RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chilla Tenga, amesema kitendo cha klabu kongwe za Simba na Yanga kugubikwa na migogoro, kinaitia aibu nchi.
Alisema jana jijini Dar es Salaam kwamba, kwa ukongwe wao, Simba na Yanga zilipaswa kuigwa kiuendeshaji na kimafanikio, lakini imekuwa kinyume cha hayo kwa kuendekeza migogoro isiyokwisha.
Tenga aliyewahi kukipiga katika klabu ya Pan Africans na timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, alisema migogoro hiyo imekuwa kikwazo cha maendeleo ya klabu hizo na soka kwa ujumla.
“Dunia nzima inajua katika soka ya Tanzania, kuna Simba na Yanga na hata viongozi wa CAF (Shirikisho la Soka la Afrika) na FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa), wakija wanataka kuziona timu hizi,” alisema Tenga na kuongeza:
“Wanazo habari za ukongwe na upinzani wa jadi wa timu hizi, hivyo wafikapo, mbali na kuwa na hamu ya kuziona timu, hupenda kuzitembelea,” alisema.
Tenga alitoa mfano hai wa viongozi wa FIFA wanaokuja katika semina elekezi ya viongozi wa klabu za Ligi Kuu, itakayofanyika Jumatatu, Bagamoyo, Pwani, kwamba wameomba kuzitembelea klabu hizo.
“Jumanne, tutawapeleka viongozi wa FIFA katika klabu za Simba na Yanga, hivyo ni kitu cha aibu kukuta makufuli yakining’inia katika ofisi za Simba,” alisema.
Amezitaka Simba na Yanga kubadilika ili kwenda na wakati kwa kuiga mafanikio ya klabu nyingine zikiwamo za Afrika Magharibi na Kaskazini, ambazo kimafanikio zinalingana na zile za Ulaya.
Tenga aliyejitosa kuwania uwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) katika uchaguzi wa Desemba 7, alisema Simba na Yanga zibadilike.
Alisema, kubadilika ni kuanzia kwa wanachana na viongozi kwa ujumla sambamba na klabu husika kuwa na katiba bora zenye kuziba mianya ya mapinduzi.
Kauli hiyo imekuja huku uongozi wa kikatiba wa klabu ya Simba chini ya Hassan Dalali, ukiwa umesimamishwa na mkutano uliokuwa umepingwa na uongozi uliopo madarakani.
Tangu kusimamishwa kwa Dalali, ofisi za makao makuu ya klabu hizo, zimefungwa makufuli, moja la uongozi wa Dalali na jingine la wapinzani.
Kuhusu uwakilishi wa Simba katika semina hiyo ya Bagamoyo, Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela, alisema majina yaliyowasilishwa kwao ni Makamu Mwenyekiti, Omar Gumbo, Katibu Msaidizi Mohammed Mjenga na Kocha Jamhuri Kihwelu.
Akigusia semina hiyo, Tenga alisema ina umuhimu mkubwa kwa soka la Tanzania na akazitaka klabu za Ligi Kuu kuitumia vema nafasi hiyo ya upendeleo.
Semina hiyo itafunguliwa na mkuu wa mafunzo kutoka FIFA, Jurg Nepfer kutoka Uswisi atakayewasili leo kwa ajili ya semina hiyo ambayo inafanyika katika nchi 10 tu kwa Afrika.
Tenga alisema suala la kutofautiana, ni kitu cha kawaida katika mchakato wa maendeleo, lakini tofauti hizo ziwe na hoja za msingi tofauti na ilivyo kwa Simba na Yanga.
Alisema kutokana na ukongwe na umaarufu wa Simba na Yanga, uimara na ufanisi wa klabu hizo, una faida kubwa kwa soka la Tanzania na kinyume chake, ni athari.