na Kagera Sugar anayoifundisha kwa sasa.

“Naikumbuka mechi ile, ilikuwa ngumu sana, walifanikiwa kupita lakini kwa mbinde kutokana na soka ilikuwa ikipigwa katika harakati za kuwenda Ligi Kuu msimu wa 2005” anasema.

Marsh anasema, akiwa na Geita Gold Mine FC, ndipo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), Muhidin Ndolanga, alimwona na kuvutiwa na kipaji chake.

“Nitakuwa ni mchoyo wa fadhila kama sitamtaja Mzee Ndolanga, huyu ndiye aliyenichomoa na kuniita kwa mara ya kwanza katika timu ya vijana ya taifa chini ya miaka 17, Serengeti Boys, anasema.

“Nakumbuka alikuwa amekuja kufungua mtihani wa waamuzi wa Ligi Kuu ambao mwaka huo 2004, ulifanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza,” anasema na kuongeza:

“Alipofika uwanjani hapo, nilikuwa katika mazoezi na timu yangu ya vijana wadogo, baada ya kuangalia mazoezi yale, akamuuliza Jumbe Magati, nani kocha wa timu ile?

“Magati (Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mwanza), akamweleza ni Marsh. Akasema nipatiwe mafunzo zaidi kwa kile alichosema nina kipaji,” anasema na kuongeza:

“Magati akamweleza Ndolanga kuwa kipindi hicho nilikuwa na stashahada ya juu ya ukocha, Ndolanga akaahidi kuwa angewasiliana na Katibu Mkuu (Michael Wambura).”

Marsh anasema mbali ya Ndolanga, pia anawashukuru pia Magati na Wambura, kwani baada ya kuelezwa na Ndolanga kuhusu yeye, alikubali na kuidhinisha kuwa awe kocha msaidizi wa Serengeti Boys.

Mwingine aliyeunga mkono kuhusu ujio wake Serengeti Boys ni Festo Mkemwa, aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Tabora na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya FAT wakati huo na bosi wa soka wa Mkoa wa Kagera, Amir Roshan.

Anasema, atakuwa mchoyo wa fadhila kama atashindwa kuwashukuru watu hao, kwani anaamini wako makocha wengi wakongwe na wazuri, zaidi yake, lakini akaonekana na kupewa nafasi.

Anazungumziaje Mkasa wa Serengeti Boys?

Marsh akiwa chini ya Abdallah ‘King Mputa’ Kibadeni, waliiwezesha Serengeti Boys kupata tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana nchini Gambia.

Anasema, jambo ambalo hatakuja kulisahau, ni mkasa huo kwa kusema, nafasi hiyo ilikuwa ni fursa ya wachezaji na makocha na soka ya Tanzania kwa ujumla kupata chati.

“Ingawa ilikuwa ni mshtuko mkubwa kwa Watanzania, lakini kwa wachezaji na makocha ilikuwa zaidi, kwani baada ya kupata nafasi ile, hatua iliyokuwa ikifuata ni kuonyesha kiwango nje ya mipaka,” anasema.

Marsh anasema hilo limeigharimu soka ya Tanzania, kuna haja ya kujifunza kutokana na hilo, ingawa mzigo wa lawama za sakata hilo ulionekana kuelekezwa kwa makocha.

“Katika sakata la Serengeti, usaliti ulikuwa mkubwa, tulipopata nafasi ya kucheza fainali za Gambia, tulipongezwa.. mkasa ulipoibuka, tukasusiwa mzigo,” anasema.

Anasema, suluhisho na tatizo lililojitokeza ni kuwapo kwa mipango bora na endelevu katika kuibua na kuendeleza soka ya vijana, kwani kwa kufanya hivyo, hata kiwango cha soka kitakua.

Mbali ya kuwa kocha msaidizi wa Serengeti Boys, Agosti 8, mwaka 2005, Marsh aliteuliwa kuwa msaidizi wa John Simkoko wa timu ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes.

Heroes ilishiriki michuano ya Chalenji ya vijana wa umri huo iliyofanyika visiwani Zanzibar maarufu kama Karume Cup na kukamata nafasi ya nne.

Akiwa na Kagera Sugar msimu huu, Marsh alifanikiwa kuongoza kwa miezi miwili Ligi Kuu ya Vodacom iliyoanza Februari 25 kabla ya kupokwa na Yanga.

Kuhusu ubingwa wa michuano ya Tusker kwa timu yake, Marsh anasema, siri kubwa ya mafanikio ni kujituma kwa wachezaji, jitihada za makocha na uongozi bora wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera.

“Siri kubwa ni kila mmoja kwa nafasi yake kujua na kutekeleza wajibu wake ipasavyo katika kusaka mafanikio, ukianzia kwa wachezaji, makocha na uongozi mzima wa Kagera Sugar,” anasema.

Iwapo kama anafikiria siku moja kufundisha mojawapo ya timu kongwe za Simba ama Yanga, Marsh anasema, ukocha kama taaluma nyingine, hilo halina tatizo.

Anasema, kutokana na mazingira na staili ya usimamizi wa timu hizo kongwe, inamwia ugumu kwa sababu, hayuko tayari kufundisha timu ambayo hakuisajili.

“Kitendo cha kocha kufanyiwa usajili, ni kinyume, badala yake kocha aachwe kuifanya kazi hiyo huku uongozi wa klabu husika ukiwajibika kwa gharama za wachezaji waliopendekezwa,” anasema.

Marsh anasema, kitendo cha uongozi kusajili timu na kumkabidhi kocha, ikitokea timu ikafanya vibaya, itakuwa ni uonevu kumlaumu kocha.

“Kocha ndiye anajua ni wachezaji wa aina gani anawahitaji katika kikosi chake, hivyo kitendo cha kukabidhiwa timu asiyoisajili, humpa wakati mgumu kocha katika utendaji wake,” anasema.

Anabainisha sababu hiyo na nyinginezo nyingi, ndizo zilimfanya asijiunge na timu ya Yanga msimu wa mwaka 2005, licha ya kumhitaji kabla ya kumrejesha Jack Chamangwana.

Marsh anasema kuwa kocha wa timu kama Simba ama Yanga ni fahari na sifa, lakini vyote hivyo havitakuwapo bila timu husika kufanya vema ambako huchangiwa na mambo kadha wa kadha.

Marsh, kocha asiye na makuu, anasema siri kubwa ya mafanikio yake kiufundishaji, ni kutokana na utayari wake wa kutaka kujifunza kwa wengine, kukubali ushauri na kuwachukulia wachezaji wote kuwa ni sawa na ndugu.

Anasema chini ya mwamvuli huu, mchezaji hujituma ili asimwangushe kocha wake, viongozi wake na pia kwa masilahi yake na timu kwa ujumla.

Anadokeza kuwa katika michuano ya Tusker, waliwafunda wachezaji wake kwamba, timu zote zinazoonekana ni kubwa kama Simba, ZANACO, Polisi Uganda, Yanga, Moro United ni majina tu.

“Tuliwajenga wachezaji wetu kwamba, timu zote zilizoko katika michuano ya Tusker ni majina makubwa tu, lakini wachezaji ni wa kawaida ambao wanaweza kuwamudu na kuwazidi,” anasema.

h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2006 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa mkwepu na makunganya, slp 15261, dar es salaam, tanzania
simu +255-22-2120604  •  faksi +255-22-2126234