logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumapili, 11 Novemba 2007
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1


CCM, maneno matupu hayafiki mbingu ya saba
Deus Bugaywa


HATIMAYE pilikapilika na joto la uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) sasa limemalizika, wenye kufurahi wanafurahi, wenye kulia wanalia, hiyo ndiyo hali halisi ya maisha. Ni jambo la heri kwamba mkutano mkuu huo wa nane wa chama hicho umemalizika kwa amani na kwa mafanikio.

Pamoja na mambo mengine yaliyojiri katika mkutano huo, kivutio kikubwa ilikuwa hotuba ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambayo ilifufua matumaini ya wale waliokuwa wanadhani kuwa chama hicho kiko katika siku za mwisho wa uhai wake.

Habari za hotuba hiyo kubeba ujumbe wa kuashiria kufa rasmi kwa kikundi kilichokuwa kinakuja na nguvu ya ajabu ndani ya CCM, maarufu kama wanamtandao, zimepokelewa na watu wengi kwa furaha na matumaini makubwa, kwamba sasa mwenyekiti wa chama hicho ameamua kweli kukisafisha.

Kweli ‘kuzikwa’ kwa kundi la mtandao (kama kweli limezikwa) ni habari njema kwa wanachama wa chama hicho, ambao waliliona kundi hilo kama chanzo cha mwisho wa mshikamano na umoja ndani ya chama hicho.

Ni kweli kwamba hotuba za ufunguzi na ufungaji wa kikao hicho zilikuwa na matumaini kwa wote wenye mapenzi mema, hotuba za mwenyekiti pia zinastahili pongezi, lakini zenye tahadhari kubwa.

Pongezi hizo zinatakiwa kuwa na tahadhari, kwani bila tahadhari tunaweza tukafikia mahali tukadhani kwamba matatizo ya CCM sasa yamekwisha, huku kutakuwa ni kujidanganya. Wahenga wetu walituasa kwa hekima zao kuwa matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno.

Maneno kama ilivyo nia, hata iwe njema kiasi gani, isipowekwa katika matendo huishia kuwa kelele za mlango tu ambazo hazitakaa kamwe zimfanye mwenye nyumba asipate usingizi. Lakini pia historia ni shahidi kwetu kwamba maneno matamu yanayotolewa katika majukwaa ya siasa za nchi hii ni kwa uchache sana yanageuzwa kuwa vitendo.

Mara nyingi zimekuwa ni njia za wanasiasa kusoma hisia na joto la siasa la wakati huo na kuwapa watu maneno wanayotaka kuyasikia na baada ya hapa mambo yanaishia hapo. Nina hakika kila mtu anakumbuka ni kwa jinsi gani kwa mfano hotuba za mwanzo za Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa juu ya rushwa zilivyokuwa nzito na kali kiasi cha kutusadikisha kwamba rushwa imepata mpiganaji wa kiwango chake.

Sidhani kama kuna mtu ambaye hakumwamini pale alipokuwa akisisitiza kwa nguvu zake zote kuwa atapambana na rushwa bila suluhu. Watu walijua mkombozi amepatikana na ‘Masiya’ ameshuka kumaliza matatizo na kero za wananchi.

Muda, kama ulivyo kawaida yake, ndio husema ukweli wote, baada ya muda tukasikia kila msaidizi wake aliyeshutumiwa kwa rushwa, mwenyewe alikuja juu kumtetea na kuhoji wanaoshutumu kwamba wao mitaji yao wamepata wapi.

Watu wakabaki wameduwaa nini kimemtokea Masiya wa Watanzania? Kumbe tulilokuwa hatulijui wakati huo lilikuwa sawa na usiku wa giza, yale tunayoyasikia sasa yanaweza kutusaidia kuelewa yaliyokuwa yakiendelea wakati huo.

Uchaguzi huu utumike tu kama kipimo cha uthabiti wa kauli hizo, kwamba chama kimeahidi kuwavua nyadhifa zao wote watakaobainika kwamba wamepata ushindi huo kwa rushwa. Ni matarajio ya wenye chama hicho kwamba tutasikia fagio la chuma likifanya kazi hiyo si muda mrefu ujao.

Kwa sababu ni ngumu sana kuusadikisha umma wa Watanzania kwamba viongozi wa chama hicho wamechaguliwa kwa haki bila kupitisha ‘takrima’ hapa na pale, ni kweli kwamba wapo walio safi, lakini ni hakika kwamba si wote walio safi.

Na wala hatutegemei chama kitafute ushahidi wa kimahakama ili kuthibitisha wala rushwa wake, katika siasa naamini sekretariati ya chama inalijua hilo, kwamba tuhuma zenye uzito wa haja zinatosha kabisa kumwajibisha mtu kisiasa, ili kulinda imani ya chama kwa wanachama wake na jumla.

Vinginevyo kama ahadi hiyo itaishia tu hewani, huo utakuwa mwanzo wa kukivunjia chama heshima kwa kuwa kuna baadhi waliopokea na waliotoa rushwa, wasipoona hatua zikichukuliwa hawa hawatakuwa tena na heshima wala woga kwa kauli za vongozi wao kwa kuwa wanajua zinaishia kuwa kauli za jukwaani tu.

Kosa lingine tunaloweza kufanya, ni kudhani kuwa matatizo ndani ya chama hicho kama alivyoyaainisha mwenyekiti wake kama moja ya vyanzo vinavyoleta mifarakano miongoni mwa wanachama na kupandikiza chuki binafsi ya viongozi na wanachama na baina ya chama na umma, yameletwa na mtandao huo.

Hakuna anayeweza kuukana ukweli kwamba CCM sasa hivi pamoja na matumaini yaliyoibuka wakati wa mkutano wao mkuu wa nane, yatakuwa ni ya kutuliza tu maumivu kama hawataamua kuchukua maamuzi magumu ya kurejea kwenye misingi iliyozaa chama hicho. Kama CCM sasa inapita katika msukosuko, ni wazi kwamba hali hiyo haisababishwi na mtandao au visingizio vingine vingi ambavyo vimekuwa vikitajwa mara kwa mara. Matatizo ya CCM ni matokeo ya kutosikia la mkuu. Dawa ya matatizo yote ya chama hicho ni moja tu, kurudi kwenye ‘misahafu’ iliyosababisha chama hicho kuwepo tofauti na hapa hakiwezi kuepuka laana ya kuvimba guu.

Moja ya changamoto alizozitaja mwenyekti ni pamoja na kukabiliana na vitendo vnavyoleta mifarakano miongoni mwetu na kupandikiza chuki binafsi ya viongozi na wanachama na baina ya chama na umma.

Ni kweli chama hiki kinakabiliwa na changamoto hizo leo, kuna baadhi ya viongozi tena wa juu kabisa wa chama hicho hawapikiki chungu kimoja kwa sababu za kisiasa, ama walishawahi kuwania nafasi moja wakapakana matope mpaka wakageuka ‘maadui’ au mmoja anatishia nafasi ya mwingine kisiasa.

Hali hii hata hivyo haisababishwi na kitu kingine chochote isipokuwa ubinafsi unaokitafuna chama hicho kutokana na baadhi ya wanachama wake na kuwania nafasi za uongozi kwa kusukumwa na manufaa binafsi zaidi kuliko moyo wa kutumikia wananchi.

Haiyumkiniki kwamba kama mtu anataka nafasi fulani ya uongozi kwa nia njema ya kuwatumikia wananchi, hatafikia kiwango cha kumchukia anayeshindana naye kiasi cha kutopikika chungu kimoja, chuki hizi zinaletwa na dhamira iliyojificha ya kutaka nafasi husika, ambayo kwa vyovyote vile haiwezi kuwa ni ya utumishi wa umma peke yake.

Kama dalili za kuashiria kwamba hata makundi yanayotakiwa yafe kila baada ya uchaguzi hayatakaa yafe, ni baada ya uteuzi wa makamu mwenyekiti, Pius Chipanda Msekwa na uundwaji wa sekretariati ya chama hicho kwa upande wa Tanzania bara, tayari kuna makundi yamepokea matokeo hayo kwa faraja kwamba yanatoa matumaini zaidi kwa kambi yao ili kuimaliza kambi nyingine, faraja hiyo ni kubwa kwenye baadhi ya wilaya za Mkoa wa Mwanza.

Ni kwa vile uongozi wa chama sasa hivi ni kwa ajili ya manufaa binafsi zaidi kwa baadhi ya viongozi na wagombea, ndiyo maana chuki hizi zinazaliwa, laiti kama uongozi wa chama hicho na serikali yake ungekuwa bado na mtazamo wake wa tangu kuasisiwa kwa chama hicho, kwamba cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu kwa manufaa binafsi, naamini chuki hizi zisingekuwepo.

Lakini pia suala la chuki kati ya chama na umma hili nalo chama kinajitengenezea chuki hiyo chenyewe kwa sababu hapo kilipofika hata baadhi ya wanachama wake waaminifu wanaona njia iliyochaguliwa na chama chao si yenyewe, wapo waliojaribu kusema, lakini bado sauti zao zimeishia kuwa sawa na kumpigia mbuzi gitaa, hakuna aliyekuwa tayari kusikiliza.

Chama hiki kilianzishwa ili kuwatetea wanyonge na kupigania haki zao na zaidi sana kuleta usawa katika jamii iliyotoka katika mikono ya unyonyaji wa mkoloni. Ndio kusema lengo la msingi la chama hiki wakati kinazaliwa kama TANU na baadaye CCM lilikuwa ni kuleta uhuru na baadaye usawa kwa jamii itakayokuwa imekombolewa.

Kwa tafsiri nyingine, bila kuwa na usawa katika jamii iliyokuwa inatoka kukombolewa kutoka makucha ya wakoloni, uhuru huo usingekuwa na maana kwa baadhi ya Watanzania, hasa wanyonge wangeendelea kukandamizwa tu kama kusingechukuliwa hatua za makusudi kuleta usawa katika jamii, hiyo ikawa kazi kubwa ya kwanza ya chama hicho baada ya uhuru.

Historia nzima ya dunia hii imejaa ushahidi wa jinsi gani pale pasipokuwa na usawa hapana amani, ili kuleta amani na usawa kwa jamii ya Watanzania lilizaliwa Azimo la Arusha ambalo misingi yake ilikuwa ya kibinadamu, ilikuwa ni misingi ya utu, hii ina maana kwamba tulipozika Azimio la Arusha kwa sababu zozote zile tulizika misingi ya utu, tulizika misingi ya ubinadamu.

Na kwa Watanzaia wanyonge ambao azimio hili lilikuwa ndilo tumaini lao pekee linalotambua utu wao na kuwaheshimu kama binadamu, baada tu kukoma kwa azimio hilo kulimaanisha kukoma kwa ubinadamu na kutothaminiwa kwa utu wa baadhi ya Watanzania, hapo ndipo chuki kati ya chama na umma anayoisema Mwenyekiti wa CCM inapoanzia.

Kwamba kama umma una chuki na chama hicho si ya kuchochewa au kuchonganishwa na mtu kwa unafiki au ‘itina’ za kisiasa kama wasemavyo wenye chama chao. Ni matokeo ya kutupilia mbali misingi ya chama hicho wale wenye imani thabiti na misingi ya chama hicho wanajiona wamewekwa kando, katika mazingira haya ni vigumu sana kuepuka chuki ya waliotelekezwa.

Hawa ni watu wanaotaka haki na usawa, wasipopata vitu hivyo au hata tu wakiona kuna dalili za kutopata haki na usawa, ni ngumu sana kutarajia kuwa na amani mahali hapo, kama alivyowahi kusema Mwalimu Julius Nyerere wakati mmoja kwamba, kama hakuna usawa katika jamii yetu hatuwezi kujidanganya tuna amani.

Jamii isiyokuwa na usawa ni sawa na volcano inayotokota ambayo siku moja ni lazima ilipuke. Hisia za dalili za kukosa haki ni kali sana sasa hivi katika jamii yetu, si kwa wanachama wa CCM peke yake, zipo kwa umma wote wa Watanzania, hisia hizi zina chuki ndani yake na si chuki za bure zina misingi yake.

Wananchi hata kama hawasemi waziwazi, lakini yatakuwa maajabu kutarajia kwamba Mtanzania maskini ambaye anaishi chini ya dola moja kwa siku, hana uhakika na kupata mlo mmoja achilia mbali mitatu kwa siku, ambaye mwanae anasoma shule yenye walimu watatu au wawili.

Raia huyu ambaye malaria tu pamoja na kuwa inatibika bado ni tishio kubwa kwa uhai wake, mwananchi ambaye akipata ujauzito anakuwa nusu mfu ama nusu mzima kwa sababu hana uhakika wa kujifungua salama, umtarajie awe na hisia za kawaida tu na aipende serikali yake kwa moyo mmoja huku akisikia matumizi ya ajabu ajabu ya pesa zake yanayofanywa na serikali hiyo hiyo.

Viongozi anaowatumaini na aliowapa dhamana ya kuongoza nchi yake wanasaini mikataba ya ajabu ajabu wakijua wazi kwamba taifa halina maslahi katika mikataba hiyo, lakini wanaitetea kwa nguvu zote. Tena wanasema uchumi unapaa huku wananchi wenye nchi yao wanazidi kuwa mafukara kila uchao. Maisha yanazidi kuwashinda Watanzania kila siku, idadi ya maskini na wasiojiweza inaongezeka kila siku, rushwa inazidi kushamiri katika kila uga kwenye maisha.

Haya yote hayupo wa kumnyooshea kidole isipokuwa chama ambacho kimekuwa kinatekeleza sera zake tangu uhuru, pengo kati ya maskini na matajiri linaongezeka, si kwa sababu Watanzania ni wazembe kiasi hicho, lakini hakuna mazingira mazuri ya kuwawezesha kujikwamua na hali hiyo.

Leo mkulima mwenye nia njema ya kuondokana na umaskini akijikusuru kwa nguvu zote alime ili ajikwamue na umaskini, juhudi zake zitaishia kwenye soko la mazao yake, bei ya pamba atakayoikuta sokoni haimfanyi aone ukulima kama ni kazi, isipokuwa aina fulani ya utumwa wa kuwatumikia wenye mitaji, mifano ni mingi.

Ndiyo kusema kwamba, chama kama kinataka kiweke mambo yake sawa na kitazamike vizuri mbele ya jamii, kikabili changamoto hizo kwa vitendo, kwa sababu pamoja na kuwa ‘matendo hukidhi haja kuliko maneno’, matendo pia husema kwa sauti kubwa kuliko maneno. Kisisahau kwamba maneno matupu hayafiki mbingu ya saba.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0734 449 421 au barua pepe: drbugaywa@yahoo.com


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2007 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570