jumapili, 11 Novemba 2007

Achana na Mtikila, mbane Kikwete
MASWALI MAGUMU

na Ansbert Ngurumo


UCHAMBUZI wangu Jumapili iliyopita kuhusu hotuba nzuri ya Rais Jakaya Kikwete na matendo haba ya uongozi wake, ilinipatia marafiki na maadui. Kusema kweli, kati ya watu 78 walionitumia ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu na barua pepe, ni wawili tu walionyesha hasira zao wazi wazi.

Wale 76 waliniunga mkono na hata kuandika maneno mengine makali ambayo, kwa maoni yao, yalinishinda kuandika au sikuyajua kabisa. Bahati nzuri niliweza kubaini kwamba mmoja kati ya wale wawili waliokasirishwa na maoni yangu, alikuwa anazungumza na kuandika kutoka ‘jikoni’ ingawa hakutaka kuweka wazi utambulisho wake.

Hakika, mmoja aliniahidi kunitumia hotuba ya Rais Kikwete ili niisome vizuri nione ‘uzuri’ uliomo, ambao hata mwakilishi wa wapinzani kwenye mkutano wa CCM, aliuona na kuusifia. Mwingine alitaka ‘tumpe muda’ rais, na ‘aliniomba’ niandike makala ya kumpongeza Kikwete kwa hotuba nzuri.

Kuna mambo ambayo wawili hawa hawakuyajua. Kwanza, nilikuwa na nakala ya hotuba. Sikuhitaji nyingine. Na nilikuwa nimeisoma na kuona uzuri wake -ule ule waliouona. Nilichokuwa nasisitiza katika makala yangu ni kwamba, Watanzania hawataishi kwa hotuba nzuri. Hadi sasa naamini kwamba rais anaweza kuongoza nchi vizuri bila hotuba.

Anachotakiwa kufanya ni kuweka mifumo na kuisimamia ikafanya kazi. Huu ndio utawala na uongozi. Lakini kama uongozi umegeuzwa kuwa sawa na ubingwa wa hotuba ambazo zinaandaliwa kwa malengo ya kisiasa, hapo ndipo baadhi yetu tutasema hakuna jipya na kazi haijaanza.

Pili, sijaelewa muda ambao wapambe wa rais wanataka tumpe. Kusema kweli tumeshampa, naye amejipa. Miaka miwili katika miaka mitano ni kipindi kizuri kuweza kumpima kiongozi na wasaidizi wake.

Tanzania haikupata uhuru mwaka 2005 baada ya uchaguzi mkuu. Kikwete alipoingia alisema mwenyewe kwamba mtangulizi wake, Benjamin Mkapa alimwachia misingi mizuri ya kuongoza nchi. Na aliwaonya wanamtandao wenzake waliokuwa wanaendeleza kampeni za kumbeza Mkapa, kwamba bila Mkapa hata yeye asingepata pa kuanzia.

Na kwa kutazama mahali ambapo Mkapa aliikuta nchi, hasa kiuchumi, Kikwete alikuwa sahihi kukiri hadharani kwamba ameachiwa nchi iliyo hai. Na alikuwa na kila sababu ya kuona matumaini kwamba ana mahali pa kuanzia.

Ni wazi tunakumbuka kauli zao za jeuri na dharau dhidi ya Mkapa kwa kudhani walikuwa na mwarobaini wa matatizo yaliyomshinda yeye. Lakini tunakumbuka pia mahali ambako Mkapa aliishia. Kwa hakika kama Kikwete anataka kuaminiwa, lazima akiri tena kwamba alikuwa na mahali pazuri pa kuanzia.

Kama si hivyo, yeye na wasaidizi wake watueleze walikuta mambo gani yameharibika kiasi cha kushindwa kuanza kazi. Na kama hawasemi, na kama mambo yanagoma katika miaka miwili tu ya uongozi wao, ni vema atarajie kuwa tutamkumbusha kauli zake mwenyewe. Kwa hakika, tumeshampatia muda. Kutokuhoji sasa ni kupoteza muda.

Kinachotakiwa sasa si yeye kudai tumpe muda; bali sisi ndio tunadai atupe muda – tumpime, tumhoji, tumshauri, tumtie moyo. Sasa ni zamu yetu kumhutubia; naye asikilize tunavyompima.

Kwa mfano, kuna suala hili la Mahakama ya Kadhi ambalo sasa limeleta mvutano mkubwa kati ya baadhi ya Waislamu na Mchungaji Christopher Mtikila.

Kikwete hana sababu ya kupewa muda. CCM imekuwa ikijitapa kuwa ni chama kinachotekeleza sera na ilani yake ya uchaguzi. Waislamu wanataka hili litekelezwe kama walivyoahidiwa. Serikali imeshashtuka. Haitaki tena kulitekeleza kwa sababu imeshapata kura za Waislamu.

Inachofanya sasa ni kulipiga danadana kwa kauli tamutamu na ahadi za kuliahirisha kitaalamu. Lakini wanaojua msimamo wa Kikwete na wasaidizi wake, wanasema wazi kwamba suala hili lilishawekwa kabatini.

Na linaweza kukaa kabatini hadi Kikwete akaondoka madarakani, maana ‘hataki limkute madarakani.’ Naye analiogopa. Lakini anakosa ujasiri wa kuwaambia ukweli Waislamu.

Bahati mbaya, nao wameangukia katika kundi linaloshiba hotuba na ahadi nzuri. Kwa bahati ya serikali pia, Mtikila amejichomeka na kugombana na Waislamu. Serikali imepumua kwa kuwa Waislamu sasa wanamtazama Mtikila badala ya kuitazama serikali.

Na wapo wanaomtuhumu Mtikila kwamba anatumiwa na serikali bila kujua ili kupoteza malengo. Mzigo huu utakapokuwa umeondolewa kwenye mabega ya serikali, hata kama serikali hatimaye itashindwa kutekeleza ahadi hiyo kwa Waislamu, Kikwete na wasaidizi wake wataibuka na kusema “suala hili bado linajadiliwa na taratibu za kisheria zinazingatiwa” au watasema “lipo mahakamani kwa sababu ya Mtikila.”

Wanaomjua Mtikila hawawezi kuacha kumtuhumu kwa kutumiwa. Waliomuona akienda Zanzibar kufanya kampeni za CUF na baadaye kuwageuka walipochelewesha malipo, wanaweza kulitazama suala hili kwa mtazamo huo. Wapo pia wanaodhani kwamba hata makundi kadhaa ya CCM yamewahi kumtumia Mtikila kumtuhumu Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye kwa maslahi ya kisiasa.

Wapo wanaosema ni harakati binafsi za Mtikila kwa sababu alishagundua siasa za mahakamani ndilo kimbilio lake baada ya kukataliwa na siasa za majukwaani.

Na wala simbezi Mtikila. Ukizitazama hoja zake, kwa watu wanaopenda mjadala wa hoja kwa hoja, utamsikiliza na kujibizana naye. Hiyo ndiyo kazi anayotaka kufanya na Waislamu, ingawa wao hawampi uwanja huo.

Ni wazi pia kuwa serikali ingeamua hata kesho kuwapa Waislamu mahakama yao isingeshindwa kufanya hivyo. Na kama inaona utaratibu wa kisheria kupitia bungeni unaleta mgogoro isingeshindwa kutamka kwamba Waislamu waanzishe mahakama yao wenyewe bila kuishirikisha serikali.

Lakini inajua kwanini inanyamaza. Haitoi uamuzi kwa sababu haina nia tena ya kuunda mahakama hiyo. Na imepata bahati sasa ya kuwagawa Waislamu kwa kumtumia Mtikila.

Itawachukua Waislamu muda mrefu kugundua kuwa wanapambana na mtu asiyehusika na ucheleweshaji wa ahadi ya Rais Kikwete na CCM; na sababu ni moja. Wameamua kusikiliza hotuba nzuri. Hawajapata ujasiri wa kudai matendo ya dhati.

Najua fika kwamba Rais Kikwete binafsi hakupenda wala hapendi suala hili la Mahakama ya Kadhi katika ilani ya uchaguzi ya CCM.

Bahati mbaya hakushiriki kuiandaa, lakini alishiriki kuinadi. Naamini hata yeye leo hajui ni nani aliliingiza suala hilo kwenye ilani. Na hata wakimpata leo, hawataondoa ukweli kwamba yeye (Kikwete) ndiye aliyezunguka nchi nzima analipigia debe.

Ndiye anayepaswa kudaiwa maelezo. Hawezi kubadili ilani ya CCM leo. Waislamu hawawezi kukubali kutumiwa kwa ajili ya kura na baadaye kupuuzwa tu kwa sababu ya hisia binafsi za viongozi wale wale.

Wanachopaswa kufanya ni kuachana na Mtikila na kumbana Kikwete. Na kama watasubiri hotuba nzuri kuhusu hili, wampe nafasi ataibuka siku moja na maneno matamu ya kuahirisha azma yao. Sijui kama watapiga makofi kumshangilia au watapaza sauti kumzomea.

Tuwaache wanaozibua masikio yao kwa ajili ya hotuba nzuri; na tuwaache waliofungua macho yao kuona mambo yakitendeka. Najua hatuwezi wote kuwa katika kundi moja.

Lakini kama tunataka kuwa wakweli, kama tunawatendea haki viongozi wetu, ni vema tuwakumbushe kuwa kampeni walizofanya kwa miaka 10 tulizisikia na kuziona.

Ahadi nyingine za nini leo wakati zile za awali hazijatekelezwa? Kwa nini kimya cha viongozi na mbinu zao za kuahirisha mambo zilete zogo katika jamii?

Hivi serikali ya awamu ya nne inadhani inaweza kuwapuuza Waislamu baada ya kuwatumia? Hata kama leo Mtikila anaweza kuisadia kwa muda, itaendelea ’kumtumia’ hadi lini?

Haya ni baadhi ya maswali tunayopaswa kuulizana na kuwauliza watoa ahadi. Kukusanyika mbele ya TV na redio kusikiliza hotuba tamu si dawa ya matatizo yetu.

Na kama wao hawajui, hotuba hizi ndizo zitatumika kesho kuwa vitanzi vya viongozi wetu. Sisi tunaompenda rais wetu tunamwambia wazi, hata kama mashabiki na mashushushu wake hawataki.

Katika suala hili la Mahakama ya Kadhi, ujumbe wangu kwa Watanzania leo ni huu: Achana na Mtikila, mbane Kikwete.

ansbertn@yahoo.com
www.ngurumo.blogspot.com
+447828696142