WAKAZI wa Kichangani, Kata ya Kibada, Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam ambao hadi sasa hawajalipwa fidia za nyumba na mazao yao, wanakusudia kuandamana hadi ofisini kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Pombe Magufuli, kushinikiza walipwe.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi, walisema watakwenda kumwambia waziri jinsi serikali inavyojitapa kwa kutatua kero za wananchi ilivyoshindwa kutekeleza ahadi zake licha ya tathmini iliyoifanya katika viwanja hivyo baada ya maeneo yao kuchukuliwa kupisha ujenzi wa shule na zahanati.
Walisema mwaka 1999, walipewa eneo hilo rasmi, lakini ilipofika 2006 eneo hilo liliingia katika mradi wa viwanja 2,000 na wakaahidiwa na serikali kuwa watalipwa fidia kwa mashamba na viwanja vilivyochukuliwa kwa ajili ya mradi huo.
Kwamba tathmini ya maeneo yao ilifanywa na maofisa wa ardhi waliowataka kujaza fomu za tathimini lakini muda mfupi baadaye Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa eneo hilo alipinga ulipaji wa fidia hizo kwa madai kuwa eneo hilo ni la serikali ya kijiji hicho.
Walieleza kuwa mwenyekiti wao alitaka alipwe yeye fidia hiyo kwa vile ndiye kiongozi wa serikali katika eneo hilo.
Walisisitiza kuwa wakionana na Waziri Magufuli wana uhakika tatizo hilo litapata ufumbuzi wa haraka na uhakika kuliko mahakamani ambako walikwenda awali na kesi yao kutajwa zaidi za mara sita bila kuanza kusikilizwa.