logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumamosi, 10 Novemba 2007
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1


Serikali ijizatiti kuwalinda Watanzania katika ajira



KWA mara nyingine tena, Rais Jakaya Kikwete amesisitiza msimamo wake wa kila mara, unaotaka wawekezaji nchini wawafikirie Watanzania kwanza katika ajira na mishahara kabla ya kufanya hivyo kwa wageni.

Rais Kikwete alitoa wito huo juzi wakati akitembelea kiwanda cha East Coast kinachozalisha mafuta kilichopo katika eneo la ZamCargo, Dar es Salaam.

Katika kauli yake hiyo ya juzi, Rais Kikwete alieleza kusikitishwa na tabia ya baadhi ya waajiri kuwapa mishahara mikubwa wageni wanaofanya kazi katika kampuni zao na kuwaacha wazalendo ambao wakati mwingine huwa na elimu na ujuzi mzuri zaidi.

Sambamba na hilo, rais aliwakumbusha wawekezaji, akiwamo Mohammed Dewji ambaye ni mmiliki wa kiwanda hicho cha East Coast, kuanza kuwalipa wafanyakazi wao mishahara mipya iliyotangazwa na serikali kuanzia Januari mwakani.

Rais Kikwete anatoa agizo hilo kuhusu ajira kwa Watanzania wazalendo, miezi michache tu baada ya Mbunge wa Viti Maalum Lucy Mayenga kuuliza bungeni kuhusu jambo hilo hilo.

Mayenga katika swali lake hilo lililokuwa limeelekezwa Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Ajira, alitaka kuelezwa ni wageni wangapi waliondolewa nchini kwa kupatiwa ajira kinyume cha sheria za nchi.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana na Ajira, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema msimamo wa serikali kulinda ajira za wananchi wake utaendelea kuzingatiwa.

Nchimbi alilieleza Bunge kuwa, wageni wanapaswa kuajiriwa katika maeneo ambayo watalaam wa Kitanzania wenye elimu na ujuzi hawapatikani katika soko la ndani.

Aidha, naibu waziri huyo, aliwataka waajiri kuhakikisha wanawapatia utaalam Watanzania wanaofanya kazi za kuwasaidia wageni hao katika maeneo maalum, ili mikataba ya raia hao wa nje inapomalizika waweze kuchukua nafasi zao.

Nchimbi hakuishia hapo, bali alikwenda mbele zaidi na kulieleza Bunge kuwa, wizara yake ilikuwa imeunda kamati maalum ya kufuatilia mwenendo mzima wa ajira na kuhakikisha kuwa ajira zilizo mikononi mwa wageni ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania zinarejeshwa mikononi mwa raia wa hapa nchini.

Alisema chini ya utaratibu huo, wageni wanaofikia 432 walikuwa wamerejeshwa makwao baada ya kudhihirika kuwa walikuwa wakifanya kazi kinyume cha sheria za ajira katika maeneo ya viwanda na mahoteli ya kitalii.

Kwa kweli, majibu hayo ya serikali kwa kiwango kikubwa yalitoa mwelekeo mwema na wa kutia moyo, kwani yalionyesha namna Watanzania wanavyopewa nafasi ya kwanza katika ajira.

Pamoja na ukweli huo basi, wakati tukiipongeza serikali kutokana na kusimamia sheria za nchi vema kwa kuwajali raia wake, tunapenda kurejea msimamo wetu tuliopata kuutoa huko nyuma na kukumbusha kuhusu masuala mawili au matatu ya msingi.

Kwanza, tunapenda kueleza bayana kwamba, katika miaka ya hivi karibuni na si kwa Tanzania peke yake, makali ya utandawazi, yamesababisha raia wengi kutoka nje ya nchi kuingia hapa nchini na kuweza kupenya soko la ajira na kufanya kazi pasipo kubainika.

Aidha, hali kama hiyo imekuwa ikitokea pia kwa Watanzania ambao wamejikuta wakilazimika kukimbilia nje ya nchi, aidha kufuata taratibu halali za uhamiaji au zile za uzamiaji lengo likiwa ni kusaka ajira huko, baada ya kubaini kuwa hapa nchini kuna tatizo hilo na lile la kuwajali raia wa nje kuliko wao.

Kwa sababu hiyo basi, tunapenda kuiasa serikali kwamba, wakati huu inapoonyesha nia nzuri ya kuwajali raia wake, ihakikishe kile alichokisema Kikwete cha kuweka mazingira bora ya kazi kwa raia wake kinadumishwa na kuondokana na tabia ya kuwadharau wataalam wake na kuwaheshimu wale wa nje katika mishahara, marupurupu na maslahi mengine ya kikazi.


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2007 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570