SERIKALI imekiri kuwa sheria nyingi zinazotungwa na Bunge, hazifiki kwa wakazi wa maeneo ya vijijini.
Hayo yalisemwa bungeni jana na naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, wakati akijibu swali la Mbunge wa Babati Vijijini, Paschal Nakei.
Chikawe alisema tatizo hilo limetokana na gharama kubwa, lakini serikali inafanya kila liwezekanalo kufikisha sheria hizo maeneo ya vijijini.
Alisema kutokana na hali hiyo, kumekuwa na wimbi kubwa la wananchi kuvunja sheria, hali ambayo inaonyesha wazi kuna mapungufu katika usambazaji wa elimu ya sheria.
Chikawe alisema kuna mapungufu katika sheria yenyewe au inawezekana yakawa ni matatizo ya wananchi wenyewe kutojua sheria zinazohusika.
Alisema wakati mwingine inawezekana mtu anafahamu vizuri sheria, lakini kwa makusudi anaamua kuivunja akijua adhabu yake ni ndogo.
Katika suala zima la kupambana na vitendo vya uhalifu, alisema kitu kinachotakiwa kuzingatiwa ni kuwafanya wananchi kuelewa umuhimu wa kuzitumia, kuziheshimu na kuzilinda sheria za nchi.
Alisema katika kutekeleza azma hiyo, serikali imekuwa ikiwaelimisha wananchi kupitia vyombo vya habari na katika warsha mbalimbali kuhusu sheria za nchi na umuhimu wake kwa jamii.
Chikawe alisema iwapo wananchi wataendelea kuelimishwa kuhusu umuhimu wa sheria, ni dhahiri kuwa vitendo vya uendeshaji mbaya wa magari ya daladala na lugha za matusi, vitisho vya hadharani, uwekaji wa ‘tinted glass’ kwenye magari na uendeshaji kasi wa magari unaosababisha ajali, vitatoweka mara moja.
Alisema Watanzania wengi wataanza kuogopa kuvunja sheria pale tu watakapokuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu sheria hizo, na pale usimamizi utakapokuwa umeimarishwa.
Alisema sheria, hasa za Jeshi la Polisi, ili ziweze kusimamiwa vizuri wakati wa utekelezaji wake, wananchi nao lazima wawe walinzi wa sheria hizo na wanapaswa kushiriki katika kukemea usimamizi wa sheria kwa kukemea vitendo vya uvunjaji wa sheria.