KATIKA hali ambayo haikutarajiwa, Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (CHADEMA), ameitaka serikali kupunguza mara moja kodi katika bia.
Ndesamburo alitoa utetezi wake huo kwa bidhaa hiyo wakati akichangia bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2007/08 iliyowasilishwa wiki iliyopita na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji.
Katika mchango wake, Ndesamburo alionyesha kusikitishwa na kitendo cha kodi ya bia kupanda kupitia bajeti ya mwaka 2007/08.
Mbunge huyo mkongwe na mfanyabiashara mzoefu, alitanabaisha kuwa kupanda kwa bei ya bia, kunaweza kusababisha wananchi waache kuinywa na kuhamia kwenye vilevi vingine ambavyo ni hatari kama vile gongo.
“Hivi kila mwaka mnaongeza bei kwenye bia tu hakuna vyanzo vingine vya mapato, mbona mnatuumiza jamani, au mnataka watoto wapate kwashakoo?” alihoji Ndesamburo.
Katika kauli iliyomaanisha jinsi watu wanavyothamini bia, Ndesamburo alisema ni vigumu kwa mtu kununua chakula cha mtoto au kulipa ada ya shule kabla hajatenga hela ya bia.
Aliitaka serikali kama ina nia ya watoto wasome, basi ipunguze kodi kwenye bia ili kuwawezesha wazazi kumudu gharama za vitu vingine.
“Mimi siwezi kuacha kunywa ka-bia kangu nimnunulie mtoto chakula, wote hapa tunakunywa bia jamani, tutaua watoto wetu na njaa, tupunguzieni,” aliomba
Ndesamburo.
Alisema bia isipoongezwa kodi wananchi wataongeza kasi ya kunywa na kuiingizia serikali mapato zaidi kuliko ikiongezwa bei maana wanywaji watakuwa wachache.
Wakati huo huo, Ndesamburo ameshauri serikali ifunge migodi ya madini mpaka hapo itakapopata uwezo wa kuiendesha badala ya kuwaachia wageni waiendeshe.
Ndesamburo alisema kuwa chini ya utaratibu wa sasa, migodi mingi inawanufaisha zaidi wageni kuliko wenyeji ambao ndio wenye rasilimali.
Alisema haoni faida ya sekta ya madini katika uchumi wa nchi zaidi ya upotevu wa rasilimali za nchi ambazo zingeweza kutumiwa na watoto wa baadaye kwa masilahi ya taifa.
Alisema bajeti ya mwaka 2007/08 haiwezi kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania kwa kutenga chini ya asilimia 10 ya bajeti kwa ajili ya sekta ya kilimo ambayo ndiyo inategemewa na wananchi wengi.
Alisema kiwango kilichotengwa kwa ajili ya kilimo hakitoshelezi mahitaji ya kilimo nchini na hakiwezi kuwaletea wananchi mapinduzi ya kilimo kwa haraka.
Aliulalamikia ukaguzi unaofanywa bandarini kwa wazalendo kuwa unadhalilisha utu wa mtu kwa kupekuliwa zaidi ya mara tano na watu tofauti.
Alisema hali hiyo inaonyesha Watanzania hawaaminiani, hali inayowatisha wageni kuja kufanya biashara zao Tanzania.
“Hivi sisi ni wezi kweli? Mnashindwa kuweka ukaguzi mmoja mpaka mtu akaguliwe na watu zaidi ya watano! Mnawatisha wawekezaji jamani,” alisema Ndesamburo.
Alisema Watanzania wanapaswa kuaminiana ili kuwashawishi wageni kuleta biashara zao na kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza ndani ya nchi.