jumapili, 11 Novemba 2007

Hili la Mahakama ya Kadhi linamhusu Rais Kikwete

TAHARIRI


TAIFA linaelekea kuingia kwenye mgogoro mwingine mbaya wa udini, ambao kama hautatafutiwa ufumbuzi sasa, ukaachwa uendelee kuenea, madhara yake yanaweza kuwa ni maafa makubwa kwa Watanzania wenyewe.

Chanzo cha mgogoro huu ni kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, jambo ambalo sasa waumini wa dini ya Kiislamu wanaidai serikali ilitekeleze, kama ilivyoahidi katika ilani yake ya uchaguzi.

Ahadi hii ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndiyo iliyowafanya Waislamu kuanzisha harakati, kama aina ya shinikizo kwa serikali, wakiitaka itekeleze haraka uanzishwaji wa mahakama hiyo.

Tunatamka kwa kujiamini kuwa, madai ya Waislamu yana msingi kwa CCM na Rais Kikwete.

Tunasema hivi kwa kurejea ahadi iliyotolewa na Rais Kikwete na CCM kwa Waislamu, ambayo kwa hakika, sisi tunaamini ilimuwezesha Rais Kikwete kushinda kwa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Msimamo wetu huu, haumaanishi kuwa tunaunga mkono kuanzishwa kwa mahakama hiyo kwa sababu tunatambua kuwa Tanzania si nchi ya kidini. Hivyo kitendo chochote cha kuanzishwa Mahakama ya Kadhi kunaweza kufanya waumini wa dini nyingine nao kudai kuanzisha mahakama yao.

Kwa sababu hiyo basi, ingawa tunatambua wazi kabisa kuwa wanachodai Waislamu ni kutekelezewa kwa ahadi yao hiyo, sisi tunadhani busara isipotumika katika madai haya, basi kunaweza kuibuka mgogoro mkubwa wa kitaifa kulingana na mwenendo wa mambo ulivyo sasa.

Hatutaki kurejea katika sheria, katiba au historia ya nchi katika suala hili, kwa sababu tunaamini kuwa watawala waliotoa ahadi hiyo, waumini wa dini zote na Watanzania kwa ujumla wanazifahamu fika.

Ila tunachopenda kukizungumza katika hili, ni kwamba mgogoro huu ambao sasa umeanza kusababisha uhasama baina ya Wakristo na Waislamu, wanaoweza kuupatia ufumbuzi ni Rais Kikwete mwenyewe akisaidiwa na CCM kwa ujumla.

Tunasikitika kueleza kuwa, ahadi hii iliyotolewa na CCM na Rais Kikwete wakati wa kampeni za uchaguzi, ni moja ya ahadi mbaya ambayo madhara yake yanaanza kuonekana sasa.

CCM inafahamu fika kuwa Tanzania haiendeshwi kwa misingi ya dini, hivyo kuliingiza jambo hilo katika ilani yake ya uchaguzi, ilikuwa kukiuka taratibu.

Labda tuwakumbushe CCM kuwa, mwanzoni mwa miaka ya 1990, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alikataa Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC).

Sababu aliyoitoa ni kwamba, Tanzania si nchi ya kidini na alimwambia aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, John Malecela kuwa, kuruhusu jambo hili kufika bungeni ni kushindwa kwake, akiwa kama msimamizi mkuu wa shughuli za serikali bungeni, kusimamia msimamo wa serikali kutokuwa na dini.

Kwa kumbukumbu hiyo ya msimamo wa Mwalimu dhidi ya udini, tunadhani kwamba mbinu hii iliyotumiwa na CCM ili kuwashawishi Waislamu kumpigia kura Rais Kikwete, ni yenye mwelekeo wa kulielekeza taifa hili katika udini.

Kwamba Rais Kikwete ndiye aliyetoa ahadi hii, ambayo utekelezaji wake unapingwa na Wakristo, huku Mchungaji Christopher Mtikila akifungua kesi mahakamani, tunadhani ndiye mtu anayepaswa kuzungumza mapema kabla uhasama baina ya wananchi wake haujakuwa mkubwa.

Tunatamka hadharani kuwa, tutamuunga mkono Kikwete katika uamuzi wowote atakaoutoa katika hili, kwa sababu wakati akitoa ahadi hii, Watanzania walikuwa wanasikia, wakiwemo maaskofu, wachungaji na waumini wao.

Walimsikia akitoa ahadi hii mbaya kabisa, lakini hakuna aliyeonekana kumtilia shaka, wakamuita chaguo la Mungu! Kwa sababu hiyo, tunapenda kumuasa Rais Kikwete kuwa, kinachotakiwa ni kueleza msimamo wake kuhusu utekelezaji wa ahadi yake hii, ili Watanzania watulie, waache kukabana mashati kuhusu hili, kwa sababu ni dhahiri uamuzi wake ni wa mwisho.