KARIBU kwa mara nyingine msomaji wa 'Asili ya Muziki' kwenye safu yetu ya uchambuzi wa kina wa chanzo cha mitindo mbalimbali ya muziki duniani.
Bado tuko katika mambo ya Sebene na leo tunaingia katika kituo cha kumi na mbili kinachotupeleka ukingoni kabisa mwa safari yetu ya takriban miezi mitatu ya kuuchambua mtindo huu.
Kama kawaida yetu, kwanza tufanye marejeo ya muhtasari wa yale tuliyoyachambua wiki iliyopita kabla ya kuendelea na uchambuzi wa kituo cha leo.
Tuliona athari za kijiografia ya kimuziki kwa eneo letu kwa kupokea mirindimo ya Afrika ya Kati kila inapobadilika, lakini pia nao waliotuambukiza walichanganya vitu vingi walivyovitoa sehemu mbalimbali kwa wakati mmoja na kupata kile tulichokipenda.
Hali ya kuingia kwa muziki huu wa 'mabolingo' ya kisasa yenye 'Sebene' ndani yake ikaturudisha nyakati za zamani, ambapo kila Mkongomani alionekana ni mtaalamu wa muziki.
Kuanzishwa kwa bendi zenye silika hizo mpya kukasababisha kuja kwa wimbi jingine jipya la Wakongomani wa kizazi kipya, wenye mambo mapya ya kimirindimo na unenguaji.
Kila mtu akawa ananengua, si wanawake wala waume, wote walitekwa na uchezaji mpya wa kisebene ulioingia na mambo yakazidi kunoga.
Tukaja kwenye jambo jingine muhimu la kisiasa lililochangia kwa sehemu kubwa kukua kwa Sebene hapa nchini, kuruhusiwa kwa uhuru wa kibiashara uliowezesha kuingizwa kwa bidhaa mbalimbali zikiwemo zana bora za muziki.
Hiyo iliondoa uduni wa maendeleo ya kiteknolojia, ambao awali ulitufanya tustaajabie midundo mikubwa kutoka zana bora za Wakongomani walipokuja kufanya maonyesho hapa nchini.
Bendi zilizoanzishwa katika mazingira hayo, ziliporomosha mirindimo mchanganyiko ya Kikongo na Kiswahili, lakini kionjo muhimu cha Sebene 'rapu' hakikuwa kimekaa sawa sawa bado.
Lafudhi za 'kibudu' jina lisilo rasmi la Kiswahili kilichopindapinda cha Kikongo, ndizo zilikolea zaidi kabla ya kuingia zile 'rapu' za kizalendo tulizopata siku za baadaye.
Tuliona pia jinsi Ukongomani ulivyotukuzwa hata na wanamuziki wa kizalendo hapo zamani, watu walijiita 'mapapaa' na kuongea Kiswahili kibovu cha Kikongo alimradi waonekane Wakongo.
Kuundwa kwa makundi ya wanamuziki mchanganyiko wa kizalendo na Kikongo, hatimaye taratibu kuliondoa mchanganyiko usioeleweka wa 'ukongo-utanzania' na kuleta ladha nyingine mpya yenye mwelekeo.
Mambo hayo yaliyojiri kutokana na teknolojia yalisababisha bendi ambazo zilishakuwepo, kujibadilisha na kwenda na wimbi jipya la kuporomosha mirindimo ya Kiswahili yenye ladha ya Kikongo.
Tukajikumbusha mambo ya ngoma za maghorofani, mambo ya 'Ngulupa Tupa Tupa' na 'Tukunyema mpaka chini' na wanenguaji wa kwanza kabisa wa mitaani, watu kama kina Kibengo Shabani 'Super Cadet' Tukafahamishana kuwa, kile kinachoonekana hivi sasa kama masebene mazito ya kibongo kwenye nyimbo za bendi mbalimbali, yalitokea kwenye mazingira hayo tuliyoyazungumzia awali.
Pia tuliona kuwa, maendeleo ya kibiashara ya kimuziki kimauzo yalichangia mabadiliko ya muziki huo uliovutia 'mapromota' na udhamini wa makampuni.
Tija ilileta ubunifu uliowabana Wakongomani, japo kadri siku zilivyozidi kupita wakaanza kutamba tena kwenye medani hiyo na kujenga upinzani mkubwa na wazalendo. Upinzani ambao wakati fulani ulivuka mipaka na kutaka kugeuka uhasama baina ya baadhi ya bendi, tulisimamia hapo wiki iliyopita katika kujenga picha ya kuelekea mwishoni mwa simulizi za Sebene.
Niliahidi kuwa wiki hii tutakuwa na sehemu ya mwisho ya uchambuzi wetu kwa kuzama zaidi hapa nyumbani.
Tukiendelea mbele na uchambuzi wetu, nianze kwa kunukuu kauli iliyowahi kutolewa na baadhi ya wanamuziki wa Kikongo waliotembelea hapa nchini miaka ya karibuni.
Walipoulizwa wanauonaje muziki wa kisasa wa dansi wa bendi za hapa nchini? Walisema kuwa kinachopigwa na bendi hizo ni mirindimo ya kwao ya Kikongo, huku lugha ya kuimbia ikiwa ya Kiswahili.
Natamani ningeweza kukutana nao wanamuziki hao na kuwauliza, je, wanauonaje muziki wa sasa wa bendi za Kikongo za hapa nchini?
Sijui jibu lao lingekuwa lipi, japo pale zamani sana walikuwa wanasema kuwa hawaujui muziki wa Kitanzania. Jambo ambalo sidhani kama ni kweli, maana hata ile 'Dada Asha' ya mzee Shem Karenga wasingeiiga kama wangekuwa hawaujui muziki wetu hata kidogo.
Nachojaribu kukuelekeza hapa kutokana na hoja hizo hapo juu, ni mchanganyiko wa siku za karibuni uliozaa kilichopo sasa.
Maana mpaka sasa tumeshajua jinsi Sebene lilivyoanza hadi lilipotufikia sisi hapa nchini, lakini majibu ya yale maswali waliyoulizwa wanamuziki wa Kikongomani niliyoyanukuu hapo juu ndiyo yanatupa mwelekeo wetu.
Kwamba tunachopiga ni muziki wenye mirindimo yao, lakini tunauimba kwa lugha yetu, kwamba wangejibu nini kuhusu bendi za Kikongo zilizopo hapa nchini hivi sasa kwa mirindimo zinazoporomosha.
Kwa vyovyote jibu lingekuwa, wanapiga muziki wa kwao, lakini wanatumia sana nguvu ya lugha yetu ya Kiswahili kuukubalisha muziki huo.
Hiyo inathibitisha kuwa mirindimo iliyopo hivi sasa katika dansi ni mchanganyiko wa mitindo na mambo mbalimbali kama ambavyo tumeona tangu awali.
Sebene lililopo hivi sasa limevaa taswira ya Kitanzania zaidi kuliko lilivyoingia, huku likipitia vipindi kadhaa vya mabadiliko tokea pale zilipoundwa bendi za Kikongomani hadi sasa.
Kutoka Kiswahili kibovu kilichoimbwa na 'rapu' zilizokaa tenge, muziki huo ukaanza kujenga taswira sahihi kwa ubunifu wa wanamuziki wazalendo waliobadili kile kilichoonekana cha kigeni kuwa cha kinyumbani.
Ubunifu mpya wa mirindimo ukazalisha Sebene zito lisilo na mwendo wa kasi sana lakini likichezesha hasa na kuvutia.
Wale watu muhimu wanaolijenga Sebene, wapiga drums, marepa na wanenguaji wakaleta ubunifu wa kuingiza 'chuchizo' zilizoeleweka zaidi kwa mashabiki wa nyumbani na kuzusha ushindani mkubwa.
Ubunifu huo wa mambo ya kinyumbani ukahamisha kwa kiasi kikubwa muziki huo kutoka Ukongo hadi Utanzania, japo si kwa ujumla kamili.
Kawaida hakuna ukamili wa kujitegema kwa kila kitu kwenye mtindo wowote wa muziki duniani.
Nikisema hakuna ukamili wa kujitegemea kabisa kwenye mitindo ya muziki, katika hili la Sebene, nakurudisha hapo juu kwenye mchanganyiko wa mirindimo na lugha katika kupata midundo safi inayokubalika.
Jambo la mwisho ninalotaka kukufahamisha ni kuwa, sina shaka unawafahamu wanamuziki wanaoporomosha miondoko hiyo hapa nchini kwa sasa.
Watu kama kina Abuu Semhando, Ramadhani Masanja 'Banza Stone' Ally Choki, Muumin Mwinjuma, Chalz Baba, Msafiri Diouf, Rogart Hega 'Catepilar' na wengi wengineo.
Hawa wanatupa msingi wa mchanganyiko kutokana na walikotokea na kuivishwa, ndiyo maana nikasema kuwa, kilichopo au kinachopigwa hivi sasa ni cha kinyumbani zaidi kisebene kuliko kilipokuja hapo mwanzoni.
Unapoiangalia bendi kama African Stars 'Twanga Pepeta' kwanza hilo jina lenyewe tu la mtindo wao ni la Kitanzania zaidi kuliko kigeni 'Kikongo'.
Wanaporomosha midundo ya nyimbo zao kwa kuimba kwa ghani zao zenye lafudhi za kinyumbani, kisha kinakuja kipande cha pili cha 'chemka' tunayoiita 'Sebene'.
Hapo ndipo unapata mapigo ya magitaa yaliyoelemea zaidi ladha za upande wa Afrika ya Kati.
Nadhani unanipata msomaji, kwamba muziki hauna mipaka na mirindimo huvuka mipaka, kuteka hisia na kukubalika hadi sehemu za mbali na ulikoanzia.
Kama ambavyo tumeona safari yetu ilivyoanzia Marekani ya Kusini, ikapitia Marekani ya kaskazini, Afrika ya kaskazini, hadi kufika Afrika ya Kati.
Hatimaye mirindimo hiyo ilitua Afrika ya Mashariki kabla haijaanza tena safari ya kurudi Afrika ya Kati na kuishia Ufaransa.
Kutoka huko ikaanza kuteremka tena upande huu ikiwa na mabadiliko kutokana na vionjo ilivyochota katika mzunguko wote mzima.
Ndipo tukapata tulicho nacho hivi sasa kwa ubunifu wa wanamuziki wetu, wakikiweka kwenye taswira yetu zaidi iliyo tofauti na awali midundo hiyo ilipotufikia.
Msomaji, hadi hapa ndipo tunafika mwisho wa safari yetu ya uchambuzi wa Sebene, natumaini umeelimika, kufurahia na kuburudika na yote niliyoweza kukuletea.
Japo sikuweza kukuletea kila kitu kutokana na urefu wa historia na fursa tuliyo nayo, lakini kama tulikuwa wote tangu mwanzo najua unakumbuka tulikopita.
Kama hatukuwa wote tangu mwanzo, basi Jumapili ijayo nitafanya majumuisho ya yote tuliyoyachambua tangu mwanzo hadi mwisho. Tukikamilisha majumuisho hayo tutakuwa tumehitimisha mambo haya ya Sebene, kabla ya kuanza kuuchambua mtindo mwingine wiki inayofuatia. Alamsiki!
Mwandishi wa makala hii ni mwanamuziki mkongwe wa miondoko ya reggae hapa nchini. Kwa maoni na ushauri anapatikana kwa simu namba: +255 752 227 594, barua pepe : rasinnonganyagwa@yahoo.com