logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumapili, 11 Novemba 2007
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
sp.l_icon sp.r_icon
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1


Sebene - (7)
Innocent Nganyagwa


KARIBUNI kwa mara nyingine mpenzi msomaji wa safu hii ya Asili ya Muziki. Safari yetu kuielekea sebene bado inaendelea na leo tunaingia kituo cha saba.

Kama ulikuwa nami wiki iliyopita, basi natumaini unakumbuka tulipoishia na kama hukuwa nami, basi hujakosa mengi.

Tuna kawaida ya kufanya muhtasari wa yale tuliyoyachambua kituo kilichopita kabla ya kuendelea na kituo tulichopo.

Hii huwa mahususi katika kuwekana sawa kwenye mtiririko wetu wa uchambuzi, bila umakini unaweza kupotea msomaji.

Maana historia hizi tunazozitoa za asili ya chanzo cha mitindo mbalimbali ya muziki zimefanyiwa utafiti wa kina, si za kukisia.

Basi tuanze kwa kujikumbusha kwa ufupi yale tuliyoyaona wiki iliyopita, ambapo kwa hakika kisu kimeanza kuuelekea mfupa sasa.

Tuanzie pale ambapo nilitoa mfano mzuri wa athari za muziki wa Kilatino kwenye muziki wa Congo, kuwa ni nyimbo za Dk. Nico Kassanda.

Tuliona awamu mbili tofauti za mapigo ya muziki huo, ya taratibu, mambo ya Bolero na baadaye mapigo ya kasi yalipojiri.

Nikatafsiri kwa mfano hai wa karibu mambo hayo ya taratibu kwa kuutathmini mtindo wa ‘Kamanyola bila jasho’ wa bendi ya Marquiz du Zaire ambao kwa hakika ni mambo yale yale ya taratibu bila jasho.

Ila tu yalitafsiriwa kwenye lugha ya kibiashara iliyokubalisha miondoko hiyo hapa kwetu.

Tukaona ujasiri mkubwa wa Wakongomani wa kuthubutu kutafuta mafanikio bila woga pale wanapohisi wana uwezo wa kufanikiwa, fursa mojawapo waliyoitumia ni kukimbilia Ufaransa.

Tukaona mchanganyiko wa awali kwenye miondoko hiyo ulisababisha kubadilika kasi ya mapigo ya mirindimo iliyokumbatiwa na kizazi kipya cha Kikongomani na kuleteleza mapigo ya ‘kavasha’ Tukaelezea kiufundi tofauti ya kimsingi ya ‘kavasha’ na ‘sebene’ kutokana na ngoma ‘drums’ kugunduliwa na kuingia kwenye muziki.

Tukapata somo muhimu sana lililoonyesha kuwa msingi wa mapigo ya baadhi ya vyombo katika muziki huo wa Kikongo umebaki kama ulivyo. Tukachunguza kwa makini na kudhihirisha mapigo ya gitaa ya Lwanzo Luambo Makiadi ambaye naye aliitoa kwa mpiga gitaa mahiri wa zamani wa miondoko ya Kilatino, Grenhert, mapigo ambayo vionjo vyake vinatumika kiufundi hadi sasa.

Tukatua kwenye mambo ya ‘Benga’ la Afrika Mashariki, miondoko ya kasi ya Kijaluo kutoka Kenya iliyokopwa na Wakongomani na kuzalisha mambo mapya kabisa yaliyozua maswali kwa walioshindwa kuelewa na kuikubali kwa haraka miondoko hiyo mchanganyiko.

Walioshindwa kuuelewe muziki huo mchanganyiko waliuliza “C’est quoi ca?” kwa Kifaransa cha kizairwaa kisicho rasmi.

Neno hili linatamkwa “Se kwa sa” na ndio chanzo cha jina la mtindo wa ‘Kwasa Kwasa’ Kifaransa sanifu cha lugha hiyo ni “Qu’est ce que c’est” inayotamkwa “Kes ke se” maana yake ‘ni nini hii?’ hiyo ilidhihirisha mshangao wa watu kwa kile kinachopigwa.

Nikamalizia sehemu ya wiki iliyopita kwa kuahidi kuzama kwa kina na kuona zilikotokea ‘rap’ za mirindimo hiyo, tusonge mbele kutokea hapo.

Utakumbuka pale awali kabisa kwenye uchambuzi huu niliwahi kusema kuwa matokeo ya kilichozalisha mtindo uliosababisha kuwepo kwa Sebene ni mchanganyiko wa mambo mengi kutoka pande mbalimbali.

Turejee pale tuliposema kuwa, mirindimo ya Kilatino ilifikia Afrika ya Magharibi na baadaye kuteremka maeneo ya Afrika ya Kati ikiwa na mchanganyiko wa ziada wa mirindimo ya tembo la mnazi.

Kawaida kwenye utamaduni wa Mwafrika hasa ‘mbantu’ kuna ile tabia ya kuimba kingonjera au kusemasema, iwe kwa furaha au kwa huzuni.

Huo ni mtindo ulio kwenye urithi wa chembe hai za ‘Waafrika Wabantu’ na ukaja kuibukia kwa Waafrika wa ughaibuni na baadaye kudakwa na kutiwa nguvu kwenye muziki wa Kikongo.

Najua itakushangaza, lakini hivyo ndivyo ukweli ulivyojiri, ni kutoka kwenye miondoko ya ‘Soul’ ambayo gwiji wake alikuwa ni hayati James Brown ndiko zilikotokea ‘rap’ za mabolingo.

Ndiyo maana sehemu iliyopita nilisema kuwa, pamoja na Wakongomani kuhemea kwa watawala wao lakini hawakuchukua utamaduni wa hao wakoloni wao.

Maji hufuata mkondo, wao walikopa vionjo kwingineko kabisa kwenye silika sawa na wao, Uafrika. Kuna ushahidi wa jambo hilo? Ndiyo, tena wa kutosha, lakini nikupe mifano midogo mitatu.

Kwanza kuna wale watu waliokimbia vita, pili kuna vijana waliowahi kupelekwa na serikali yao huko ughaibuni kusoma kwa dhamira ya makusudi kabisa na kujiingiza kwenye muziki na utamaduni wa ‘ki-soul’ Lakini ushahidi ulio wazi kabisa ambao waliowahi kuhudhuria maonyesho ya Lwambo watakubaliana nao, ni kundi lake la muziki ambalo hupiga vyombo kabla yeye mwenyewe hajapanda jukwaani.

Kundi hilo lililotumbuiza kwa muziki wa ala, baadhi ya nyimbo walizopiga zilikuwa kwenye ladha ya ‘Soul’ na cha kustaajabisha zaidi hata maongezi ya vijana hao yalikuwa kwa Kiingereza chenye lafudhi ya Kimarekani! Unahitaji ushahidi zaidi?

Mfano wa karibu zaidi ni huu hapa, kwa kuwa wanamuziki wetu waliozoea sana kuiga mirindimo inayotokea kwa Wakongomani, basi hata hapa kwetu athari za ‘ki-soul’ kupitia Ukongomani zilikuwepo.

Tafuta wimbo wa Mbaraka Mwishehe unaoitwa ‘Mapenzi shuleni’ na wa Marijani Rajabu unaoitwa ‘Salama’ sikiliza kwa makini mapigo yake ya ‘drums’ utakubaliana nami.

Sina shaka hawa waliovutiwa sana na mapigo ya watu kama Franklin Bukaka.

Kusemasema, yaani ‘rap’ au ‘kurapu’ neno lililoleteleza ‘marepa’ kwenye zama za Sebene hapo baadaye, kukaingia kwa nguvu kubwa kwenye miondoko hiyo.

Kwa kuchanganyika na Ubantu asilia wa Kiafrika, mizizi yake ikaota ndani ya mtindo huo.

Mchanganyiko huo ukaambatana na kionjo cha ziada na cha wazi kabisa kutoka mirindimo ya ‘ki-soul’. Hayo ni mambo ya namna mapulizo, matarumbeta na midomo ya bata ‘saxophone’ zilivyopigwa.

Tupeane faida kidogo, neno ‘rap’ linalotokea kwenye mambo hayo ya ‘soul’ ni muunganiko wa maneno matatu ya Kiingereza yenye maana ya ‘ghani na mrindimo’ yaani ‘Rhythm And Poetry’ ukifupisha maneno hayo ndipo unapata ‘RAP’ yaani kusemasema au kughani juu ya muziki.

Hiki ndicho kile ambacho upande wa pili wa mitindo mingine mahususi kwa kusemasema tu kama ya kina Dk. Dre, Snoopy Doggy Dog, Tupac Shakur na Eminem huitwa Rap.

Rap ilipoendelea na kupata sifa ya ukakamavu au ugumu kama wanavyoita wenyewe, ikageuka na kuwa Hip Hop. Tusizame sana kwenye mambo hayo, fursa yake ipo, kuna siku tutachambua mambo hayo kwa kina.

Msomaji, mambo yanazidi kwenda yakiongezeka, tuna vionjo vitano hadi sasa. Latino fever, tembo la mnazi, mapigo ya Wakongomani wenyewe, benga na soul.

Nini kitafuatia? Sina shaka wiki ijayo tutaona vionjo zaidi. Kwa leo naomba tuweke kituo hapa ili utafakari vyema uchambuzi wa kituo hiki cha saba. Tukutane Jumapili ijayo, baki salama!

Mwandishi wa makala hii ni mwanamuziki mkongwe wa miondoko ya reggae hapa nchini. Kwa maoni na ushauri anapatikana kwa simu namba: +255 752 227 594, barua pepe: rasinnonganyagwa@yahoo.com


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2007 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570