MAKAMU wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema Serikali ya Awamu ya Nne inafanya kila jitihada, ili kuhakikisha inatekeleza ahadi zake za kuwaletea maendeleo wananchi.
Akihutubia mkutano wa hadhara juzi katika Uwanja wa Ilulu mjini Lindi, Dk. Shein, alisema wakati wa kampeni mwaka juzi serikali iliahidi mambo mengi ya kuwafanyia wananchi katika kuleta maendeleo.
Alitaja baadhi ya ahadi hizo kuwa ni pamoja na kuimarisha huduma za jamii zikiwemo za afya, elimu na maji, ujenzi wa barabara na pia suala zima la kuimarisha bandari nchini.
“Ahadi ni deni, na tangu tumeingia katika madaraka, tumefanya mambo mbalimbali katika kutekeleza ahadi hizo,” alisema Makamu wa Rais.
Alisema jitihada zilizochukuliwa na serikali za kuendelea kuijenga barabara ya Kibiti – Lindi ambazo zinaonekana wazi na kila mmoja katika jamii ni miongoni mwa utekelezaji wa ahadi hizo.
“Wengi wenu mnaona jitihada hizi. Nami nikasema nije niione barabara hii, maana haya ni matunda ya maendeleo yaliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tatu na Serikali ya Awamu ya Nne tukaahidi kuyatekeleza kwa nguvu zote,” alibainisha.
Aidha, alisema utekelezaji wa ahadi hizo unaonekana pia upande wa elimu ambapo ameupongeza Mkoa wa Lindi kwa kujenga shule za sekondari zipatazo 62 katika kipindi cha miezi 18, hivyo kuweza kuwapeleka watoto wote waliofaulu sekondari.
Hata hivyo, Dk. Shein alielezea kusikitishwa kwake na tabia ya wanafunzi kukatizwa masomo kwa sababu ya mimba na kuagiza watakaopatikana na hatia ya kuwapa wanafunzi mimba wachukuliwe hatua za kisheria mara moja.
Katika mkutano huo, Dk. Shein alikabidhi hundi za mkopo wa sh milioni 150 kwa wanachama wa Ilulu SACCOS na kuwataka watumie vizuri fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.