logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumatatu, 11 septemba 2006
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1
Kwa juhudi za pamoja, Stars itacheza Ghana
Leodegar Tenga


TIMU yetu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, imetutoa kimasomaso wapenzi wa soka na Watanzania kwa jumla kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Burkina Faso katika mchezo wa kwanza wa kundi la saba la mashindano ya kuwania kucheza fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Ghana mwaka 2008.

Mchezo huo ulifanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Jumamosi ya Septemba 2, mwaka huu.

Ushindi ule ni mkubwa, wa kwanza katika mashindano haya kwa kipindi cha miaka 9 iliyopita.

Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza vijana wetu na viongozi wao, Kocha Mkuu, Marcio Maximo, wasaidizi wake, meneja na daktari wa timu kwa ushindi huo.

Ushindi wa Taifa Stars ulishuhudiwa na maelfu ya watazamaji waliojazana Uwanja wa Taifa wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.

Ulikuwa ni umati mkubwa kuliko wowote uliowahi kuishabikia timu yetu ya taifa katika historia ya nchi yetu. Ushabiki na ushangiliaji huchangia kwa kiasi kikubwa kuitia nguvu timu kufanya vizuri.

Katika ulimwengu wa mpira ushangiliaji ni nyenzo muhimu ya ushindi na huhesabika kama mchezaji wa ziada; mchezaji wa kumi na mbili wa timu inayoshabikiwa.

Hapana shaka kuwa siku ya Jumamosi timu yetu ya taifa ilikuwa na mchezaji wa ziada.

Kwa niaba ya TFF napenda kumshukuru Rais wetu na wote waliofika uwanjani kuitia shime timu yetu.

Nawashukuru pia wananchi wote waliokuwa wakiiombea dua timu yao japokuwa hawakupata fursa ya kufika uwanjani.

Kuhamasika kwa Watanzania kuishangilia na kuichangia timu hakukutokea kwa bahati. Kumetokana na mkakati madhudhuti uliopangwa na kutekelezwa kikamilifu na viongozi wetu na wadau wa mpira.

Kinara wa kampeni hii ni Rais Kikwete, ambaye ni mpenzi mkubwa wa soka na michezo mingine. Alianza kwa kutoa ahadi ya kuiendeleza soka nchini kwa kutupatia kocha wa timu ya taifa, na akatimiza ahadi hiyo kwa kutupatia Kocha Marcio Maximo na msaidizi wake.

Akatoa changamoto kwa TFF na wadau wake wahakikishe kuwa nchi yetu inashiriki katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Ghana mwaka 2008.

Hakuishia hapo. Siku tano kabla ya mchezo, rais alifika Uwanja wa Karume kuwaona vijana wakifanya mazoezi na kuzungumza na vijana.

Akawahakikishia kuwa serikali ipo nyuma yao na kuahidi kuwasaidia kwa hali na mali. Tendo hilo la kihistoria likafuatiwa na rais kuwahimiza wananchi wajitokeze kuichangia na kuishangilia timu yao katika hotuba yake kwa taifa ya mwisho wa mwezi Agosti.

Mwishowe, yeye mwenyewe akafika uwanjani kuishangilia timu yake ya taifa. Tumefaidika na kufarijika kwa kiasi kikubwa mno kwa msaada wake.

Amewasha moto. Wajibu wetu sisi viongozi na wadau wa soka ni kuhakikisha kuwa moto huo hauzimiki. Shukurani za pekee zimfikie rais wetu.

Tunapenda pia kutoa shukurani kwa uongozi wa Jiji la Dar es Salaam wakiongozwa na Meya wa Jiji, Adam Kimbisa, pamoja na Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwatembelea vijana na kuchukua jukumu la kuwahamasisha wakazi wa jiji kufika uwanjani kuishangilia timu yao.

Tunamshukuru Amina Chifupa kwa kuwatia shime vijana na kuwazawadia sh 2,080,000. Tunamshukuru Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho kwa kuitembelea timu ya taifa, kutoa mchango wa sh milioni 4 kwa wachezaji na kufika Uwanja wa Taifa kuishangilia timu ya taifa.

Tunapenda pia kuwashukuru Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF; Augustino Mrema, Mwenyekiti wa TLP na James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi kwa kujumuika na wapenzi wa soka katika kuishangilia Taifa Stars.

Kujumuika kwao ni kielelezo cha uzalendo na mshikamano uliopo miongoni mwa Watanzania katika masuala ya kitaifa. Tunauenzi mchango wao.

Tunaushukuru pia uongozi wa Benki ya Posta Tanzania (TPB), kwa kuitembelea kambi ya timu ya taifa na kutoa motisha ya sh 1,500,000 kwa wachezaji.

Msaidizi wa Mzee Kawawa aliwasiliana nasi na kutueleza kuwa Mzee Kawawa anatuma salamu zake kwa vijana na angependa kufika uwanjani.

Tulimweleza kuwa tungeshukuru kuwa naye, lakini asipofanikiwa salamu zake zingetosha na kwamba vijana wangepambana wakijua kuwa mzee wao yupo nyuma yao. Tunamshukuru sana Mzee Kawawa kwa kututakia heri.

Pamoja na hao walijitokeza viongozi wengi wa serikali, ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, waheshimiwa wabunge kadhaa, na wadau waliojitolea kuchangia na kuuhamasisha umma kwa ajili ya mchezo huo akiwano Shy-Rose Bhanji aliyetoa sh 500,000.

Walifanya hivyo kwa kuwashawishi wananchi waishangilie timu yao na wenyewe kufika uwanjani kushuhudia pambano hilo. Tunawashukuru kwa mchango wao.

Mchango uliotolewa na vyombo vya habari hauna kifani. Nimekuwa nikivishukuru vyombo vyetu vya habari kwa mchango wake katika harakati tulizo nazo za kukuza kiwango chetu cha soka na ninapenda tena kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa kazi nzuri walioifanya kwa ajili ya pambano hilo.

Moja ya mambo muhimu yaliyofanywa na waandishi wetu wa habari ni kujitolea kufanya kazi ya kuuhamasisha umma ujitokeze kuishangilia timu yetu ya taifa.

Waliifanya kazi hiyo baada ya kuunda kamati inayowajumuisha wao wenyewe, viongozi wa klabu na wadau wengine ya kusimamia kampeni hiyo. Kazi walioifanya ni ya kupigiwa mfano. Tunawashukuru sana.

Ni imani yangu kuwa ushirikiano huu ni matunda ya sera ya kujenga na kudumisha uhusiano mzuri baina ya TFF na wadau wake wakuu.

TFF imekuwa na ushirikiano wa karibu na wizara yetu ya michezo na vyombo vya serikali. TFF imejenga uhusiano wa karibu na wanachama wake na wadau wake wakuu wakiwemo wafadhili wa soka.

Tunatoa shukurani maalumu kwa Waziri wetu, Muhammed Seif Khatib na manaibu waziri wake, Joel Bendera na Dk. Emmanuel Nchimbi pamoja na viongozi wengine wa wizara na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa msaada na ushirikiano wao.

Tunapenda pia kuwashukuru viongozi wetu wa mikoa na klabu. Kwa wadhamini na wafadhili wa soka - Vodacom, Coca Cola, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), METL, TIOT, IPP, Quality Group, Cargo Star na wengineo; tunasema asante kwa mchango wenu.

Nina hakika kuwa mshikamano na utulivu uliopo ndiyo unaomtia moyo Rais Kikwete kutusaidia na wadau wengine kuwa na imani na TFF. TFF itahakikisha kuwa ushirikiano huu unadumishwa.

Baada ya kutoa shukrani kwa wote waliochangia kupatikana ushindi katika mchezo wetu na Burkina Faso, ni vyema nikakumbusha kuwa tulichofanikiwa ni kuvuka hatua ya kwanza.

Ili kushiriki katika fainali za Afrika zitakazofanyika Ghana mwaka 2008, tuna hatua nyingine tano za kupita. Tunachotakiwa kufanya sasa ni kuendeleza na kuudumisha ushirikiano huu.

Ushindi huo uwe chachu ya kufanya vizuri zaidi. Waswahili wanasema ‘siku njema uonekana asubuhi’. Sisi tumeanza vyema, lakini tusilale wala kupumzika. Tuimarishe pale tulipofanya vizuri na tujikosoe pale palipokuwa na udhaifu.

Ikumbukwe kuwa ushindi dhidi ya Burkina Faso utawazindua wengine waliokuwa wakiichukulia Taifa Stars kuwa ni timu dhaifu na kuwafanya wajizatiti tutakapokutana nao.

Kwa sababu hiyo hatuna budi tujiandae vizuri zaidi kwa vile tuna hakika ya kukutana na ushindani mkubwa zaidi. Tuendeleze utamaduni mzuri tuliouanzisha wa kuishabikia timu yetu ya taifa na kuichangia ili ifanye vizuri.

Wachezaji wetu wanapaswa kutambua kuwa kazi iliyo mbele yetu ni kubwa na kwamba wanawajibika kujituma zaidi ya walivyofanya katika mchezo wetu na Burkina Faso.

Mchezo unafuata utakuwa dhidi ya Msumbiji na utachezwa kwao kati ya Oktoba 6 hadi 8. Kocha ametoa mapumzika ya wiki mbili.

Timu itarejea kambini mara baada ya hapo, hivyo itakuwa kambini kwa wiki tatu kabla ya mchezo. Katika kipindi hicho timu yetu inatarajiwa kupata angalau mchezo mmoja wa kimataifa wa kirafiki.

Hii itategemea maoni ya kocha na upatikanaji wa timu za kucheza nazo. Kocha wa timu ya taifa amepewa jukumu la kuiimarisha timu hiyo.

Yupo huru kuijenga timu hiyo kadiri atakavyoona inafaa. Jukumu la TFF na wadau wengine ni kumsaidia afanye kazi yake vizuri, ikiwa ni pamoja na kumpa ushauri bila ya kumwingilia katika uteuzi wake.

Atapewa fursa ya kutembea mikoani kuangalia wachezaji wanaofaa kwa timu ya taifa. Tumefarijika na kitendo cha serikali kuunda Kamati ya Operesheni Ushindi.

Kuundwa kwa kamati hii ya kitaifa itasaidia sana katika jitihada ya kuuhamasisha umma uchangie timu ya taifa. Dhana ya kuujumuisha umma katika kuihudumia timu yao ya taifa badala ya kuiachia TFF na serikali peke yake, ni moja ya mihimili muhimu ya programu ya TFF ya kuiendeleleza timu ya taifa. Tunaishukuru serikali kwa ushirikiano wake.

Tungependa kuchukua nafasi hii kuwapongeza wajumbe wa kamati hiyo na Mohammed Dewji kwa kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo. TFF inawahakikishia ushirikiano wake katika kufanikisha utendaji wa kamati hiyo.

Baada ya kuundwa kwa kamati hiyo, michango na misaada yote itakayotolewa kwa ajili ya timu za taifa itaratibiwa na kamati hii.

Mwelekeo tunaokwenda nao wa ushirikiano miongoni mwa wadau wa soka ni mzuri. Nina matumaini makubwa ya mafanikio siku za usoni.

Leodegar Tenga ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

 

h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2006 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa mkwepu na makunganya, slp 15261, dar es salaam, tanzania
simu +255-22-2120604  •  faksi +255-22-2126234