SERIKALI imesema jumla ya nyumba 1,000 za kuishi, zinahitajika kwa ajili ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kisiwani Zanzibar.
Maelezo hayo yalitolewa na Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Omar Yusuf Mzee, wakati akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Bububu, Masolwa Cosmas (CCM) aliyetaka kujua ni nyumba ngapi zinahitajika kwa askari wa JWTZ.
Naibu waziri huyo alikiri katika jibu lake kuwa, askari wa jeshi hilo wanakabiliwa na uhaba wa nyumba za kuishi, lakini serikali inafanya kila jitihada za kujenga nyumba hizo haraka.
Alisema wizara yake inaendelea na juhudi za kuhakikisha mikopo nafuu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za askari katika nchi nzima.
Alisema lengo kubwa la serikali ni kuhakikisha wanajeshi wote wanarejeshwa kwenye makambi na ili kufikia lengo hilo, nyumba nyingi zinahitajika.
Akizungumzia kambi ya Mwanyanya, Mzee alisema kuwa imepimwa na ina hatimiliki namba 831 iliyotolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Machi 17, 2003.
Awali, Waziri Mzee alisema lengo la serikali ni kuhakikisha maeneo yote ya jeshi yanapimwa na hatimaye kupewa hatimiliki.
Alisema serikali imeanza kuchukua hatua za kuzifanyia ukarabati pamoja na kujenga nyumba mpya za askari na maofisa katika kambi mbalimbali Tanzania Bara na Visiwani.
Alisema moja ya mipango mikubwa ya Wizara ya Ulinzi ni kuzungusha uzio kambi zote za Jeshi la Wananchi, ikiwemo kambi ya Mwanyanya baada ya hali ya fedha kuimarika.
Alisema kwa kipindi hiki, makao makuu ya jeshi imeagiza eneo la mzunguko wa kambi ya Mwanyanya iliyoko Wilaya ya Magharibi Zanzibar, ipandwe miti, hali itakayosaidia kulitambua eneo la kambi kwa haraka na kulinusuru kuvamiwa.
Kuhusu upatikanaji wa gari, alisema wizara yake imeshaandaa utaratibu wa kuagiza sehemu ya magari kwa ajili ya matumizi ya jeshi na mara baada ya kuwasili, na kwamba suala la usafiri kwa kambi ya Mwanyanya na kambi nyingine litaangaliwa kulingana na uzito wake.