HIZI si habari mpya kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Si habari mpya kwa sababu nitakachokiandika hapa si changu, bali ni chake yeye, na pengine kitakachomshangaza ni uamuzi wangu wa kujipendekeza na kuwa msemaji wake au mahali nilikoyatoa maneno haya mapesi nitakayoyaandika.
Hata hivyo, habari hizi zitakuwa mpya kwa mawaziri na naibu mawaziri, ambao wengi miongoni mwao wanayo matumaini makubwa kuwa, Kikwete ni mwenzi wao, mpiganaji pamoja nao, rafiki yao, mwanamtandao mwenzao, kaka yao, na rafiki yao pia. Nimehakikishiwa kuwa wanajidanganya.
Wiki iliyopita, nilizungumza na Watanzania wenzangu tunaoamini katika uzalendo kwa mtazamo wetu kuhusu simulizi nyingi tulizokuwa tukipewa kuhusu Kikwete ambaye zama hizo alikuwa rais mtarajiwa au kwa kimombo; ‘President in waiting.’
Miezi 18 baada ya jemedari huyo wa wanamtandao waliotujengea imani ya kuaminisha Watanzania, dhamira yao ya kumuandalia Kikwete ushindi wa kishindo imetimia.
Kama nilivyoandika wiki iliyopita, matarajio ya Watanzania hao walioaminishwa u-Kikwete hata wakajifunga vibwebwe vya kumuunga mkono kwa kishindo, leo hii yameanza kufifia.
Bajeti ya Waziri wa Fedha, Zakia Hamdan Meghji, aliyoitangaza katikati ya wiki iliyopita, ni ushahidi wa mwisho wa kukatisha tamaa wa Serikali ya Rais Kikwete.
Uamuzi wa serikali kuamua kutangaza bajeti ngumu inayolenga moja kwa moja kumkamua zaidi Mtanzania kwa kuongeza kodi kwa bidhaa za msingi, kama mafuta ya taa na petroli wakati huu watu wanapolia hali ngumu ya maisha, ni sababu kuu ya kuendelea kupungua kwa imani kwa serikali ya Kikwete.
Wasaidizi kadhaa wa Kikwete wa zama za kampeni kwa nyakati tofauti walipata kuandika kuhusu hatari aliyokuwa akikabiliana nayo kiongozi huyo wakati huu akiwa madarakani.
Siku za mwanzo za uongozi wake, mmoja wa wasaidizi hao wa Kikwete, ambaye pia ni mchambuzi wa habari, alipata kuandika kuhusu changamoto atakayokabiliana nayo mwanasiasa huyo wakati akiwa rais, na akaitaja kuwa ni matumaini makubwa waliyokuwa nayo Watanzania kwake.
Naamini Kikwete alipata kuelezwa kuhusu hilo, na pengine hata kabla ya kuambiwa jambo hilo, huenda hata yeye mwenyewe alilitambua, hasa kama alikuwa akiamini kuwa, asilimia 80 ya ushindi alioupata ulikuwa ushindi halali.
Hicho kilichosemwa na wasaidizi wake kweli ndicho kilichotokea. Na kwa bahati mbaya sana, matarajio hayo makubwa taratibu yalianza kuyeyuka na hatua zisipochukuliwa, kuna hatari yakatoweka kabisa.
Wiki iliyopita, nilitoa tahadhari na leo ninairudia tena. Serikali na hususan Kikwete, wanao wajibu wa kuhakikisha hilo la matumaini kutoweka kabisa halitokei.
Ili lisitokee hilo, Kikwete anao wajibu mmoja rahisi kabisa kimantiki na mgumu sana kimaamuzi na kimatendo. Anapaswa kuiangalia upya serikali yake kwa maana ya mawaziri wake, makatibu wakuu wa wizara, watendaji wakuu serikalini, wakuu wa mikoa na hata wale wa wilaya.
Katika hilo la kwanza la kuwaangalia watendaji wake, Kikwete anapaswa kufunga na kufungua macho. Wakati akifanya mapitio ya utendaji wa wasaidizi wake hao, anao wajibu pia wa kuziangalia upya wizara zake zote na kutafakari upya iwapo zinafaa zikaendelea kuachwa zikawa hivyo zilivyo.
Huu sasa ni wakati wa Kikwete kwa vitendo kuwathibitishia Watanzania kwamba urais wake hauna ubia na mtu mwingine yeyote, isipokuwa Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein, kiongozi ambaye kwangu anabakia kuwa mfano wa uadilifu na uongozi usio na makuu.
Kikwete anapaswa kutambua kwamba, baadhi yetu leo hii tumeanza kujiuliza iwapo yale maneno yaliyokuwa yakisemwa na wapinzani wake wakati wa mchakato wa kuusaka urais, yaliyoonekana kuwa ya utani zama zile, yalikuwa na chembe ya uhalisi.
Profesa Ibrahim Lipumba, wakati wa mikutano yake kadhaa ya kampeni, hususan kule Tabora na baadaye jijini Dar es Salaam, alipata kusema kwamba, iwapo Watanzania wangemchagua yeye (Lipumba) kuwa rais wa nne, basi alikuwa amepanga kumfanya Kikwete kuwa waziri atakayehusika na masuala ya michezo na maendeleo ya utamaduni.
Mimi nilikuwa mmoja wa Watanzania walioyapuuza maneno hayo ya Lipumba, kwani harakaharaka yalionekana kuwa ni ya dhihaka za kisiasa za nyakati za kampeni.
Miezi 18 tangu aingie madarakani, eneo pekee ambalo halina shaka hata kidogo kuwa Rais Kikwete amelifanya barabara, ni lile la michezo, na hususan soka.
Katika kipindi cha urais wake, ni kweli pia kwamba, Tanzania (sijui ni kwa sababu gani hasa) inaelekea kuanza kufanya vyema katika ulimwengu wa masuala ya ulimbwende.
Ni bahati kwamba, hatujamsikia bado Profesa Lipumba akikumbusha kauli yake hiyo, ambayo ingawa ilionekana kuwa kejeli mbaya wakati ule, akiikumbusha tena leo, inaweza ikageuka na kuwa hoja ya msingi.
Binafsi ninao mtazamo tofauti na huo. Ninapojaribu kuvivaa viatu vya Kikwete, japo kifikra, napata jibu moja tu ambalo naliona kuwa jibu jingine kwa rais wangu.
Anapaswa kujifunza kutoka kwa kocha wa Taifa Stars, Marcio Maximo ambaye wakati fulani baada ya Wasenegali kukidhalilisha kikosi chake kwa kukibamiza mabao manne bila ya malipo, alilazimika kukifanyia mabadiliko makubwa.
Uamuzi wake huo wa kupangua wachezaji, miongoni mwao wakiwamo wale wenye majina makubwa, ulipokewa kwa hisia tofauti na mashabiki wa soka na wataalam wengine wa mchezo huo.
Maximo hakuwasikiliza wapinzani wake hao, ambao baadhi yao waliungwa mkono na vyombo mbalimbali vya habari kwa kiwango cha kufikia hatua ya kuitaka serikali iangalie upya uwezekano wa kumpata kocha mwingine.
Leo hii kikosi kipya cha Stars kilichofinyangwa upya na Mbazili huyo, kimefufua matumaini ambayo yalishaanza kupotea baada ya kipigo cha Senegal.
Wachezaji wapya walioingizwa, pamoja na kwamba hawakupata bahati ya kukanyaga Brazil wakati timu ilipokwenda huko kwa mazoezi, wamekuwa chachu kuu ya ushindi na hata wale waliokuwapo tangu awali, wanaonyesha dhahiri kujizatiti zaidi kisaikolojia na kimaamuzi.
Mapokezi makubwa ambayo hayajapata kutokea yakihusisha timu hiyo, yameiwezesha serikali ya Rais Kikwete iliyo katikati ya shinikizo la bajeti ngumu kupata fursa ya kupumua vyema.
Kwa maneno mepesi, alichofanya Maximo ndicho anachopaswa kukitenda Kikwete leo hii. Ndani ya Bunge na nje ya baraza lake la mawaziri, kuna wanasiasa shupavu ambao pamoja na ukweli kuwa hawakwenda Ngurdoto kuhudhuria semina elekezi iliyogharimu shilingi bilioni 1.6, wanaweza kukidhi matakwa ya kaulimbiu ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya.
Kwa kuwa Maximo alilazimika kukisahau kipimo cha urefu wa baadhi ya wachezaji aliowaona awali kuwa wanafaa, akaweka nidhamu kuwa ajenda muhimu ya pili na akakataa kuikubali safari ya Brazil kuwa ndiyo kipimo cha mafanikio ya kikosi chake, Kikwete naye anao wajibu wa kujifunza hilo.
Kikwete anapaswa kutambua na kukubali kuwa, hadi hivi sasa, ‘Wasenegali’ (umaskini, ujinga, maradhi, ukosefu wa ajira, rushwa, wizi wa mali ya umma, uongozi mbovu na mambo yanayofanana na hayo) wamekibwaga kikosi chake (serikali yake) mabao manne kwa bila.
Kama hiyo haitoshi, Kikwete anatakiwa kukubali kuwa safari ya kuipeleka timu yake Brazil (semina elekezi za Ngurdoto, ziara za kutembelea wizara na idara za serikali na hatua nyingine za namna hiyo) zimegonga mwamba, na anao wajibu wa kuanza upya kwa kuunda serikali yake.
Kikwete hana njia, isipokuwa kulivunja baraza lake la mawaziri. Anapaswa kuangalia anakokwenda na linakokwenda taifa analoliongoza badala ya kugeuka nyuma na kuangalia alikotoka.
Kwa Rais Kikwete huu si wakati wa kugeuka nyuma na kuwaangalia wanamtandao wachache walioamua kutumia jina lake, karisma (charisma) yake na historia yake kupata madaraka.
Kama alivyopata kusema yeye mwenyewe wakati fulani, mtandao wake hivi sasa ni chama chake na wananchi wake ambao wote tunamwangalia yeye kama rais wetu na kiongozi wetu na wala si chaguo la Wanamtandao.
Nimelazimika kuandika waraka huu leo, nikitiwa moyo baada ya kupata simulizi jipya kuhusu Kikwete, simulizi ambalo ingawa kimantiki linafanana na lile la zama za kampeni, kidogo linaweza likawa na maana nzito kuliko lile la awali.
Simulizi lenyewe na ambalo lina kila dalili za ukweli linasema, tena kwa uhakika kuwa, Rais Kikwete katika siku moja isiyo na jina atafanya mabadiliko makubwa ya mawaziri, akizingatia uwajibikaji na utendaji wa kazi wa waziri mmoja mmoja.
Iwapo kweli Kikwete atafanya hilo, huku akisikiliza kilio cha wananchi walioanza kupoteza imani kwa serikali yake, kwa hakika kabisa atavuna mafanikio mema ambayo leo hii kocha Maximo na vijana wake wanajivunia.
Matokeo ya maamuzi hayo ambayo Kikwete atayafanya, yatamfanya akosane na kundi dogo la marafiki wasiomtakia mema yeye na wanaoliombea mabaya taifa hili, kwa sababu tu ya kuweka maslahi ya matumbo yao kabla ya utaifa wao.
Kwa upande mwingine, mabadiliko hayo ambayo baadhi tunayatarajia, yatamwezesha hatimaye kujenga msingi imara wa kufanikisha kaulimbiu zake zote zinazohitimishwa na dhamira ya kufanikisha maisha bora kwa kila Mtanzania.
Baadhi yetu tunaamini kuwa, iwapo Kikwete ataendeleza hulka ya miaka nenda, miaka rudi ya wana CCM kulindana chini ya mwavuli wa ‘huyu ni mwenzetu’ basi iko siku ataporomoka yeye na serikali yake yote. Huko ndiko tuendako.