PAMOJA na makengeza yangu kuwa yamejaa michozi ni kijililia mimi na kura yangu niliyoichezea kwenye uchaguzi, nimeokoteza miwani yangu ya mbao na kuisoma kwa kina hotuba ya bajeti yetu ya mashaka.
Kwanza nisema wazi kuwa naanza kukubaliana mia kwa mia na wanaoiita serikali yetu kuwa haina nia ya kuondoa umasikini.
Sitasema mengi kwa hili nisijeonekana naitukana serikali ambayo kimsingi kwa jinsi mambo yanavyokwenda inajitukana yenyewe.
Kwanza natoa makosa. Katika hotuba ya bajeti ambayo kimsingi ndiyo bajeti yenyewe, sijaelewa ni kwanini wahusika wametunyima jedwali la jinsi pesa nzima itakavyotumika.
Kwa sisi tunaotegemea vyombo vya habari ukiniuliza Ofisi ya Rais, Makamu wake, Waziri Mkuu na wengine zimetengewa kiasi gani, utakuwa umeniua.
Kwangu naona ni kama hili limefichwa. Je, ni kwanini iwe hivyo ili iweje?
Natoa nukuu ya ‘figures’ nilizozidaka kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Zakia Hamdan Meghji.
“Kwa tafsiri hii kilimo kimetengewa asilimia 6.3 ya bajeti ya 2007/08”.
Ukiendelea chini yake kuna maneno haya.
“Kwa tafsiri hii pana maeneo yaliyopewa kipaumbele katika bajeti ya 2007/08 ni pamoja na: (1) Elimu, sh bilioni 1,086.1 (trilioni 1.086) sawa na asilimia 18 ya bajeti.
(2) Barabara, sh bilioni 777.2 sawa na asilimia 12.8 ya bajeti.
(3) Afya, sh bilioni 589.9 sawa na asilimia 10.0 ya bajeti.
(4) Kilimo, sh bilioni 379 sawa na asilimia 6.2 ya bajeti.
(5) Maji, sh bilioni 309.1 sawa na asilimia 5.1 ya bajeti.
Ukiangalia nukuu ya kwanza ni kwamba kilimo kimepewa asilimia 6.3. Ukija nukuu ya pili, kilimo hicho hicho kimepewa asilimia 6.2. Je, ni lipi ni sahihi kati ya haya mawili? Je, kilimo kimepewa asilimia 6.3 ya bajeti au 6.2?
Ukijumlisha pesa iliyotajwa hapo juu unapata kuwa ni jumla ya asilimia 52.1 ya bajeti yote.
Je, hii asilimia 47.1 italiwa vipi? Hapa ndipo jedwali lilihitajika. Na ni kwanini waziri ameamua kutaja matumizi ya anachokiita kipaumbele na kuacha matumizi ya ofisi nyingine? Je, anaficha nini au nalo hili atasema ni makosa?
Nijuavyo unapopanga bajeti lazima kitu cha kwanza uorodheshe kila kitu na baadaye ndipo uanze mchezo wa kugawa asilimia husika.
Je, huu ni usanii wa kutaka wananchi wasijue wakubwa wetu mabingwa wa ufujaji watapata kiasi gani?
Je, kama wananchi hawakujulishwa kuna usalama wa pesa hii? Je, kwa kuficha matumizi ya wizara nyingine si uchochoro mwingine wa kubinafsisha bajeti na kuifuja kama ilivyotokea kwenye mwaka uliopita ambapo serikali ilishutumiwa kufuja pesa nyingi?
Bahati mbaya kwa sasa huwezi kujua ni nini kilifanyika nyuma ya pazia! Maana ukiachia mbali kuwapangua kina Blandina Nyoni, CAG naye sijui kalishwa, maana ameishakuja na staili ya kujipiga mtama ili kuitetea serikali yake!
Inatia kinyaa wana taaluma wanapoanza kugeuzwa mabonzo na wanasiasa tena wababaishaji wa kawaida.
Nasema wababaishaji maana itakuwa ni jambo la hatari kwa daktari kutoa taarifa za kitaalamu kwa lugha ya mgonjwa. Huyu daktari naye atakuwa ni mgonjwa ingawa mgonjwa wake atabakia kuwa mgonjwa. Hatakuwa daktari.
Je, Meghji na wale waliokamua mapesa yetu kuandaa bajeti hii walisahau umuhimu wa kuja na hotuba yenye kila kitu au wamesimamiwa kufanya hivyo?
Mtu asiniletee jibu la wabunge watapewa kopi. Wabunge wanajadili pesa yetu siyo pesa yao wala ya wazazi wao ya urithi.
Tunapaswa kujua kwanza kabla ya hata hao wabunge maana wanatuwakilisha sisi. Ingekuwa ni wabunge kujua kusingekuwa na hata muda wa kutupotezea kula mawimbi ya radio na televisheni zetu bure.
Je, hapa tatizo ni mimi na makengeza yangu au ni Meghji au hata wakubwa wake?
Lakini ikumbukwe kuwa na mimi ni mwananchi mwenye kusukuma guruduma la maendeleo ya taifa hili kapuku lenye mzigo mzito na mchafu wa walafi wachache.
Kuna mtu mmoja mtundu alisema kuwa ukitaka kuwaibia Waswahili hasa Watanzania, andika ‘volume’ kubwa hata kama unaloeleza linataka kurasa mbili.
Jamaa huyu anasema Waswahili huwa ni wavivu wa kusoma. Hivyo ukificha kitu chako kwenye maandishi mengi hata kama utayaweka kwenye mashubaka yao ya vitabu hawatafichua.
Lakini usifanye kosa ukawafichia Waswahili kitu nje ya kitabu. Hata kama itakuwa ni maili moja kutoka walipo watapekenyua hadi watakipata.
Nakumbuka hata kwenye semina, warsha na makongamano. Wajanja wakitaka kutuibia huwa wanakuja na makabrasha makubwa.
Baya zaidi zinapokuwa zinajadiliwa hoja za maana, watu wao huanza kupitisha vinywaji, vyakula na posho.
Hapo ndipo utauona uovyo wa tabia hii ya kutopenda kusoma.
Utaona baba au mama zima linatokwa jasho huku likihamisha mawazo kwa mihemko kuelekea vilipo vilaji na vinywaji.
Kwa waliowahi kuhudhuria semina hizi kule Bagamoyo nadhani hata Ngurdoto wanajua hali inakuwaje.
Utakuta jitu zima linaficha bia hata uvunguni mwa meza likidhani ni za dezo kumbe limeuza mustakabali wake na vizazi vijavyo.
Leo watu wengi tunalaumu bajeti kwa kupiga kelele nyingi tu. Je, ni wangapi wamechukua muda kuisoma hatua hadi hatua, neno hadi neno, mstari hadi mstari?
Je. kama hatusomi bajeti tunayoambiwa na kuaminishwa ni yetu tena ya kutukomboa japo ni tusi la nguoni, tuna haki ya kulalama?
Na hali ni mbaya sana kule bungeni. Kuna ushahidi kibao tu wa wabunge kusinzia bungeni, wengine kutoroka na kuja wakati wa kugawa posho na upuuzi mwingine kama huu.
Kama wanavyofanya Bagamoyo, serikali imeishaandaa mtego wake. Usishangae mikataba na hati za nyongeza za maulaji ya wabunge zikapitishwa ili zisainiwe wakati wa kujadili bajeti ya wizara nyeti au zenye mazabe. Huu ndiyo usanii.
Huu ndiyo uoza na kupooza vinavyolisumbua taifa hili. Bahati mbaya ugonjwa huu umeanzia kwenye kichwa hadi miguu.
Nitaeleza. Kadiri wao wanavyotufanyia usanii kwenye kuhalalisha jinai zao, ndivyo nao wanafanyiwa usanii wakienda kuombaomba huku wanakojigonga na kujidhalilisha kama nilivyoelezea kwenye makala ya viongozi wa G8 na watwana wa Kiafrika.
Nitatoa mfano.
Leo mtu anakwambia kwa mfano, ziara ya Rais ilifana sana nchini Marekani kwa sababu aliongea na Mkurugenzi wa Soko la Hisa la New York.
Hili si dili. Kwani wewe na nchi yako mna hisa gani pale Wall Street? Au mtu anajisifu amepeana mkono na George W. Bush!
Kina Malik pale Irak wanakumbatiana naye, acha kupeana mikono. Waulize balaa alilowasababishia.
Nimalizie na bajeti. Meghji ametoa changamoto kwa kusema “it can be done play your part.”
Nami namrudishia changamoto: “How can I play my part whereas I have been forgotten? Which part am I to play if what is seen is nothing but abracadabra so to speak. Meghji nisaidie.