WACHIMBAJI wadogo wadogo wa madini wilayani hapa, mkoani Morogoro ambao wana hofu ya kuondolewa katika migodi yao, wametishia kuandamana kwenda Ikulu kupinga hatua ya serikali kuiruhusu Kampuni ya Interstate kuchimba madini katika migodi yao iliyopo katika Kijiji cha Ipanko.
Katibu wa Chama cha Wachimba Madini wilayani hapa (CHAWAMAU), Christoms Msakamba aliiambia Tanzania Daima mjini hapa kuwa, Interstate ilipaswa kupewa eneo jipya la kufanyia utafiti badala ya kupewa eneo hilo la wachimbaji ambalo lilishafanyiwa utafiti na wachimbaji hao wadogo wadogo.
“Sisi hatuna tatizo na mwekezaji huyo, tunataka serikali ituachie maeneo yetu tuliyokwisha yafanyia utafiti, Mahenge kuna maeneo mengi yenye madini, kwanini mwekezaji huyo asipewe eneo lingine?” alihoji Msakamba.
Alisema wana imani kuwa baada ya Kamishna wa Madini, Paul Masanja na ujumbe wake kufika katika Wilaya ya Ulanga kusuluhisha mgogoro kati ya wachimbaji hao na mwekezaji wa Interstate, haki na busara zitatumika kumaliza mgogoro huo.
“Tunashukuru serikali kwa hatua yake ya kuwaleta maofisa wa madini kushuhudia mgogoro huo na kupata bahati ya kuzisikiliza pande zote mbili, hivyo tunaomba watoe maamuzi ya busara vinginevyo tutaandamana hadi Ikulu kuhakikisha haki inatendeka,” alisema.
Naye Azizi Shemetule ambaye aliwahi kugombea ubunge katika jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisisitiza kuwa wako tayari kuandamana na wachimbaji madini hao endapo serikali itamruhusu mwekezaji huyo kuchimba madini katika maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo.
Alisema biashara ya madini kwa vijana hao imekuwa na manufaa makubwa kwao na kuondolewa kwao, ili kumpisha mwekezaji huyo, kutasababisha ukosefu wa ajira na vijana kujiingiza kwenye vitendo vya ujambazi.
Hivi karibuni Wizara ya Nishati na Madini ilituma ujumbe wilayani Ulanga na kuitisha kikao cha pande zote mbili ili kusuluhisha mgogoro huo.
Hata hivyo, ujumbe huo ulioongozwa na Kamishna Masanja, ulipeleka taarifa yake wizarani na wizara inajiandaa kutoa tamko la serikali juu ya nani mwenye uhalali wa kuchimba madini ya spino, katika eneo la Ipanko, Ulanga, Morogoro.