Mkutano Mkuu wa 14 wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM), unaanza leo mjini Havana, Cuba. MANYERERE JACKTON, anayehudhuria mkutano huo, anaeleza umuhimu wa NAM hata baada ya kumalizika kwa vita baridi.
VITA baridi imemalizika, lakini maudhui ya kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Zisizofungama na Upande Wowote (NAM), bado yako pale pale.
Mmoja waliokuwa viongozi watiifu na watetezi wakuu wa NAM, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, yeye aliweza kuainisha kazi za NAM kwa kuwataja maadui wakuu watatu.
Maadui hao ni ujinga, maradhi na umasikini. Maadui hawa ndiyo wanaopigwa vita na wanachama wa NAM.
Lakini kila vita huwa na chanzo. Ujinga, maradhi na umasikini si maadui waliochipuka tu kwa bahati mbaya. Maadui hawa wamezaliwa, wamelelewa na hatimaye wamepelekwa katika nchi za Kusini.
Ingawa walezi wake wengine wanaweza kuwa huko huko Kusini, lakini ukweli ni kwamba shina la ulezi huu lipo Kaskazini.
Hii ina maana kwamba pamoja na nchi za Kusini kuwa masikini, umasikini huo kwa kiasi kikubwa umechangiwa na sera mahususi za kudumaza maendeleo ya nchi za hizo.
NAM ilianzishwa rasmi mwaka 1961 ikiwa na kazi kubwa ya kupambana na aina zote za dhulma, uonevu, ukoloni mkongwe, ukoloni mamboleo, usawa katika masuala ya uchumi, na kadhalika.
Kwa ufupi, maudhui ya NAM ni kuhakikisha kuwa binadamu walio katika mataifa ya dunia ya tatu, wanapata haki ya kufaidi yale yanayomstahili binadamu.
Suala la ukoloni mkongwe limemalizika. Lakini ukoloni mamboleo bado upo - na sasa umebatizwa jina la utandawazi (globalization).
Dhulma bado ipo. Baada ya kumalizika vita baridi, dunia imegawanyika katika makundi mawili makuu - Kaskazini na Kusini. Katika medani ya uchumi, mataifa ya Kusini yanafanyiwa dhulma ya hali ya juu.
Serikali za mataifa ya Kaskazini, zinatoa rukuzu kwa wakulima wake, jambo linalozidi kuwaumiza wakulima wa Kusini. Pamoja na mbinu hiyo, ni mataifa hayo hayo yanayopanga bei za mazao na maliasili nyingine.
Moja ya mambo ambayo NAM ilikusudia kupambana nayo tangu kuanzishwa kwake, ni hiyo dhulma. Mandhari, dhulma hiyo bado ipo, umuhimu wa NAM unaendelea kuwa pale pale, au zaidi ya hapo mwanzo.
Makubaliano ya Doha kuhusu biashara, yanapaswa kutekelezwa kwa kuangalia athari ambazo mataifa ya Kusini yamekuwa yakizipata.
Sera mbovu za WTO, zimesababisha madhara makubwa mno kwa nchi masikini. Kinachoonekana hapa ni kwa nchi tajiri kuwa na mkakati wa pamoja na kuziumiza nchi masikini.
Nchi wanachama wa NAM zikiacha haya yaendelee, maana yake ni kuwafanya binadamu katika nchi hizo kuwa watumwa na watwana wa mabwana wakubwa - nchi tajiri.
NAM ilidhamiria kupinga unyonyaji uliofanywa na mashirika makubwa ya fedha kama Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), dhidi ya mataifa machanga.
Miaka 45 tangu viongozi waasisi walione tatizo hilo, ukweli bado uko pale pale. Benki ya Dunia na IMF wamekuwa mwiba mkali kwa mataifa machanga. Sera zake mara kadhaa zimekuwa za kuyadidimiza mataifa ya Kusini.
Masharti ya mikopo ni magumu, kiasi kwamba inahatarisha uhuru wa mataifa mengi masikini. Mapambano dhidi ya hali hiyo, bado ni dhima iliyo mbele ya NAM.
Mataifa ya Kusini, hasa ya Asia Mashariki, ambayo kwa kiasi fulani yamekinzana na mashirika hayo ya fedha, zimefanikiwa. Hiyo imekuwa changamoto kwa mataifa mengine, wanachama wa NAM ya kuyafanya yatambue athari za mashirika hayo, na umuhimu wa kuungana katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.
NAM inapinga mfumo wa sasa wa muundo wa Umoja wa Mataifa. Nchi tano pekee - Marekani, Urusi, Uingereza, Ufaransa na China, kuwa na kura ya turufu, hakutoi haki kwa mataifa mengine.
Kudai haki katika muundo wa UN ilikuwa moja ya malengo ya kuanzishwa kwa NAM. Kwa kuwa usawa huo bado haujaonekana, umuhimu wa NAM unaendelea kuwapo hadi hapo itakavyokuwa vinginevyo.
NAM sasa ina nchi wanachama 116; na leo kuna nchi nyingine mbili zinazojiunga na kufanya idadi iwe nchi 118.
Mataifa 118 yakiungana pamoja kudai mabadiliko, bila shaka yanaweza kufanikiwa, hasa ikitiliwa maanani kuwa “umoja ni nguvu, na utengano ni udhaifu”.
Ukoloni mamboleo ambao sasa unaitwa utandawazi, umeziathiri mno nchi za Kusini. Umeziathiri kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, umezidisha ugaidi na kadhalika.
Pamoja na kuukubali, nchi wanachama wa NAM zimekuwa na jukumu mahsusi la kuhakikisha utandawazi unadhibitiwa katika maeneo fulani fulani.
Mathalani, udhibiti wa sinema zinazokiuka maadili ya asili ya mataifa mengi ya Kusini, ni suala muhimu na linalopaswa kushughulikiwa kwa pamoja na nchi wanachama.
Athari za sinema za Kaskazini zimeanza kuonekana kwa kasi ya kutisha. Matumizi ya mihadarati, siyo siri kuwa yanachangiwa mno na uigaji wa vijana wa mambo ya Ulaya na Marekani.
NAM lazima ipambane na hali ya utandawazi ambayo imeifanya iwe soko la bidhaa za Kaskazini. Hili litawezekana tu kwa nchi wanachama kushirikiana katika nyanja za kiuchumi, na kadhalika.
Kutokana na utandawazi, tayari kuna tofauti kubwa ya kipato kati ya mtu na mtu, nchi na nchi, na hata bara kwa bara.
Tofauti hizo zinaigawa wazi wazi Kaskazini na Kusini. Hali hii si ya kuachiwa hivi hivi. Ndiyo maana NAM katika moja ya kazi zake, ni kuhakikisha kuwa dunia inajengwa katika misingi ya usawa, ili hata kama ni suala la tofauti ya kipato kati ya mtu na mtu, au nchi na nchi, basi tofauti hiyo isiwe kubwa sana kama inavyoendelea sasa.
Haya yatawezekana tu kama nchi wanachama wa NAM wataendelea kuwa na sauti moja katika kudai usawa na kufanya kazi kwa pamoja.
Mataifa ya Kaskazini, kwa kutaka nchi za Kusini zitekeleze yale zinayotaka, kama tulivyosema, yametumia mbinu za uonevu kwenye biashara.
Lakini yametumia mbinu au visingizio vya kisiasa, kuziumiza nchi za Kusini. Mara kadhaa yametumia pia vikwazo kama njia mbadala ya kuadabisha mataifa yasiyokubaliana na mfumo wao.
Mwalimu Nyerere katika Mkutano wa NAM uliofanyika Septemba 1-6, 1992, Jakarta, Indonesia, alipata nafasi ya kuhutubia.
Hotuba yake ilijaa wosia mwingi. Na hii ni sehemu ya hotuba yake katika tafsiri isiyo rasmi:
“Nipo mbele yenu nikiwaomba waheshimiwa kwamba badala ya kuruhusu umoja huu ufe, mnapaswa kuupanua na kuuimarisha zaidi.
“Sasa hakuna tena Kaskazini iliyogawanyika, hakuna tena presha kutoka Mashariki au Magharibi, yakaribisheni mataifa yote ya Kusini yaungane nasi ili kwa pamoja tuwe na chombo cha kweli cha ukombozi wa Kusini yote.
“Kwa nini tujiwekee wigo sisi wenyewe kutokana na sababu zetu za kisiasa? Mataifa yote ya Kusini yana matarajio yanayofanana. Tuthubutu kushirikiana pamoja kwa malengo mamoja.
“Kwa sababu hiyo, nina furaha kuona China imepewa hadhi ya kuwa mwalikwa mtazamaji. Kama wengi katika nchi za Kusini, ninatarajia Kusini yenye nguvu pamoja na China ikiwa mwanachama kamili.
“Ni vema nchi za Kusini zikatambua kuwa kumalizika kwa vita baridi, maana yake ni kwamba Kaskazini iliyogawanyika, sasa inaungana.
“Hakuna sababu ya msingi, ya kufanya kumalizika kwa mgawanyiko wa matajiri, usababishe mgawanyiko miongoni mwa masikini.” Mwisho.
Kwa viongozi waliokubali kuanzisha NAM, sababu za kuwapo kwake bado zipo, na kwa kweli sasa zinazidi kuwapo.
Bila kuwa na sauti moja, Marekani na marafiki zake, wataendelea kuzibana nchi za Kusini, na hivyo ustawi wa maisha ya wananchi katika nchi hizo, utakuwa matatani. NAM idumu.