VIONGOZI wa muungano wa vyama vya siasa kambi ya upinzani nchini, wamedhamiria kuwaeleza wananchi mapungufu yaliyopo kwenye bajeti ya serikali, iliyosomwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, alisema ziara hiyo itaanza kesho, mkoani Kigoma ambako Rais Jakaya Kikwete aliahidi kujenga uwanja wa ndege wa kisasa katika mkoa huo wa pembezoni mwa nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye ofisi za makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), Buguruni, jijini Dar es Salaam, Mrema aliiponda bajeti hiyo kwa maelezo kuwa haina huruma kwa wananchi wake, hali inayopoteza dira na mwelekeo wa kauli ya Rais Kikwete ya maisha bora kwa kila Mtanzania.
Alisema, ahadi za rais hazitatekelezeka kutokana na ugumu wa maisha utakaowakabili Watanzania wenye kipato kidogo baada ya kodi ya mafuta kupanda.
Mrema alisema, akiwa mkoani Kigoma, Kikwete aliahidi kuwa serikali yake itajenga uwanja wa kisasa wa ndege, lakini katika bajeti hii, serikali imetenga sh milioni 100 kwa ajili ya uboreshaji wa uwanja wa ndege wa mjini Mwanza na Kigoma.
Alisema fedha hizo ni kidogo kujenga viwanja viwili, na kulaani kitendo cha serikali kutenga sh bilioni 5.6 kwa ajili ya ukarabati wa ofisi ya rais (Ikulu) na sh bilioni 1.7 kupelekwa kwenye ukarabati wa ofisi ya waziri mkuu.
“Haiwezekani Ikulu ikarabatiwe kwa sh bilioni 5.6 halafu sh milioni 100 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya viwanja viwili vya ndege, tena vya kimataifa… kuona hivyo, waziri mkuu nae akapata sehemu ya kuvuna pesa, eti nae anakarabati ofisi yake kwa sh bilioni 1.7.
“Hivi kuna kitu gani pale kinachofanya kila mwaka jengo hili lifanyiwe ukarabati? …katika bajeti ya mwaka 2005/06 jumla ya sh bilioni 3.23 zilitengwa ili kukarabati Ikulu, mwaka 2006/07 zikatengwa sh bilioni 6.12, mwaka huu wamejiwekea sh bilioni 5.6. Jamani, huu ni usanii.
“Haya wameona hakuna pa kupatia fedha, safari hii wameongeza bajeti ya ukarabati wa ofisi ya waziri mkuu, na yenyewe mwaka jana walitenga sh bilioni moja, safari hii wameongeza hadi kufika sh bilioni 1.7, kuna nini hasa kwenye ofisi hizo kiasi cha kuzifanyia ukarabati wa gharama kubwa kila mwaka?” alihoji Mrema.
Alisema: “Tunakamuliwa kwa ajili ya kuwashibisha watawala wetu, halafu wanasema maisha bora kwa kila Mtanzania, si kweli, hii bajeti imeongeza pengo na kuimarisha tofauti kati ya matajiri na fukara nchini.
“Viongozi hawa wana nia mbaya na Watanzania, wamejitafutia ulaji baada ya kuona mianya ya rushwa imezibwa, hivyo wanatafuta pa kujineemesha wao na matumbo yao.
“Mwanzoni viongozi walikuwa wananeemeka kwenye sekta za viwanda, machimbo na nyingine zilizokuwa mali ya umma, sasa wameuza vyote, hawana namna, wanataka kutukamua tusio na uwezo kifedha.
“Shilingi trilioni 6.06 ni fedha nyingi zinazoweza kuleta mabadiliko ikiwa zitatumika ipasavyo kwa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa, lakini kutokana na ubabaishaji wa viongozi tuliowachagua, maisha ya walalahoi yatazidi kuwa magumu.
“Watanzania haya tunayoyaona ni matokeo ya viongozi wababaishaji, walioamua kuunda serikali ya kisanii, huu ni ukweli, lakini tukisema tunaambiwa tunawakashifu na kuwadharau viongozi wetu,” alisisitiza Mrema na kuongeza kwamba, watahakikisha wananchi wote wanaelewa kilichomo kwenye bajeti hii, ili waone tofauti ya kauli za watawala wetu na hali halisi ya maisha.
Akizungumzia kuhusu nafasi ya kilimo katika bajeti hiyo, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema sekta hiyo muhimu inaendelea kupewa mgongo hali inayohatarisha ustawi wa jamii yetu ambayo kwa asilimia 90 kilimo ni uti wa mgongo.
Lipumba alisema, tafsiri pana ya kilimo kwa mujibu wa bajeti ya mwaka huu, sekta hiyo mama hapa nchini imetengewa sh bilioni 379.578 sawa na asilimia sita ya fedha za bajeti nzima.
Alisema, Tanzania imekwenda kinyume na makubaliano ya nchi za maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC) ya kutenga asilimia 10 ya fedha za bajeti kwa ajili ya kilimo ili kukuza sekta hiyo.
Aidha, aliongeza kuwa, fedha nyingi katika bajeti hiyo zimeelekezwa kwenye matumizi yasiyo ya lazima.
“Uchambuzi wa kina wa matumizi ya serikali katika idara na wizara zake, unaonyesha sehemu kubwa ya bajeti hiyo inatumiwa na watawala.
“Pamoja na kwamba watumishi wa serikali wanalipwa mishahara, lakini lipo fungu kwa ajili ya kuandaa bajeti ya kawaida na ya maendeleo, kuandika hotuba ya bajeti na kadhalika… aidha, inakadiriwa asilimia 38 ya bajeti ya Wizara ya Elimu wakati sehemu kubwa inatafunwa katika posho za vikao na masurufu ya safari,” alisema Lipumba.
Mbali na ahadi ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa mkoani Kigoma, Rais Kikwete aliahidi kuwa serikali yake itajenga kituo cha kuzalisha umeme cha Mto Malagalasi ili kuondoa kero ya umeme kwa wakazi wa Kigoma, lakini bajeti ya Wizara ya Nishati haionyeshi mradi huo.
Aidha, Lipumba alisisitiza uwepo wa bajeti mbadala yenye mwelekeo chanya kwa Watanzania wote, itakayoonyesha utekelezaji wa ahadi za kimaendeleo nchini.
Wakati huohuo, Lucy Ngowi anaripoti kuwa, wakati wananchi wengi wakiilalamikia bajeti ya serikali iliyowasilishwa bungeni mwishoni mwa wiki, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, kinaiunga mkono.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, Kapteni John Barongo, alisema CCM inaamini kuwa bajeti hiyo ni ya aina yake katika historia ya Tanzania, kwa maana ya kulenga katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi mkuu ya chama hicho mwaka 2005, ambayo shabaha yake kuu ni kuchochea maendeleo ya wananchi.
“Hii ni bajeti ambayo pia inalenga moja kwa moja katika kupambana na kuwatoa Watanzania katika umaskini, kama ilivyoahidi na kuainishwa katika ilani hiyo ya uchaguzi ya mwaka 2005,”alisema Barongo.
Alisema Serikali ya CCM imeamua kuelekeza nguvu zake katika miezi 12 ijayo ya fedha katika mambo ya msingi yanayohusu wananchi kama elimu asilimia 18, miundombinu asilimia 12.8, afya asilimia 10, kilimo asilimia 6.2 na maji asilimia 5.1.
“Ukiondoa miaka ya mwanzo ya uhuru wa nchi hii, mara ya mwisho ikiwa mwanzoni mwa miaka ya 1970, wakati serikali ilipotangaza elimu bure kwa ngazi zote, haijapata kutokea dira ya serikali katika bajeti ikawa ya wazi na kuwalenga wananchi kama ya mwaka huu,” alisema Kapteni Barongo.
Kwa mujibu wa Barongo, pale serikali ilipolazimika kupandisha kodi, imefanya hivyo kwa nia na dira thabiti, yaani kujaribu kupata fedha zaidi za kuwekeza katika shughuli za kuboresha maisha bora kwa kila Mtanzania.
Alisema serikali pia imechukua hatua nyingine muhimu ambazo zitapunguza ukali wa maisha ya wananchi kwa kuahidi kupandisha mishahara ya wafanyakazi, kupunguza ushuru wa vyakula nchini na inapunguza kodi ambayo wafanyakazi wa nchi hii wanakatwa kwenye mishahara yao.
CCM Mkoa wa Dar es Salaam, inatoa wito kwa wananchi na wabunge kuijadili bajeti hiyo kwa namna ya kuiboresha kwa manufaa ya wananchi.