JUMLA ya sh bilioni 4 zilitumika kwa ajili ya kupambana na homa ya bonde la ufa (RVF), Bunge lililezwa jana.
Maelezo hayo yalitolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk. Charles Mlingwa, wakati akijibu swali lililoulizwa na Lucy Owenya (Viti Maalumu-CHADEMA), alitaka kujua homa ya bonde la ufa ilipoingia nchini serikali ilichukua hatua gani za kufuatilia na kudhibiti ugonjwa huo.
Dk. Mlingwa alisema serikali ilifuatilia mwenendo mzima tangu ugonjwa huo uliopingia nchini ambapo mifugo
ilikaguliwa na jumla ya sampuli 5,360 kutoka kwa wanyama zilichukuliwa na kufanyiwa uchunguzi.
Alisema katika kuimarisha hali hiyo, serikali ilinunua chanjo kiasi cha dozi milioni tano na nusu kwa ajili ya kuchanja ng’ombe, mbuzi na kondooo sanjari na kutoa elimu na kuhimiza wananchi kujikinga.
Alisema tangu kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa huo, kulitokea milipuko minane iliyosababisha vifo kwa mifugo na binadamu.
Alisema hadi Februari na Machi 2007 kulikuwa na matukio katika vijiji 26 vya wilaya 10 za Mkoa wa Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Morogoro na Tanga.
Alisema katika kipindi cha Aprili na Mei 2007, matukio yalikuwepo katika vijiji 46 vya wilaya 19 za mikoa ya Dodoma, Iringa, Mbeya na Singida.
Alisema hadi Mei 31, mwaka huu, ng’ombe 46,680, mbuzi 56990, na kondoo 32,900 nchini kote walikuwa wameathirika, ambapo kati ya hao, ng’ombe 51,610, mbuzi 6,896 na kondoo 3,998 walikufa.
Alisema tangu ugonjwa huo kutokea hadi Mei 29, 2007, idadi ya wagonjwa 306 walilazwa na 15 kati yao bado wamelazwa hospitali wakitibiwa na 156 walitibiwa na kuruhusiwa huku 134 wakiwa wamefariki kutokana na RVF.
Alisema mikoa yenye wagonjwa waliofariki ni Arusha (watatu), Dodoma (85), Iringa (wawili), Manyara (wanne), Morogoro (13), Mwanza (wanne), Pwani (wawili), Singida (20) na Tanga (mmoja).