TIMU ya soka ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Novemba 21 itaikaribisha Zambia ‘Chipolopolo’ katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayopigwa kwenye Uwanja wa zamani wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo iliyopo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kwa mujibu wa kalenda hiyo, inapaswa kuchezwa kati ya Novemba 17 na 21, mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela, alisema jana ya kuwa, Chipolopolo ni miongoni mwa timu walizoomba kucheza nazo mechi za kirafiki za kimataifa.
Alisema, Chipolopolo inakuja nchini kwa gharama za TFF kwani licha ya kuwa tayari kuja, hawakuwa na fedha, hivyo TFF itatumia jumla ya sh mil 30 kwa ajili ya chakula, malazi, usafiri wa ndani na gharama nyinginezo.
Msafara wa timu hiyo utajumuisha wachezaji 20, viongozi watano ambao watawasili Novemba 20 huku viingilio vikiwa ni sh 25,000 kwa viti maalum, Jukwaa Kuu sh 15,000, Kijani sh 8,000 na Mzunguko sh 3,000.