WANAFUNZI tisa kati ya 12 wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), waliofukuzwa chuoni hapo kwa madai ya kuchochea mgomo, wamerejeshwa.
Akizungumza na Tanzania Daima chuoni hapo jana, Rais wa Serikali ya wanafunzi (IFM-SO), Boniphace Baltazar, alisema kurejea kwa wanafunzi hao tisa kumetokana na agizo la Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, alilolitoa kwa uongozi huo juzi jioni.
Alisema baada ya agizo hilo, wanafunzi wote 12 waliitwa kwa simu, lakini cha kushangaza walipowasili chuoni hapo walitaarifiwa kuwa wanaotakiwa kurudi chuoni hapo ni wanafunzi tisa tu.
Alisema awali uongozi wa shule uliwafukuza wanafunzi watatu na baadaye Juni 15 uliwafukuza wanafunzi tisa na kufanya idadi ya wanafunzi waliofukuzwa kufikia 12, ambapo mwanafunzi mmoja kati yao (Salum Mwalimu), alipewa adhabu ya kusimamishwa shule kwa muda wa mwezi mmoja tofauti na wenzake.
“Jana tulituma ujumbe wa watu wawili Ignas John, na Milambo Milambo, ambao ni miongoni mwa wanafunzi tuliofukuzwa kwenda Dodoma kuonana na waziri mwenye dhamana na walifanikiwa, ilipofika jioni tulipigiwa simu na utawala na kutaarifiwa kuwa tulitakiwa kuwapo chuoni leo hii (jana).
“Baada ya kufika chuoni hapa leo tumekuta majina matatu hayapo katika orodha hiyo ambayo ni mimi, Ditrik Mwita, pamoja na Boniventure Makanga na hili ni tatizo jingine lililojitokeza,” alisema Baltazar.
Alisema wanafunzi hao tisa walioruhusiwa kurudi chuoni wataungana na wanafunzi wenzao wa chuo hicho na kufanya mitihani iliyobaki kwa kuwa baadhi yao walitakiwa kuanza mitihani jana na hivyo wamekosa mtihani mmoja.
“Mimi ni mmoja wa wale waliotakiwa kuanza mtihani leo lakini kwa kuwa wao ndio sababu ya kuukosa mtihani huo, nitaufanya baadaye kama watarekebisha hii orodha yao na sisi kuruhusiwa kujiunga na wenzetu, na Jumatatu tuanze mitihani,” alisema.
Uamuzi wa uongozi wa IFM kuwafukuza wanafunzi hao ulisababishwa na mvutano kati yao na wanafunzi hao baada ya kubatilisha sifa za wagombea wa nafasi ya urais katika serikali ya wanafunzi (IFM-SO) uliosababisha mgomo uliohusisha wanafunzi zaidi ya 600 Aprili 27, mwaka huu.