CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), jana kilimchagua mchezaji wa timu ya taifa ya kriketi, Athumani Kamponzi kuwa mwanamichezo bora wa Agosti, mwaka huu.
Hafla ya uteuzi wa mchezaji huyo ilifanyika jana kwenye Mgahawa wa Hadees jijini Dar es Salaam ambako Kamponzi aliwashinda wanamichezo wengine watatu katika mchakato wa kura za baadhi ya waandishi wa habari za michezo Tanzania kutoka vyombo mbalimbali vya habari.
Kamponzi aliyeisaidia timu ya Tanzania kupata tiketi ya kucheza michuano ya dunia na kuwa mchezaji bora wa michuano ya Kanda ya Afrika iliyofanyika jijini Dar es Salaam, alipata kura 112 na kuwabwaga bondia Rogers Mtagwa aliyepata kura 82; Omari Changa wa Kagera Sugar aliyepata kura 74, na Shaun Miller aliyepata kura 67.
Tuzo hizo zinazodhaminiwa na Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, zilianza kutolewa Januari ambako zawadi ya kila mwezi ni sh 100,000. Tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka itafanyika mapema mwakani na zawadi iliyoandaliwa hadi sasa ni sh 300,000.