logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumapili, 11 Novemba 2007
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
sp.l_icon sp.r_icon
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1


Dk. Mvungi: Uchumi unaopaa ni wa nani?
Happiness Katabazi


BAADA ya wiki iliyopita kuwa na sehemu ya kwanza ya makala hii, leo tunaendelea katika sehemu ya pili, kama Mwandishi Wetu Happiness Katabazi alivyofanya mahojiano na Dk. Edmund Sengondo Mvungi, Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Endelea…

Swali: Dokta Mvungi hayo unayosema yanatisha. Sasa wanamageuzi mmejipanga vipi kukabiliana na hayo uliyoyaelezea?


Jibu: Ni vema kwanza kujiweka sawa kuyafichua maovu haya wananchi wayajue. Kulijua tatizo ni hatua ya kwanza katika kulipatia jambo hilo ufumbuzi. Mimi siamini kuwa kule CCM kila kiongozi au kila mwanachama ni fisadi. Wapo wenye nia njema kule ambao pia wanaumia wakiona ufisadi huu. Kumbuka ufisadi ni uovu wa kupindukia na hauna itikadi. Hiyo ni sura moja ya kukuonyesha kuwa tatizo tulilonalo ni la kitaifa na linahitaji ufumbuzi wa kitaifa si wa chama kimoja au vyama vya upinzani peke yake.

Tunahitaji sasa uhuru wa pili. Tunahitaji kuanzisha mchakato wa kulikomboa taifa kutoka kwenye ufisadi unaojijenga hivi sasa. Hatunaye Baba wa Taifa kutuongoza na kutuonyesha jinsi ya kulitekeleza hili. Lazima tukae chini tutafakari mambo haya ili kwa pamoja tuvute kamba kuzuia maangamizi ya taifa letu. Mimi kweli naona wenzetu hawa hawana aibu kabisa kufanya maovu haya. Tunazo rasilimali nyingi mno, kiasi kwamba tunaweza kusema Tanzania ni Bustani ya Eden. Lakini kumezuka waroho na mafisadi wakubwa wanaotumia nguvu za dola kuruhusu uporwaji wake na wageni kwa kisingizio cha “uwekezaji”. Tusipogundua kuwa lugha ya “uwekezaji” ni lugha ya utandawazi inayohalalisha ubeberu hatutagundua ukweli kuwa “uwekezaji” ndio ufunguo wa umasikini wa mataifa ya dunia ya tatu. Sijui kama viongozi wetu wa leo wanatofautiana sana na Sultani Mangungo wa Msovero. Afrika imefilisika kiuongozi na tunahitaji sasa mapambano ya uhuru wa pili kuikomboa Afrika kutoka kwenye ubeberu huu unaojiita utandawazi.

Kumbuka uhuru wa pili ni dhana kubwa na nzito kifalsafa. Tutakuwa tunajipanga kupambana na Watanzania wenzetu ambao wamesimama upande mmoja na ubeberu. Hawa wanao ndugu, jamaa na marafiki wa ndani na nje ya nchi. Hawa wameshikilia hatamu za dola. Hawa wamejilimbikizia mabilioni ya fedha kuweza kumrubuni kila mtu mwenye roho nyepesi. Kwa pamoja hawa wanaunda tabaka la kinyonyaji na kifisadi linaloangamiza taifa. Tabaka hili halina aibu, huruma wala uzalendo.

Linajali matumbo yao tu na likishapora huhifadhi fedha na rasilimali hizo nje ya nchi. Hili ni tabaka hatari kabisa. Hivyo usiniulize kama wanamageuzi tumejipanga vipi, jiulize wewe uko upande gani katika harakati hizi, na uko tayari kufanya nini kwa ajili ya nchi yako. Mimi nikuulize: Je, kuna kabila la Watanzania linaloitwa “wanamageuzi”? Kama hakuna kwa nini mwanamageuzi awe mimi, asiwe wewe?

Swali: Je, unadhani ushirikiano wa vyama vya CUF, CHADEMA, TLP na NCCR-Mageuzi ni jambo makini na litakalofanikiwa?

Jibu: Mimi naona ushirikiano huo ni jambo zuri na la kuungwa mkono. Tuwape moyo waimarishe ushirikiano ule, labda utazaa mafanikio kama tutapata chama kimoja kikubwa cha upinzani nchini.

Swali: Je, wataacha ubinafsi na kuweka mgombea mmoja wa urais?


Jibu: Suala la mgombea mmoja wa urais si zito wala gumu kama kukubali kuunda chama kimoja. Tunachopigania ni kuwa na upinzani unaoleta maana, unaoweza kuiondoa CCM madarakani au kuligawa Bunge na serikali za mitaa ili chama kimoja kisiwe na ukiritimba wa siasa na maamuzi nchini. Hatutaki kuwa na Bunge la chama kimoja ambako wanakutana kama kamati ya chama na kufanya maamuzi kisha wakaingia bungeni na kupiga muhuri maamuzi yao.

Swali: Kuna baadhi ya Watanzania wanasema wanaotaka katiba mpya wanataka kugawana vyeo, wewe unasemaje?

Jibu: Ah! Hayo ni mawazo yao kama wanasema hivyo na ninayaheshimu. Mimi nataka katiba mpya na sina lengo la kugawiwa cheo chochote. Nataka katiba mpya kwa kuwa katika katiba ya sasa misingi ya demokrasia ni finyu sana. Lazima tuwe na katiba ya taifa huru la kidemokrasia ambapo kila raia ana haki sawa na fursa sawa. Nataka katiba inayoweka misingi ya demokrasia ya umma hivyo kwamba umma uwe na nafasi ya kuidhibiti serikali badala ya serikali kuudhibiti umma. Nataka katiba inayounda tume huru ya uchaguzi badala ya hii ya sasa ambapo uchaguzi unaendeshwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama.

Swali: Kwani ni kweli kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ndiyo inaendesha uchaguzi?

Jibu: Sijui ni lipi zuri, kujua ukweli na ukaishi kwa taabu na mahangaiko au kutojua chochote na ukaishi kwa amani mustarehe. Kamati ya Ulinzi na Usalama haina mamlaka ya kuendesha shughuli za uchaguzi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi na katiba ya nchi. Lakini katika utendaji, kamati hiyo ndiyo inapanga kila kitu na kutekeleza mikakati yote ya nani ashinde na nani ashindwe. Wananchi hupiga kura, lakini kamati hii huchagua nani awe kiongozi.

Swali: Rais Kikwete amesema tayari mikataba ya madini inadurusiwa. Tutapata sasa asilimia 30 kupitia kodi na mrahaba. Je, huoni hiyo ni hatua nzuri?

Jibu: Mimi namsifu Rais Kikwete kwa kutambua ukweli kuwa mikataba ile na sheria ya madini ina kasoro. Hilo ni jema kabisa. Sikubaliani naye kuwa asilimia 30 inatosha! Mimi nadhani tungepata asilimia sabini wawekezaji wakachukua thelathini. Sasa mwenye rasilimali ni nani, sisi au wawekezaji? Tatizo hapa ni woga tulionao kuwa wawekezaji hawatapatikana. Hiyo si kweli. Ramani ya madini ipo, wao hawaji hata kutafuta madini hayo, wanakuja kuchimba tu!

Nchi zenye sheria nzuri za madini huhakikisha kuwa migodi ni mali ya raia wake hivyo hata ukitoza asilimia 30 kodi na hata usipotoza mrahaba hupotezi kitu kwani rasilimali iko mikononi mwa raia wako. Tatizo hapa ni kuwa tunatoa bure rasilimali ya Watazania kwa wageni, jambo ambalo si la busara wala halali. Lakini kule migodini hatuna udhibiti kwa kujua kiasi gani cha madini kimepatikana. Wanachimba na kumimina dhahabu na kuondoka nayo bila sisi kujua wamepata kiasi gani. Wanachotuambia wamepata ndicho chetu. Watanzania tunayo tanzanite, dhahabu, almasi, na sasa tunayo pia mafuta. Kwa nini sisi ni masikini kuliko mataifa ambayo hayana kabisa rasilimali asili kama hizo? Kama mtu ataniambia kuwa tunao uongozi bora, sasa tumwombe Mungu atupe nini zaidi?

Swali: Unasemaje kuhusu ubinafsishaji wa sekta ya umma, huoni kama sasa uchumi wa nchi unapaa ukilinganisha na hapo zamani tulipokuwa tunafuata ujamaa?

Jibu: Wengi wanaozungumzia kushindwa kwa ujamaa hawaujui hata huo ujamaa ni kitu gani. Hebu nieleze hao wanaotetea ubinafsishaji wanaweza kuonyesha mradi gani mpya waliojenga ukiacha hizo mali zetu walizogawiana bure kwa kisingizio cha ubinafsishaji? Mimi naona ubinafsishaji ungeandaliwa vizuri ungetusaidia kwa maana kwamba rasilimali zile tungeziweka mikononi mwa wazawa au kuzibakiza mikononi mwa umma, lakini tukaruhusu wageni kuwekeza kama wabia. Tusingekubali kabisa kuwapatia rasilimali zile kwa asilimia zaidi ya hamsini. Kwa kufanya vile tulijikata miguu ya kuingilia kwenye ubepari, sasa tumekuwa viwete kiuchumi kwenye nchi yetu wenyewe.

Si kweli kuwa uchumi unapaa. Uchumi unaopaa ni wa nani? Labda ule wa wageni tuliowapatia rasilimali zetu bure. Kwa mfano serikali iliuza benki nzima ya Biashara ya Taifa kwa shilingi bilioni 15 tu, thamani ambayo hailingani na hata lile jengo yalimo hivi sasa makao makuu ya benki hiyo. Mara baada ya kukabidhi benki kwa wanunuzi, tuliwalipa wanunuzi hao bilioni 15 kama fedha za huduma za kibenki kutoka benki ya NMB. Sasa tuliuza benki hiyo kwa bei gani? Lakini pia tuliwapatia akaunti yetu ya dhamana za fedha za kigeni yenye dola milioni 80 hivi, kule Marekani. Unaweza kusema sisi ni wafanyabiashara wazuri kwa kufanikisha uuzwaji huo wa benki yetu? Naweza kuchukua mfano wowote wa ubinafsishaji na nitakuonyesha kuwa tulifanya madudu.

Swali: Hivi karibuni serikali imetangaza kuwa itapeleka bilioni 22 kila mkoa katika mchakato wake wa kupunguza umasikini, hili nalo walionaje?

Jibu: Ah! Ndugu yangu acha tu wapeleke, hazitakosa walaji hizo. Mimi siamini kuwa kila mtu anaweza kujiajiri au kuwa mwekezaji. Kuamini kuwa mtu ambaye hajawahi kufanya biashara na ambaye hana hata uzoefu wa biashara ataandika andishi la mradi na kufaulu kuanzisha biashara au mradi wa uzalishaji mali ni hatari. Ubepari haujengwi kiholela hivyo. Ubepari ni mfumo wa kisayansi kabisa wa uchumi. Ukiuendea kichwa kichwa utapoteza rasilimali za walipa kodi bure. Kumbe kwa kudra ya Mungu wako watakaoweza na pia wako wengi watakoshindwa. Tusishangae hayo yote mawili yakitokea kwa kuwa kweli hakuna maandalizi ya kutosha yamefanywa kwa mchakato huo.

Swali: Maandalizi gani hayo unadhani yangefanywa?

Jibu: Kila jambo litafanyika vizuri kama watendaji au wadau wake wataandaliwa kwanza kielimu. Mimi naona silaha dhidi ya umaskini ni elimu bora na afya bora. Mengine yanaweza kuja kama ziada. Taifa ambalo linaweza kuamua kuwa vijana wake walioko nje ya nchi kujitafutia elimu hawana haki ya kusaidiwa wanapokwama kama wale waliokwama kule Ukraine bado halijajiweka sawa kupambana na umasikini. Tuko tayari kuchangia harusi, vifo, michezo na kadhalika, lakini tunasita kutoa fedha za kodi zetu kuwasomesha vijana wachache tu ambao wamekwama kule Ukraine.

Mimi sioni mfungamano wa kisera wa malengo yetu. Iko wapi mipango ya elimu ya ujasiriamali kwa hao watakaokopesha mabilioni hayo? Je ni kitu gani shilingi milioni moja katika biashara au mradi wa kukimu familia ya kawaida yenye watu wanne hivi? Zipo nchi zinayo miradi ya kujikimu kwa raia wake. Lakini nchi kama hizo hazitoi mikopo holela kwa kila mtu. Zinatoa mikopo kwa watu waliokwishahitimu kiwango fulani cha elimu na pia utaalamu wa mradi unaoombewa fedha. Kisha wameunda taasisi ya kifedha yenye wataalamu wa kusimamia mafunzo ya miradi, uendeshaji wa miradi na usimamizi wa miradi kwa wanaokopeshwa hadi miradi yao iweze kujiendesha. Hili si jambo dogo la kukurupuka.

Swali: Eleza mtazamo wako wa serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambayo imebakiza miezi michache itimize miaka miwili tangu iingie madarakani.

Jibu: Mimi naona wamewaahidi watanzania mbingu, lakini tulichopata ni jehenamu. Maisha yetu sasa ni hoi bin taabani. Wakubwa uchumi wao binafsi unapaa, sisi walalahoi tumechoka! Kiutendaji inaonekana katika kila jambo kuna ‘usanii’ mwingi, lakini tunachokipata ni duni kabisa. Sipendi kubeza wala kudanganya. Je, walimu bila elimu ni jambo jema kwa elimu ya taifa? Mimi naona ni kujidanganya tu kudahili wanafunzi na kuwajaza kwenye madarasa bila walimu. Si kila mtu anaweza kuwa mwalimu, hiyo kazi ni wito, lakini pia ni taaluma.

Unaweza kusifiwa kwa kuanzisha chuo kikuu kipya, lakini chuo hicho kina wahadhiri? Na je, hivyo vyuo vikuu vilivyopo umevifikisha wapi? Mimi naona tumekwama hapo, vyuo vikuu tulivyonavyo hatuna uwezo kuviendeleza, ila tunajenga vingine! Kwa nini hatuoni kwamba kuendeleza na kupanua vyuo vilivyopo ni bora kuliko kujenga vipya? Sasa naona elimu ya juu imevamiwa kimamluki. Wale binafsi wanatoa tu vyeti bila kujali viwango vya elimu kwani akifeli mwanachuo watakula wapi? Mimi naona hayo si mambo mazuri kwa taifa letu. Maendeleo ya taifa hutegemea elimu, na tukichezea elimu tunachezea uwepo wa taifa letu. Tutakuwa na watu wenye vyeti, lakini wasio na elimu. Tutashindwa katika kila jambo tutakalotaka kulifanya kwa kuwa hakuna jambo linaloweza kufanywa na mbumbumbu.

Mimi naona utendaji wa papara katika kila jambo, lakini kwa kweli hakuna serikali inayoweza kufanya kila kitu. Wangechagua mambo machache wakayafanya vizuri badala ya kupapasa kila kitu na kukifanya vibaya. Naona uchungu kabisa kuona jinsi wanavyoachia rasilimali asili kuporwa na wageni. Hilo nina uchungu nalo na sioni woga kulisema. Sheria ya madini ni bomu na viongozi wa awamu ya tatu na ya nne walaumiwe kwa hilo. Naona pia uchungu kwa ubinafsishaji holela wa rasilimali zetu. Tulijiuza rahisi mno, hilo ni jambo ambalo sioni cha kujivunia. Naona pia kuwa ufisadi umekithiri na umegubika serikali nzima. Hii kashfa aliyoibua Kabwe Zitto na ile anayoizungumzia Dk. Willbrod Slaa ni ishara mbaya kwa taifa letu. Wakubwa wengi wanadanganya na kulihujumu taifa.

Mimi naona hayo yanatosha, hakuna haja ya kuzungumza mengi kwani yanatia uchungu. Watanzania wawe tu na juhudi na ushujaa wa kukabiliana na hayo, wasikate tamaa. Sisi wanamageuzi tutaendelea kueleza kasoro hizi, si kwa nia mbaya ila kwa kuwa bila ukweli, hakuna haki na bila haki taifa huangamia.

Swali: Sasa ni jambo gani la kuwatia moyo Watanzania unaweza kulisema?

Jibu: Kwa Watanzania wenzangu sote tunajua hali tuliyofikia. Wengi hatuna chakula, mavazi, tiba na watoto wao hawapati elimu. Hatuhitaji nguvu nyingi kuelezea hali mbaya tuliyomo kijamii na kiuchumi. Lakini hali hii isitukatishe tamaa kwani hakuna shida isiyo na mwisho na penye nia pana njia. Najua kila mwananchi sasa ni mwanamageuzi. Tulipoanza tulikuwa wachache. Sasa kila mmoja ni mwanamageuzi. Hili halina rangi za vyama kwani umasikini hauna chama. Lazima tujifunze sasa na kwa haraka jinsi gani ya kubadili hali zetu kwa kujikomboa wenyewe badala ya kungojea ukombozi uletwe na serikali. Nadhani kwa hili tuko mbioni kufikia hatua ya mgeuko kote nchini.

Lazima mbinu za mageuzi zibadilike haraka. Hatuwezi kufunzwa mbinu za mageuzi na walio madarakani. Inawezekana sasa tukaamua kubadili kabisa mchakato wa mageuzi kwa jinsi ambayo italeta tija na kupunguza hasara ya upotevu wa muda na rasilimali. Kwa kuwa wenzetu walio madarakni wamejikita katika ufisadi, wizi wa kura, matumizi ya dola kubaki madarakani na kila jitihada ya kuleta mageuzi kwa amani wanazipiga vita, inawezekana tukaziacha mbinu za sasa na kuona jinsi nyingine ya kuleta mabadiliko. Sijui tutachagua njia ipi, lakini wakati ukifika njia itapatikana. Hakuna linaloshindikana wananchi wakiamua.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0755 312 859; barua pepe; katabazihappy@yahoo.com na tovuti; www.katabazihappy.blogspot.com


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2007 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570