BAADA ya kuifyatua Burkina Faso, matumaini ya Watanzania yameanza kuwa juu kwa Taifa Stars, timu ya soka ya Tanzania iliyotumbukiza kwa mbwembwe kete yake katika michuano ya awali ya Kombe la Mataifa ya Afrika ikiwania kufuzu kwa fainali za mwaka 2008, nchini Ghana.
Umekuwa mwanzo mzuri kwa Stars, huku ikiwa na kazi nyingine pevu mbele ya Msumbiji na Senegal ambazo kama Stars, kila moja ina ndoto za kunyakua tiketi pekee ya Kundi la Saba la michuano hiyo.
Ngoma dhidi ya Msumbiji itapigwa ndai ya wiki ya kwanza ya Oktoba, kati ya Septemba 6 na 8 nchini Msumbiji, ambako wenyeji wana hasira za kupokea kichapo cha 2-0 kutoka kwa Senegal.
Mazingira ya timu hizi mbili yanayaweka mazingira ya mchezo huo kuwa ya presha kubwa kwa pande zote, Stars ikitaka kuendeleza rekodi huku Msumbiji ikitaka kufukuza jinamizi la kushindwa.
Joto la presha hiyo limeshaingia kwa makocha na wachezaji wa timu hizo, huku Mbrazil Marcio Maximo wa Tanzania akitaka apewe pambano la kimataifa dhidi ya Uganda jioni ya Septemba 30 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, siku ambayo watani wa jadi katika soka nchini, Simba na Yanga wamepangwa kukipiga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom.
Msimamo wa kocha huyo huenda ukapokewa kwa shingo upande na wanazi wa klabu hizi zinazoongoza kuwa na mashabiki wa soka katika kila pembe ya Tanzania, ingawa pia ni vinara wa ubabaishaji.
Kama wadau wa michezo nchini, tunadhani, pamoja na Maximo kuingilia ratiba ya ligi, kama atafanikiwa kupata mchezo, apewe nafasi na aungwe mkono, lengo likiwa kuiimarisha Taifa Stars kabla ya kuingia vitani Msumbiji.
Tunamuunga mkono katika hili tukiamini kwamba, ratiba ya Simba na Yanga inaweza kusogezwa mbele, ilhali utaifa ukiwekwa mbele zaidi, hasa katika kipindi hiki ambacho kila mpenda michezo nchini ana kiu ya kuona Tanzania inafanya mapinduzi ya kweli katika soka.
Kwa mantiki hiyo, tusimchukulie Maximo kama ‘dikteta’, bali mtu anayeitakia mema Tanzania, ndiyo maana tunaungana naye katika kila juhudi za kuhakikisha anapata ari ya kuirudisha Tanzania katika ramani ya soka ya kimataifa.