KAMBI ya Upinzani bungeni jana iliwasilisha bajeti mbadala ikijibu hoja za Waziri wa Fedha, Zakia Meghji na Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa.
Waziri Kivuli wa Fedha, Hamad Rashidi Mohamed (Wawi-CUF), alieleza kusikitishwa kwake na matumizi makubwa na yasiyo na tija serikalini.
Hamad katika hotuba yake iliyochapishwa ndani ya gazeti hili, aliorodhesha njia mbalimbali ambazo zikitumika sawa sawa zitaisaidia serikali kupunguza utegemezi kwa wahisani kutoka asilimia 42 za sasa hadi kufikia asilimia 31, huku akipendekeza bajeti iongezwe kutoka sh trilioni 6.06 za sasa hadi kufikia trilioni 8.
Aidha, Hamad katika hotuba yake alisema wapinzani wamebaini upotevu wa makusanyo katika wizara na idara tano yasiyopungua sh 73.8 bilioni na kwamba hadi kufikia Juni mwaka huu misamaha ya kodi aliyoielezea kuwa ni ya kutisha itakuwa imefikia sh 673 bilioni.
“Hiki ni kiasi kikubwa kwa nchi inayoomba misaada kila kukicha. Kambi ya upinzani inaona huu ni upungufu mkubwa wa mapato ya wanyonge - Watanzania kwa kuyatupa bila utaratibu wa wazi na unaoeleweka,” alisema Hamad.
Katika vipaumbele vyao katika mgawanyo wa fedha za bajeti, wapinzani walisema kuwa wangetoa kipaumbele kikubwa kwa sekta ya miundombinu, ili kufungua uchumi wa nchi na kuwawezesha wananchi kujijenga kiuchumi.
Hamad Rashid katika hotuba yake hiyo alisema sekta ya miundombinu wangeitengea asilimia 21 ya bajeti yote, sawa na sh bilioni 1,678.734 ikifuatiwa na sekta ya elimu ambayo ingetengewa asilimia 20 ya bajeti yote, sawa na sh bilioni 1,598.794.
Meghji katika hotuba yake, alisema serikali ilitenga asilimia 18 kwa elimu ambayo ndiyo ilikuwa sekta inayoongoza kwa kutengewa fedha nyingi na ikafuatiwa na afya huku miundombinu ikitengewa asilimia 10 ya bajeti nzima.
Kwa mujibu wa Hamad Rashid, kilimo kingepewa asilimia 12 ya bajeti sawa na sh bilioni 959.277 badala ya asilimia sita za sasa, wakati afya ingepewa asilimia tisa sawa na sh bilioni 719.457. Nishati asilimia nane sawa na sh bilioni 639.518 na maji asilimia saba sawa na sh bilioni 559.578.
Alisema huo ni ushauri unaotolewa kwa serikali kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi na kuondokana na bajeti tegemezi.
Hamad alisema pia kuwa, bajeti yao hiyo italiwezesha taifa kuwa lililoelimika na lenye utawala unaoheshimika.
Kuhusu ndege mpya ya rais, Hamad Rashid aliitaka serikali kuiuza ndege hiyo ambayo alisema inatumia sh milioni sita kwa saa moja kuruka, na kuongeza kuwa fedha zitakazopatikana ziongezwe kwenye ujenzi wa barabara za kusini.
Aliongeza kuwa ndege hiyo imegeuka kuwa mzigo kwani gharama za kuitunza ni kubwa mno na kuwa uamuzi wa kuiuza utaiwezesha serikali kuongeza mapato kwa sh bilioni 35.
“Ndege hiyo iliyonunuliwa kwa gharama ya sh bilioni 42 inao uwezo wa kutua katika viwanja vitano tu nchini, ambapo hata katika mji wa Dodoma ambayo ndiyo makao makuu ya nchi haiwezi kutua,” alisema.
Alisema bajeti ya mwaka 2007/08 iliyosomwa na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji wiki iliyopita, haimsaidii mwananchi mwenye kipato cha chini kutokana na kupanda kwa kodi ya mafuta yote wakati ikifahamika kuwa mwananchi
anategemea zaidi nishati ya mafuta ya taa.
Alisema serikali imepanga fedha nyingi zaidi kwa ajili ya matumizi ya kawaida kuliko matumizi ya maendeleo, na kwamba suala hilo linadhihirisha wazi kuwa, ukubwa wa serikali unasababisha matumizi makubwa ya kawaida.
Hamad alisema, ili kupunguza rushwa na bajeti tegemezi, serikali haina budi kuweka utaratibu ulio wa wazi katika kutoa misamaha ya kodi ili wanaosamehewa wajue kwamba, hawadaiwi kodi hizo.
Wakati huo huo, Kambi ya upinzani imeitaka serikali kutoa ufafanuzi kuhusu gharama halisi zilizotumiwa na serikali katika ujenzi wa majengo ya Benki Kuu (BoT), kwani upo utata kuhusu gharama hizo.
Hamad Rashidi alisema wanavyofahamu wao, ni kuwa ujenzi huo umegharimu dola za Marekani milioni 34, kiasi alichosema ni cha juu kuliko hata kujenga jengo la kifahari katika majiji makubwa duniani kama New York, nchini Marekani.
Pia aliomba ufafanuzi kuhusu uwekezaji wa BoT katika Kampuni ya Mwananchi Gold Mine, kwamba kama bado inaendelea kuwekeza katika kampuni hiyo binafsi na iliwekeza kiasi gani na jumla ya mapato yaliyopatikana.
Aliomba pia kupatiwa tathmini inayofanywa na BoT kuhusu mradi wa Nyumbu na Meremeta Gold Co. ambayo ilikuwa chini ya uongozi wa Time Mine ya Afrika Kusini na kudhaminiwa na BoT kwa dola za Kimarekani milioni 100.
Naye Waziri Kivuli wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji Kabwe Zitto, katika hotuba yake alisema hali ya uchumi kwa mwaka wa fedha uliomalizika ilionyesha kudorora kuliko ilivyokuwa mwaka uliotangulia.
Zitto alisema kuyumba kwa hali ya uchumi baada ya kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Nne kumetokana na kuporomoka kwa shilingi na kupungua kwa uzalishaji wa mazao kulikosababisha kushuka kwa pato la taifa.
Takwimu za kuporomoka kwa uchumi katika mwaka wa fedha uliopita, zinaonyesha kuwa thamani ya shilingi ya Tanzania kwa dola moja ya Marekani ilikuwa sh 1128.8, huku pato la taifa likiwa sh trilioni 13.
Aidha, kwa mwaka 2006 thamani ya shilingi ya Tanzania ilikuwa sh 1251.9 kwa dola moja ya Marekani, wakati huo pato la taifa lilikuwa sh trilioni 15, hali inayodhihirisha kuwa thamani ya fedha hapa nchini ilishuka kwa asilimia 10.9 na kufanya thamani halisi ya pato la taifa kuporomoka, alisema Zitto.
Mbunge huyo, aliainisha sekta tisa muhimu zinazosaidia kukua kwa uchumi ambazo ni kilimo, uchimbaji madini, bidhaa za viwandani, umeme na maji, ujenzi, biashara na mahoteli, mawasiliano na uchukuzi, fedha na huduma za biashara na uendeshaji wa serikali.
Akitoa mfano wa mporomoko huo, Zitto ambaye hotuba yake iko ndani ya gazeti hili pia alisema, sekta ya kilimo inayochangia sehemu kubwa ya pato la taifa ukuaji wake umeporomoka kwa asilimia 1.0.
“Kwa kuwa Tanzania inapima uchumi wake kutokana na thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa nchini…kushuka kwa ukuaji wa kilimo kunaashiria kuporomoka kwa uzalishaji katika sekta hii,” alisema Zitto.
Kwa upande wake Zitto alisema, kambi inaitaka serikali kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa madini kwenda nje ya nchi kunakofanywa na makampuni ya madini, kwa kuwa usafirishaji huu unapoteza fedha nyingi na maliasili za taifa.
Pamoja na hayo kambi hiyo pia ilielezwa kushangazwa na hatua ya Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Juma Ngasongwa, kutozungumzia sekta ya mafuta na gesi asilia kwa kina na kwenda kinyume na maelezo ya serikali kuwa sekta ya viwanda imekua.
Kabwe, alisema sekta muhimu katika uchumi wa nchi iliporomoka, hali iliyosababisja kushuka kwa ukuaji wa sekta ya viwanda na kuthibitisha athari za mgawo wa umeme zilizolikumba taifa letu kinyume na kauli za serikali kwamba mgawo wa umeme haukuathiri uchumi. Alisema, pia wakati umefika kuangalia uwezekano wa kuifanya mikoa ama mmoja mmoja au kikanda ijitegemee katika uzalishaji wa nishati ya umeme ili kuchochea maendeleo sawa kwa mikoa yote.
Aidha, kambi hiyo imeitaka serikali kueleza mikakati ya utekelezaji wa miradi ya umeme badala ya kuwekeza katika miradi ya dharura.
Kuhusu tatizo la ajira, kambi ya upinzani imependekeza kutizamwa upya kwa tatizo hilo kwa kufanya mchakato wa kuchambua vyema sera ya taifa ya ajira na kuwepo kwa mjadala wa kitaifa kuhusu ajira, ujira na tija.
“Tatizo la Ajira ni ‘bomu’ linaloweza kulipuka wakati wowote lisiposimamiwa vizuri,” alisisitiza Kabwe.