BARAZA Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) limetoa tuzo za heshima kwa watu watano kutokana na mchango wao katika jamii.
Waliotunukiwa tuzo hizo ni Mkuu wa Vodacom Foundation, Rechal Phares, Mkrugenzi wa ITV na Radio One, Joyce Mhavile, Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Charles Kimei, mfanyabiashara Mustafa Sabodo na Mbunge wa Viti Maalum, Amina Chifupa (CCM). Hata hivyo, Amina hakuwapo wakati wa utoaji wa tuzo hizo.
Walitunikiwa tuzo hizo juzi na mke wa rais, Mama Salma Kikwete katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Tuzo hizo zilizopewa jina la Upendo wa Kweli, ni kwa ajili ya kuthamini mchango wa wahusika kwa jamii, hasa kusaidia vijana na watoto yatima.
Akizungumza baada ya kukabidhi tuzo hizo, Mama Salma, alisema: “Juni 16 tuliadhimnisha siku ya watoto kimataifa. Hii ni suku ambayo watu wote duniani tuliyakumbuka maandamano ya wanafunzi wa Soweto nchini Afrika Kusini. Mamia ya watoto waliuawa wakiwa wanadai haki zao pamoja na nchi yao.
“Mfuko wa Vodacom Foundation umekuwa ukihudumia watoto waishio katika mazingira magumu, walioathirika na virusi vya ukimwi kwa kugundua mahitaji yao na kuandaa mikakati madhubuti, ili kuwasaidia kwa kujitolea muda wao, misaada mbalimbali na kuwapatia vitu vya kuwawezesha.”
Phares aliishukuru Bakwata na Mama Kikwete kwa kugundua yote hayo na kuzithamini kazi nyingi zinazofanywa na Vodacom Foundation.
Hafla hiyo iliandaliwa na Bakwata kwa kushirikiana na Chama cha Kuendeleza Michezo na Kupambana na Ukimwi (TASCA).
Katika hafla hiyo, zilichangwa fedha taslimu sh milioni 55 na ahadi ilikuwa sh 118.9 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa shule ya watoto yatima inayojengwa na Bakwata kwa kushirikiana na TASCA.