logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumapili, 11 Novemba 2007
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
sp.l_icon sp.r_icon
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1


Uchaguzi Z’bar ulikuwa huru?
Peter Nyanje


MCHAKATO wa uchaguzi mkuu uliopita Visiwani Zanzibar ulitawaliwa na malalamiko mengi. Kati ya hayo, mengi yalielekezwa kwa Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC).

Malalamiko hayo yalihusu mwenendo wa uchaguzi huo, katika masuala kama uandikishwaji wa wapiga kura, uendeshwaji wa vituo vya kupigia kura na kuvunjwa kwa haki za wapiga kura.

Katika suala la uandikishwaji wa wapiga kura mathalan, yalikuwepo malalamiko kuwa wapo watu waliokuwa wamejiandikisha zaidi ya mara moja. Hili, kwa kiasi fulani lilikubaliwa na ZEC, wakalifanyia kazi na kutoa taarifa kuwa takribani watu 5,000 walibainika kujiandikisha zaidi ya mara moja.

Lilikuwepo pia suala la kuandikishwa kwa watu ambao walikuwa hawajafikisha umri rasmi wa kujiandikisha (miaka 18).

Yapo malalamiko yaliyoelekezwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), hasa kuhusu matumizi ya vyombo vya dola. Ilidaiwa kuwa sehemu nyingi vyombo hivyo vilitumika kukandamiza wapinzani, hasa wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), ambacho ndicho chenye wafuasi wengi wa upinzani visiwani humo.

Wakati huo, mengi ya madai haya, pamoja na mengine mengi yalikanushwa kwa nguvu zote na taasisi ambazo zilituhumiwa. ZEC ni mojawapo ya taasisi ambazo zilikanusha kasoro kadhaa walizotuhumiwa.

Vyombo vya dola navyo vilikanusha kuhusika na unyanyasaji wowote dhidi ya vyama na wapiga kura. ZEC ilikaa kimya wakati vyombo hivyo vya dola vikikanusha kuhusika na kuvunja taratibu za uchaguzi.

Lakini waswahili wana msemo; Mambo hadharani. Na sasa ZEC imeamua nayo kuweka mambo hadharani.

Tume hiyo, ilipomaliza muda wake wa kuwa madarakani, iliandaa ripoti ambayo imewasilishwa kwa Rais Amani Karume, aliyewateua wajumbe na mwenyekiti wake. Kwa bahati nzuri sana, ingawa si yote, lakini mambo muhimu yaliyomo katika ripoti hiyo, yamewekwa hadharani. Mambo hadharani, hongera ZEC.

Pamoja na hongera hizo, lakini lazima mshangao unaosababishwa na ripoti hiyo uonyeshwe wazi. Kikubwa kinachoshangaza ni kuwa kasoro nyingi zilizokuwa zimeainishwa wakati wa uchaguzi, ambazo ZEC na taasisi nyingine ilizikanusha, ndizo ambazo kwa kiasi kikubwa zinabainishwa kwenye ripoti hiyo.

Kwa sababu bado rekodi ya ZEC kukanusha mambo haya ipo, na sasa wanaibuka na ripoti inayoonyesha kuwa yale waliyoyakanusha yalitokea kweli, inabidi waje na msimamo ambao utatuweka sote kwenye uelewa mmoja kuhusu mambo hayo; yalitokea au hayakutokea? Ufafanuzi huo unatakiwa kwa sababu baadhi ya yaliyomo kwenye ripoti yanazua maswali mengi ambayo majibu yake hayapaswi kuwa ya kufikirika.

Mathalan, katika ripoti yao ZEC wanabainisha kuwa jumla ya watu 1,197 walibainika kujiandikisha zaidi ya mara moja. Lakini ripoti za awali zinaonyesha kuwa watu zaidi ya 5,000 walibainika kujiandikisha zaidi ya mara moja. Kimetokea nini mpaka namba hii ikabadilika kiasi hiki?

Pia inapaswa ielezwe kinagaubaga, hao watu waliobainika kujiandikisha zaidi ya mara moja, wamechukuliwa hatua gani? Inafahamika wazi kabisa zipo sheria zinazoharamisha mtu kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura zaidi ya mara moja, pamoja na mambo mengine sheria hiyo imepanga adhabu kwa mtu au watu watakaobainika kutenda kosa hilo.

Inapaswa ielezwe hapa watu hao ambao ZEC imebaini kuwa wamejiandikisha zaidi ya mara moja wamechukuliwa hatua gani?

Hili linapaswa kuelezwa kwa sababu kuna tetesi kuwa kati ya watu waliobainika kujiandikisha zaidi ya mara moja, ni vigogo serikalini. Haiyumkini hawa wakaachwa hivi hivi. Hii ni kwa sababu iwapo wao hawakuona haya kutaka kuliingiza taifa katika madhila yanayotokana na njama za kuvuruga uchaguzi, serikali nayo haipaswi kuona haya kuwashughulikia ipasavyo.

Katika ripoti yake, ZEC inavinyooshea kidole na kuvilaumu vikosi vya SMZ pamoja na wanasiasa kuingilia utendaji wake, wakati wa uchaguzi wa 2005.

Ripoti ya tume hiyo yenye kurasa 70, imetoa lawama kali kwa vikosi vya SMZ, vikiwemo KMKM, JKU, Zimamoto, Mafunzo na Valantia, kwamba wakati mwingine vilifanya maamuzi yanayohusu ulinzi wakati wa uchaguzi bila kuihusisha tume.

Baya zaidi, ZEC inaeleza kuwa vikosi hivyo vilishiriki katika kuwaandikisha askari bila ya kuihusisha tume. Sote tunafahamu kuwa jukumu la uandikishaji wapiga kura ni la tume, iwapo askari au mtu yeyote anataka kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, analazimika kufuata taratibu zilizowekwa.

ZEC inaeleza kinagaubaga kuwa pamoja na kuchukua hatua ya kuchukua hatua ya kuwaita viongozi wa vikosi hivyo, lakini walikataa katika nyakati walizoombwa ili kwenda kurekebisha hali mbaya ya mambo iliyokuwa ikijitokeza wakati wa uandikishaji wapiga kura, hasa katika Mkoa wa Mjini Magharibi.

Ripoti imesema viongozi wa Serikali za Mitaa (Masheha) ambao ni mawakala wa tume hiyo, wakati wa uandikishaji wapiga kura walisikiliza zaidi maelekezo ya wakubwa wao kutoka Serikali za Mikoa na kupuuza maelekezo ya tume hiyo.

Kutokana na matatizo hayo, ZEC inapendekeza katika ripoti yake hiyo kuwa masheha waelekezwe kutekeleza majukumu ya Tume ya Uchaguzi wakiwa wakala wa tume, lakini amri zote ambazo zinahusiana na shughuli za uchaguzi zitolewe na tume yenyewe na si vinginevyo.

Imeelezwa katika ripoti hiyo kwamba, kuna baadhi ya vyama vya siasa vilishauri watoto wadogo chini ya umri wa miaka 18 wakajiandikishe kwenye daftari, huku wakijua kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Ripoti hiyo ilisema mbali ya kukubali kusaini maadili ya uchaguzi, baadhi ya vyama viliyavunja kwa sababu hayakuwa na nguvu za kisheria. Ndiyo maana sasa ZEC inapendekeza maadili ya uchaguzi yawe ni sehemu ya sheria za uchaguzi.

ZEC inagusia pia mambo nyeti likiwemo la taasisi yenye mamlaka ya kuongeza au kupunguza majimbo ya uchaguzi. Kwa mujibu wa tume hiyo, suala hili lina utata wa kikatiba. Wakati tume inaamini kuwa yenyewe ndiyo yenye mamlaka ya kufanya hivyo, lakini kwa utaratibu uliotumika, Baraza la Wawakilishi ndilo lililopitisha uamuzi kuhusu suala hilo.

Kasoro hizi pamoja na nyingine zilisababisha mivutano ambayo ilihatarisha uchaguzi huo. Lakini uchaguzi Zanzibar haukuishia mwaka 2005, tunatarajia kuwa itafanya uchaguzi mwingine mwaka 2010 na ili kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unatumika kuimarisha demokrasia, ni vema kasoro hizi, ambazo ZEC imezikiri zifanyiwe marekebisho.

Ni vema tukaangalia tunakokwenda ili kujiepusha na matatizo yoyote ambayo yanaweza kutukwamisha katika jitihada zetu za kujenga taifa tajiri.

Hatupaswi kuangalia nyuma kwani tukifanya hivyo tunaweza kujikuta tunajiuliza maswali ambayo kimsingi yanaweza kutufanya tuone giza mbele na kushindwa kujua njia ambayo tunapaswa kuifuata.

Hata hivyo, yapo ambayo tunapaswa kujiuliza kwa ajili ya kuweka msimamo wa pamoja na kupanga mustakabali utakaotufikisha tunapokusudia kwenda. Ni lazima tujiulize na kupata jibu la iwapo hivi uchaguzi huo uliofanyika ukigubikwa na kasoro hizo zote, ulikuwa huru na wa haki kama ilivyoelezwa?

pnyanje@gmail.com, http://nyanje.blogspot.com


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2007 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570