JUMLA ya taasisi zisizokuwa za kiserikali (NGOs) za kimataifa 107 ziko nchini, zikiendesha shughuli zake mbalimbali.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, aliliambia Bunge jana mjini hapa kuwa, mashirika hayo yako kihalali nchini na yanatambuliwa na serikali kutokana na shughuli zake zinazofanywa.
Alisema taasisi hizo zinapoingia nchini, husajiliwa chini ya sheria ya NGOs namba 24/2002, ambayo husimamiwa na wizara yake.
Alisema mara baada ya kusajiliwa, taasisi hizo huruhusiwa kuendesha shughuli zao kuanzia ngazi ya taifa, mkoa hadi wilaya na idadi hiyo inahusisha zilizosajiliwa chini ya sheria ya NGOs namba 24 ya mwaka 2002, sheria ya vyama, sura 337, sheria ya udhamini sura 375 ya kampuni na sura 212 kama ilivyorekebishwa.
Alisema taasisi hizo zimetanda nchi nzima na zimekuwa zikiendesha shughuli zake katika mikoa na wilaya mbalimbali kulingana na uwezo wao wa kifedha.
Alisema serikali inaendelea kuhimiza na kuzielekeza NGOs za kimataifa kutanda na kuendelea kutoa shughuli zao nchi nzima.
Alisema serikali itahakikisha kwamba maeneo mengine ambayo hayana miradi inayoendeshwa na NGOs za kimataifa ikiwemo Mkoa wa Ruvuma yanafikika.
Alisema shughuli za mashirika hayo huendeshwa kwa dhana ya kujitolea hivyo si rahisi kuwalazimisha kisheria kutanda nchi nzima au kuwapangia kwa nguvu maeneo ya kufanyia kazi kwa kuwa huduma zao pia hutegemea rasilimali watu au fedha.
Alisema uzoefu umeonyesha kuwa wafadhili wa NGOs hao hawachangii sekta zote bali hujikita kwenye maeneo machache, hivyo taasisi nyingi hulamizika kuendesha shughuli, bali hujikita kwenye maeneo machache ambayo huona kuna faida wanazotaka.
Waziri Simba alitoa maelezo hayo wakati alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Devota Likokola (CCM), aliyetaka kujua idadi ya mashirika ya kimataifa yanayofanya kazi zake hapa nchini.