logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumamosi, 10 Novemba 2007
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1


Wanaowapa mimba wanafunzi wafanywe nini?
Innocent Mallya


TANGU Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete aamue kuvalia njuga tatizo la wanafunzi kupachikwa mimba, maeneo mengi ya nchi yamegubikwa na hofu ya aina yake.

'Operesheni kamata vijogoo' binafsi naona Kikwete aliamua kulijulisha taifa kuwa, yeye ingawaje ni rais wa nchi, ni baba Ridhwani.

Inapendeza rais au kiongozi yeyote kuwa na mtazamo huo kwani, ni ukweli kwamba, sote tunatambua kiongozi mzuri siku zote huanzia nyumbani.

Kaya ndicho kitovu cha kuaminika kuzalisha wataalamu wa kila aina.

Leo hii Watanzania lukuki na baadhi ya maeneo ulimwenguni wanamjua Kikwete na kumuunga mkono katika shughuli zake akiwa kama rais, kwa sababu alilelewa kwanza katika familia ya mahali pamoja.

Rais alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akisema, sasa imetosha wahuni kuharibu mustakabali wa elimu ya watoto wa kike, kwani ni kikwazo kwa maendeleo katika sekta ya elimu nchini.

Taasisi, asasi, wanaharakati na mtu mmoja mmoja, kila mmoja kwa wakati wake, kwa njia moja au nyingine, wamekuwa wakimuunga mkono rais katika kuhamasisha mapambano dhidi ya uharamia huu wa mimba za utotoni.

Karibu katika vikao vyote vya Bunge, suala la mimba za wanafunzi hujitokeza na kila mbunge huonyesha kukerwa na suala hilo.

Baadhi ya wabunge waliochangia hoja ya makadirio ya matumizi na mapato ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka wa fedha 2007/2008, wengi walimuunga mkono rais kuhusu tatizo hilo.

Baadhi ya wabunge hao ni Benedict Losurutia, (Kiteto - CCM), Suleiman Kumchaya (Lulindi - CCM), Jenista Mhagama (Peramiho - CCM) na Mbunge wa CHADEMA viti maalumu Suzan Lyimo.

Binafsi, sina shida na jitihada kuanzia za rais, taasisi, asasi, viongozi wa dini, Bunge na mtu mmoja mmoja katika mapambano haya.

Nitakuwa mtu wa ajabu sana ikiwa sitapongeza jitihada hizi. Napongeza kwa nguvu zangu zote na mapambano yaendelee mbele.

Mimi ni mwanahabari. Nimekuwa nafuatilia mambo haya katika jamii yetu hii, hata kabla rais hajalivalia njuga na kutema 'cheche'.

Kwa muda wote tangu nianze ufuatiliaji, nimebaini wengi wetu katika mapambano haya, tumeelekeza mashambulizi sehemu moja.

Nimegundua kuwa, wengi wetu tumejikita kwenye msimamo mmoja. Wahusika wahasiwe. Basi.

Ni kweli kwamba kuwahasi hawa ‘vijogoo’ ndio utakuwa muarobaini wa matatizo haya? Tumefanya utafiti kwa kiasi gani.

Jirani zetu Kenya kwa muda mrefu sasa nao wamekuwa na wimbo huu huu, ‘wahasiwe, wahasiwe’.

Naomba nieleweke hivi; kwanza siwatetei hawa nyang’au. Pili, sipingani na juhudi za rais wala msimamo wa Bunge kuhusu suala hili.

Isipokuwa, naona wengi wetu tumeelekeza silaha zetu sehemu moja. Kwa njia zipi, nitazizungumzia baadaye kidogo.

Leo hii, wazazi na walezi walio wengi (hasa wanawake) wanachangia kwa kiwango kikubwa katika kumong’onyoa maadili mema katika jamii katika suala zima la uvaaji wa nguo za kusitiri mwili.

Nani miongoni mwetu asiyejua chanzo kikubwa cha 'laana' hii kushamiri na kushika mizizi ni matamanio yatokanayo na uvaaji wa mavazi yasiyo na staha katika jamii?

Mbunge mmoja miaka kadhaa iliyopita alipata kusema, eti kama suala ni matamanio, “basi angalia pembeni huyo bibie akishapita, wewe chukua hamsini zako.”
Wengine wanasema, kama ni suala la matamanio, je wanaobaka watoto wadogo wametamani nini?

Mimi hapo hapo nauliza swali. Kama tungemuuliza huyo ‘kijogoo’ swali kwamba, kabla hajaingiliwa na 'pepo la ngono' hadi ‘kumbaka malaika wa Mungu’ (mtoto) muda uliopita alikuwa ametazama nini, atajibu nini?

Si atasema macho yake yalinaswa na 'mtandao' wa maungo ya wanawake wakiwa na mitindo yao ya mavazi yasiyo ya heshima almaarufu ‘utajiju’?

Hili ndilo linalonipa ujasiri wa kujenga hoja kwamba, wazazi na walezi hao wanahusika si tu kuhujumu maendeleo ya taifa, ila pia katika unyanyasaji kijinsia wa watoto wao wenyewe.

Leo hii si ajabu tena kuona mama mtu mzima anavalia mavazi ambayo kusema kweli ni kichefuchefu kwa kisingizio cha kwenda na wakati.

Nimeshuhudia si mara moja wala mbili, wazazi, walezi wa kike wakiwanunulia watoto wao nguo ambazo hazina tofauti na za kikahaba.

Kuanzia mijini hadi vijijini, leo ‘vitopu’ vinavyoacha vitovu vya wanafunzi nje ni maarufu kuliko magauni yanayositiri mwili.

Ni kweli hayo ni matokeo ya utandawazi baada ya dunia kuwa kijiji na hilo halikwepeki, lakini ni lini huo utandawazi ulikuwa ‘roboti’ na kuwalazimisha watoto wetu kuvaa vijinguo vilivyokwisha kuvaliwa na makahaba wa Ulaya?

Kama wazazi na walezi, tunashindwaje kutengeneza mfumo wa maisha ya familia zetu mfano wa kitalu kidogo ndani ya bustani moja kubwa ambayo ni ulimwengu ulioharibiwa kimaadili na utandawazi?

Kwa taarifa tu ni kwamba, wazazi na walezi kwa mkono wa kulia, wanatetea kwamba watoto wao wanatishiwa maisha na ‘vijogoo’ hawa, na kwa mkono wao wa kushoto, wanawaringishia jinsi watoto wao walivyo wazuri!!

Kwa jinsi maadili kwenye eneo la mavazi yatakavyoshikiliwa bango, naamini ndivyo idadi ya hawa ‘vijogoo’ itakavyokuwa inashuka polepole.

Pamoja na huu ‘mkwara’ wa kutaka kuwahasi hawa wahusika wanaohujumu maendeleo katika sekta ya elimu na taifa kwa ujumla, silaha hii ya kusimamia maadili katika mavazi itakuwa na mchango mkubwa sana katika mapambano haya.

Mzee Rashid Kawawa wakati wa miaka ya nyuma akiwa kama kiongozi, aliwahi kutoa msimamo wa 'taifa la wakati huo' kuhusu maadili katika mavazi na watu walifuata.

Muda mfupi baada ya Rais Kikwete kuingia jumba jeupe pale Magogoni (Ikulu), ulitokea uvumi kwamba aliagiza wote wanaovaa nguo fupi wakamatwe mara moja.

Wanawake wengi wakati ule, bado kidogo jiji liwashinde warudi kwao kwa jinsi walivyokuwa wakizomewa njiani.

Uvumi huo ulipofika Ikulu, rais akakanusha. Wanawake wakaanza 'kuwazodoa' waliokuwa wanavumisha uvumi huo kisha wakaanza kujivalia vijinguo vya aibu kwa raha zao, tena kwa kasi mpya!!

Najaribu kusadiki japo kidogo kuwa, kukemea maadili katika jamii si kazi ya rais (sina uhakika). Nililo na uhakika nalo ni kuwa, viongozi wa dini wanalo jukumu kubwa kuliko rais katika hili, kwani wao wako karibu nao zaidi.

Nafasi ya kiongozi wa dini na ushiriki wake katika mapambano haya ya unyanyasaji wa kijinsia, bado ni mdogo sana kwani viongozi wa dini kwa kiasi kikubwa wana ushawishi mkubwa unaoweza kugusa eneo hilo kutokana na ukweli kwamba, hadi sasa hakuna kifungu cha sheria kinachoruhusu kumsumbua mwanamke aliyevaa nguo zisizo za maadili.

Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) za mwaka 2005 zinaonyesha kuwa takribani wanawake 68,000 hufa kila mwaka kutokana na mimba zisizotarajiwa.

Bene Madunagu ni Mkurugenzi wa asasi isiyo ya kiserikali ya Girl Power Initiative (GPI) nchini Nigeria, yeye akilijua hilo la wasichana kunyanyaswa kijinsia aliamua kuaza mikakati mbalimbali ya kuwaandaa wasichana ili wagundue nguvu walizo nazo katika kupambana kupata haki zao za kijinsia.

GPI inaanza kutoa elimu ya kijinsia kwa mabinti wenye umri kati ya miaka 10 na 19, ikiwa na lengo la kuwahamasisha kuwa mbali na ngono zembe na mila zilizopitwa na wakati, ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu ya stadi za maisha ili waweze kujitunza bila kufanya ngono hadi muda muafaka.

Scottish Coalition Against Sexual Exploitation (SCASE) ya nchini Uingereza inayosadia makahaba kuachana na kazi hiyo, kwa muda mrefu sasa tangu waanze huduma hiyo walifikia mahali wakaamini kuwa dini ina nafasi kubwa sana katika kubadilisha hali hiyo.

Ndiyo maana hawakuona ni tatizo kuwashirikisha viongozi wa dini hususan Taasisi ya Kiinjili ya Salt & Light katika mipango yao jambo lililoweza kuwasaidia kufikia walengwa wao kwa ufanisi tofauti na mwanzo walipokuwa wakitoa huduma hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kutoka katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia kituo chake cha kutoa huduma ya watoto na familia (CCFCC) kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro, Tanzania, inakadiriwa kuwa na yatima 815,000 ambayo ni sawa na asilimia 11 ya watoto wote nchini walio chini ya miaka 18 .

Inasemekana kuwa asilimia kubwa ya yatima hapa wamezaliwa kutokana na jamii kutokuwa na elimu kuhusu uzazi wa mpango na hivyo watoto wengi huzaliwa pasipo kutarajiwa kwa njia ya ngono zembe na mila zilizopitwa na wakati, jambo linaloiongezea mzigo serikali na jamii kwa ujumla kila mwaka.

Viongozi wa dini wana wajibu mkubwa sana wa kuhakikisha kuwa wanawaongoza waumini wao katika mfumo wa maisha ambayo yatakuwa tofauti na wale wasioshiriki ibada yoyote.

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) nalo siku za nyuma lilikuwa na 'meno' siyo kama siku hizi linavyoachilia hivi hivi majarida, magazeti na nyimbo zinazoisababisha jamii kupotoka kimaadili.

Kimsingi, kuondokana na tatizo hili ni hadi pale umma wenyewe kuamua kubadilika kimtazamo na kuona makosa yake na kurejea kwenye mstari kimaadili, hususan katika kuanza, kuhamasisha na kudumisha hulka ya kuvaa nguo za heshima.

  Simu: 0756 864 781
Barua pepe: ifm_msimamo@yahoo.com


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2007 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570