logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumatano, 20 Juni 2007
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1


Tambwe ni Yuda msaliti wa Yesu
Mwandishi Wetu


NIMESOMA makala ya Tambwe Hiza kwenye gazeti la Juni 13. Pamoja na kutumia neno wengine na kunitaja kwenye waandishi anaowasoma, amegusia makala zangu.

Hivyo kwa msingi huo nimeamua walau nimpe dozi kiduchu.

Nimeshangaa kusoma aliyoandika, hasa kutokana na mambo makuu mawili.

Kwanza, ni kujisuta asijue anajisuta. Ukirejea historia yake na anayosema, hasa kwa kutoa darasa la subira na kuvumiliana.

Na pili, ni kuelezea alivyofarijika kuitwa msaliti kiasi cha kuuonea fahari uchafu huu!

Nasema uchafu huu kwa sababu mtu salata ni mtu anayemgeuka mtu kipenzi ambaye kwa walivyokuwa wakihusiana asingetegemea kama salata huyu angefanya hivyo.

Salata siku zote lazima awe mnafiki, mchumia tumbo, kidhabu, nyoka hata habithi. Hii si sifa nzuri hata Hiza angeivisha uyuda.

 Kwanza ashukuru uongozi wa Tanzania Daima kumpa nafasi ya kupatia mahali pa kujiuzia ingawa staili anayotumia siyo.

Yangekuwa magazeti ya chama chake mhariri angekuwa ameishajieleza na huo ungekuwa mwisho wake kutanua na hoja zake fupi fupi. 

Ukirejea kwenye hoja yake ya kwanza ya somo la uvumilivu, unashangaa. Kama anaona kuwa subira na uvimilivu ni vitu anavyotaka kutufundisha, basi asingekikimbia chama chake. Angevuta hiyo subira na kufuta tofauti zake na wana-CUF wenzake.

Bahati mbaya Mwalimu wetu wa subira uzalendo ulimshinda!

Kwa vile Hiza alifanikiwa kuwadanganya CCM wakamrejesha, nao wakamdanganya kwa kumpa kazi chafu isiyo rasmi, anadhani anaweza kuudanganya umma mzima.

Kwanini tofauti zake na viongozi wa CUF zianze baada ya kuukosa ubunge? Ina maana hata huko CCM akikosana na viongozi wake atatimka.

Huyu si mtu wa kuamini hata kidogo,. Hiza hajui kuwa karibu waganga tumbo wote waliorejea CCM, walifanya hivyo baada ya kuukosa ulaji wa Chimwaga?

Kama anabishia hili, basi awaulize wenzake ambao wengi wao wamefinywa kiasi cha kuwa kama ngumi.

 Na kama alikosana na viongozi kama anavyodai, kwanini hakuwapeleka kwa wanachama ambao ndio wenye chama chao?

Ukiachia mbali kutaka kujipa sifa, kilichomrudisha CCM Hiza si sera, kitu bali njaa na ile hali ya kutoelewana na viongozi wenzake wa CUF.

Sera hapa zinatoka wapi? Uboreshaji wa sera za CCM ulianza lini yakhe?  Kwa maneno rahisi Hiza ni ile aina ya wanasiasa wachumia tumbo,waganga njaa na wasasi wa ngawira (opportunists).

Kama angekuwa mwanamke ungemuita msungo, hata changudoa. Kama kito, basi ‘kakumba’ hata timbe.

Watoto wa mjini husema bomu.  Lakini kwa vile ni siasa, anabakia kuwa mfukuza riziki hata kwa kuikhalifu na kuikhalifisha  nafsiye ilmradi kiingie kitu tumboni.  Tukirejea kujisifia ujinga kwa kukubali usaliti ambao anataka kuubariki kwa kujilinganisha na Yuda, Hiza bado anapwaya kumshawishi mtu.

Yuda ‘alimsaliti’ Yesu ili wanaoamini ngano hizo waokoke. Hata hapa kuna utata. Maana Yuda alipewa vipande thelathini vya fedha. Je, yeye Hiza kapewa vingapi?

Hapa ndipo dhana nzima ya Ukristo, kama dini nyingine hutegemea imani badala ya uelewa.

Maana haya ni mambo ya kusadikika tu yenye kubeba mafumbo na mambo mengine ya kiruiya ruiya. Hayo tuyaache.   Je, Yuda - Hiza amemsaliti nani kwa ajili ya kuwakoa nani zaidi ya tumbo lake? Anachofanya Hiza ni ududushi wa kawaida.

Jana alikuwa akiishambulia CCM. Leo imempa mkate. Anaiabudia! Siku zinakwenda.  Kweli njaa hudhalilisha kuliko hata kaswende.  Kuna haja ya ndugu yetu huyu kuwa mkweli kuwa analazimika kuandika anayoandika. Kwani anatumia hoja za uongo, okotezi na nyepesi.

Kwanza, licha ya kudandia na kuchanganya mambo, anasema vitu ambavyo vinaleta shaka kwenye uwezo wake wa kupambanua mambo.

 Leo hii kwa mfano, mtu anamtetea Rais wa zamani, Benjamin Mkapa kwa kufanyia biashara Ikulu, eti kwa sababu hajapewa kipengele kilichovunjwa. Hii ni ajabu.

Hiza hajui katiba yetu inasema nchi hii ni ya kijamaa. Basi arejee miiko ya viongozi wa kijamaa atapata dawa yake.

 La kusikitisha na baya zaidi, anatoa mifano ya watu kama Jomo Kenyatta ambaye tofauti yake na mporaji wa kawaida haipo!

Isitoshe Kenyatta alikuwa anaendesha nchi ya kibepari uchwara kijambazi ambapo kuibiana ni jambo la kawaida.

Richard Hiza Tambwe. Aende Kenya aone athari za ujambazi mbuzi huu.

 Mbona hataji jinsi familia ya Kenyatta inavyochukuliwa kama kundi la wezi kule Kenya, ambapo mtoto wake Uhuru, angalau kuwapoza Wakenya, ameanza kurejesha baadhi ya ardhi iliyoporwa na baba yake? Watu wa Mombasa na pale jirani yake Hiza, Taveta, wanajua sana hili.

Hivi leo kweli mtu mwenye kujua mambo unaweza ukamlinganisha Rais yeyote na watu kama Hastings Kamuzu au Joseph Mobutu na Kenyatta, hata kama shida yako ni kujenga hoja na kupata utetezi? 

Anapiga hatua kwenye giza kwa kutoa mfano wa Bill Clinton! Ajabu! Clinton hakuwa anafanya biashara ya kimachinga na kwa siri tena akiwa Ikulu kama Mkapa.

Yeye na mkewe ni wanasheria kitaaluma. Hivyo walikuwa na biashara ya ofisi ya uwakili.

Hata hivyo kwa mujibu wa sheria za Marekani, alipoingia madarakani alijiuzulu uongozi wa kampuni yake yeye na mkewe.  Hata George W. Bush, ni mfanyabiashara mashuhuri wa mafuta. Lakini tangu aingie Ikulu haruhusiwi kusimamia biashara zake. Hata pesa itokanayo nayo haitumii.

 Hivyo utetezi wake wa uchafu wa Mkapa ni hafifu. Mkapa bingwa wa malumbano hawezi kutetewa na watu wasio na hoja kama Hiza hata Jakaya Kikwete akabakia nguli.

Amefinywa na kuwa mtu wa kutegemea hisani! Na kwanini Hiza aanze kumtetea Mkapa baada ya Rais, kwa sababu anazozijua kuanza kumtetea?

Anafanya hivyo ili iweje? Asikike. Ili iweje? Atupiwe riziki-masazo kutoka kwenye chama. Hivi jamani mbona njaa inatupeleka pabaya!

Nani hajui kuwa Mkapa analaumiwa hasa pale alipojiingiza kutetea miradi iliyoshukiwa na wananchi kama vile uuzaji wa NBC, uletaji wa Kampuni ya Net Group Solution, rada, ndege ya Rais, ukarabati wa Ikulu, NGO na mambo mengine.

Na ndiyo maana ameamua kunyamaa. Kwa sababu binadamu kaumbika na aibu. Ajabu Hiza huyu huyu alikuwa akimlaani Mkapa na CCM yake kwenye viriri wakati wa kuutafuta ubunge alioukosa akatimkia CCM.

Leo anamtetea! Huu si uanasiasa, bali ni uchumia tumbo wa kawaida tu.

Tukija kwenye hoja ya Katibu Mkuu wa CCM anayesema: “Makala nyingine ilikuwa inamshambulia Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu Makamba, eti kwa sababu kasema wanachama wote wa CCM wana haki ya kugombea bila kujali ni watoto wa nani, eti hilo nalo likawa hoja, akashambuliwa hadi kutaka kumvalisha viatu vya Mangula na kudai havimtoshi.”

Hii ni makala yangu iliyoonyesha shaka juu ya uwezo wa Makamba ambaye ni kweli anapwaya kwenye ukatibu mkuu.

Hiza muache mgosi ajisemee. Huna haja ya kujivika usemaji usiokuwa wa kiitifaki.

Makamba ni mtaalamu wa mipasho na mpayukaji, ni bingwa wa mipayuko. Tutajuana wenyewe. Na hilo Makamba analijua sana. Inshallah kama dozi haitoshi nitadurusu tena.

mpayukaji@yahoo.com


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2007 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Billicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570