logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumamosi, 10 Novemba 2007
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1


Kingunge usingoje kurushiwa mawe
Salim Said Salim


BABA wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mara nyingi alituusia umuhimu wa viongozi kung’atuka madarakani na kuwaachia wengine nafasi za uongozi. Alionya juu ya hatari za kung’ang’ania madaraka.

Licha ya Mwalimu kupachikwa mapambo ambayo binadamu hastahili kupewa ya kuambiwa ‘zidumu fikra za mwenyekiti wa CCM’ kama vile yeye peke yake ndiye aliyekuwa na uwezo wa kutoa mawazo mazuri juu ya mustakbali wa Watanzania, alisisitiza umuhimu wa watu wenye fikra mpya kupewa nafasi za uongozi.

Kauli hii ya Mwalimu ya viongozi kutakiwa wang’atuke kwa hiari, ilitiliwa nguvu na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Awamu ya Nne, marehemeu Dk. Omar Ali Juma. Alisema ni vizuri kwa viongozi wazee kukaka pembeni wasingoje watu wawarushie mawe.

Kwa maana nyengine binadamu hutakiwa ajifunze kutokana na anayoyaona. Hili ndio lile Waingereza waliitalo maandishi yalo ukutani (the writings on the wal l – kila kitu kiko bayana).

Mkutano wa uchaguzi wa CCM uliofanyika Dodoma, nao ulikumbusha umuhimu wa kusoma maandishi ukutani.

Katika miaka ya nyuma ilikuwa hakuna aliyeweza kufikiria mkongwe wa siasa Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru kutokuwamo katika safu ya watu watano wa kwanza kufunguliwa mlango wa kuingia Halmashauri Kuu ya CCM. Badala yake iliibuka wa 12.

Baadaye jina lake likapendekezwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kuingia Kamati Kuu wa CCM, lakini wajumbe waliliweka kando na kushindwa kumpa kura za kutosha kuingia Kamati Kuu.

Walioshindwa walikuwa sababu akiwamo waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye.

Kilichomkuta Mzee Kingunge ni kielelezo cha watu kutaka mabadiliko na kama wazee hawaoni maandishi yaliopo ukutani watapewa mkononi na kukabidhiwa miwani kuyasoma.

Ni vizuri hili likawa somo si kwa Mzee Kingunge tu bali kwa wazee wengine wanaotumia udhaifu wa msemo wa Kiswahili kwamba kuwa na wazee pembeni ni dawa. Lakini tukumbuke kwamba hata dawa ikizidi nayo huwa sumu na kusababisha maradhi au maafa.

Hakuna anayeweza kubisha kuwa mchango mkubwa wa Mzee Kingunge kwa TANU na CCM, hasa katika mfumo wa chama kimoja, ni mkubwa. Lakini zile ni zama nyingine na hili lazima tulikubali.

Wakati ule akina Mzee Kingunge na wenzake, pamoja na marehemu Moses Nnauye, ndio waliokuja na falsafa ya ‘zidumu fikra sahihi za mwenyekiti wa CCM’, kama vile watu wengine hawana fikra sahihi.

Kundi hili ndilo pia lililoleta falsafa za ajabu ajabu kama jeuri ya chama (CCM) na baadaye katika miaka ya karibuni wakaona maneno ya tunawatesa (wapinzani) kama ni vielelezo sahihi vya ushindani wa kisiasa.

Huu ni mtazamo finyu wa siasa chafu na za uhasama na hautakiwi na kizazi cha hivi sasa na ndiyo maana wazee wanaotakiwa kung’atuka wanaonekana kuanza kunyooshewa vidole kabla hawajarushiwa mawe.

Binadamu lazima akubali mabadiliko, kama mwenyewe anavyobadilika kwa kuanzia kuwa mtoto mchanga, mtoto, kijana, mtu wa makamo, mzee na baadaye kikongwe.

Hapa inafaa Watanzania tuanze kutafakari na kujiuliza; kama katika utumishi wa serikali upo umri wa watu kustaafu, kwa nini pasiwepo vigezo katika medani ya kisiasa?

Huu mtindo wa kuwa na watu bungeni wanasinzia kutokana na kuwa na umri mkubwa unatutia unyonge.

Hivi sasa tunaweka awamu mbili zenye jumla ya miaka 10 kwa utumishi wa Rais wa nchi, kwa nini tusiwe na kiwango cha aina hii kwa madiwani na wabunge?

Wakati umefika wa kukubali mabadiliko. Kinachoweza kufanyika ni kukamilisha mageuzi, lakini hatuwezi kuyazuia hasa jamii ikiwa inataka, kama ilivyoonyesha mabadiliko makubwa katika Mkutano Mkuu wa CCM, Dodoma.

Ni vizuri tukaweza kuyasoma maandishi yaliopo ukutani badala ya kungojea maandishi kutusuta na kutuadhiri kama alivyoadhirika Mzee Kingunge.


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2007 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570