na Mwandishi Wetu, Dodoma
MBUNGE wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela (CCM), ameitahadharisha serikali kuwa mpango wake mpya ilioubuni wa kupitisha mizigo na bidhaa za wawekezaji bandarini bila ya kukaguliwa, ni hatari kwa taifa.
Mbunge huyo alisema jana kuwa, mpango wa serikali wa kuwaruhusu wawekezaji waliosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), kupitisha mizigo na bidhaa zao bila ukaguzi, utaisababishia nchi matatizo makubwa.
Malecela alitoa tahadhari hiyo jana, wakati akichangia hotuba ya bajeti ya mwaka 2007/08 iliyowasilishwa bungeni Alhamisi iliyopita na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji.
Msimamo huo wa Malecela, unatokana na mpango uliotangazwa na Meghji kuwa, kuanzia mwaka ujao wa fedha, waagizaji wa magari, wawekezaji waliosajiliwa na TIC na walipa kodi wenye rekodi nzuri katika Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), wataweza kupitisha bidhaa zao bila urasimu zinapoingia bandarini.
Waziri Meghji, katika maelezo yake alisema kuwa, utaratibu huo mpya unalenga kupunguza kero ya ucheleweshaji wa mizigo bandarini.
Kwa mujibu wa Meghji, mbali ya kupitisha bidhaa na mizigo kwa haraka, hatua nyingine iliyochukuliwa kukabili tatizo hilo, ni kupunguza kiwango cha bidhaa kinachopitishwa kwenye ‘red channels’ (eneo la uangalizi mkali) kutoka asilimia 80 ya awali.
Aidha, chini ya utaratibu huo mpya, asilimia 40 ya bidhaa zitapitishwa kwenye milango ya kijani (ukaguzi wa kawaida), na kuondoshwa bandarini moja kwa moja.
Sambamba na hilo, asilimia 40 ya bidhaa nyingine zitafanyiwa ukaguzi wa kawaida bila kufanyiwa upekuzi, zikifuatiwa na ukaguzi wa kina baada ya kuondolewa bandarini.
Chini ya utaratibu huo mpya, ni asilimia 20 tu ya bidhaa ndizo zitakazofanyiwa upekuzi kabla ya kuondolewa bandarini.
Hatua ya tatu itakayochukuliwa na TRA kukabili tatizo hili, inahusu bidhaa zinazoingizwa na wawekezaji waliosajiliwa na TIC.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti, Meghji alibainisha kuwa, bidhaa hizo zitapitishwa moja kwa moja katika milango ya kijani, ambapo asilimia 25 ya bidhaa hizo zitafanyiwa ukaguzi wa kawaida, ukifuatiwa na ukaguzi wa kina baada ya kuondolewa bandarini.
Alisema magari mapya, na yale yaliyotumika kwa kipindi kisichozidi miaka mitano hayatapitishwa kwenye ‘red channel’ kama ilivyokuwa awali.
Aidha, Meghji alisema kuwa, bidhaa maalum zinazohitaji vibali kutoka idara mbalimbali za serikali, zitafanyiwa ukaguzi wa nyaraka pekee badala ya upekuzi kamili wa bidhaa zenyewe, ili kuharakisha uondoshwaji bandarini wa bidhaa hizo.
Malecela kwa upande wake aliupinga mpango huo wa serikali, wa kutoa upendeleo kwa baadhi ya wafanyabishara na kusema kuwa watu wasio waaminifu, watautumia mwanya huo kuingiza bidhaa haramu.
Mbali ya kusababisha hatari, Malecela alisema kuwa mpango huo utalisababishia taifa hasara kwa sababu mara zote, wafanyabishara wanalenga katika kujipatia faida.
“Nasema haiwezekani! Hivi ni kigezo gani mlitumia kuamua kwamba wafanyabiashara hao wapitishe bidhaa bila kukaguliwa na mnawaamini nini kwamba wapo safi?” alihoji.
Alisema iwapo utaratibu huo utaachwa ufanye kazi, nchi itakwisha, kwani huo utakuwa mwanya wa wafanyabiashara kupitisha bidhaa haramu kama vile dawa za kulevya.
“Utaratibu huu utawanufaisha wafanyabishara kuliko serikali… hata sasa hivi ambako kuna ukaguzi, mfanyabishara anasema kuwa ameagiza used computers, sijui used refrigerators, lakini ukifungua unakuta vitu vingine,” alisema.
Alibainisha kuwa, TRA ni mashahidi wa hilo, kwani wamekuwa wakikamata makontena ambayo vielelezo vinasema ni vifaa vilivyotumika, lakini ukifungua ndani ni bidhaa nyingine mpya na tofauti na zile zilizoorodheshwa kwenye nyaraka.
Alisema kuwa, mfanyabiashara yeyote, yupo kwa ajili ya kupata faida zaidi na si kupata hasara, maana na yeye ni mfanyabiashara na analifahamu jambo hilo.
Akizungumzia mikataba, Malecela aliwachachamalia watendaji wa serikali kwa kutia saini mikataba bila kuweka mbele uzalendo, hatua ambayo imekuwa ikisababisha matatizo mengi.
Alisema Tanzania si nchi masikini kama inavyodhaniwa, lakini umasikini unaletwa na watendaji wa serikali ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao kwa kutia saini mikataba inayomaliza nchi.
“Watendaji wa serikali wanaotia saini mikataba, ndiyo wanachangia kuleta umasikini, Rais Jakaya Kikwete aliwahi kuzungumzia suala la mikataba mibovu, na sisi tunapozungumzia mikataba mibovu, tunaomba wenzetu serikalini msituchukie,” alisema.
Alitoa mfano wa mkataba wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA), kwamba waliotia saini mkataba huo hawakuwa na moyo wa uzalendo wala hawakuwa wanamuogopa Mungu, kwani walijua wanaiingiza nchi matatizoni.
Alisema anavyo vielelezo vya hasara ya kila mwaka kutokana na mkataba huo, na kwamba Shirika la Ndege la Kenya (KQ) lilipoungana na Shirika la Ndege la Uholanzi (KLM), waliamua kutumia namba zote za tiketi, na hiyo ni faida kwa mashirika hayo
ya ndege.
“Tulitia saini mkataba bila uzalendo… kila anayetia saini mkataba amuweke Mungu mbele, serikali msichukie tukisema mikataba, kila mtu atimize wajibu wake,” alisisitiza.
Alibainisha kuwa, watendaji wa Rais Kikwete aliowaweka madarakani, ndio wanaomlaza macho rais kwa kutotimiza wajibu wao na kuifanya Tanzania iendelee kuonekana maskini wakati sivyo ilivyo.
Naye Mbunge wa Viti Maalum, Kidawa Hamid Salehe, akichangia mjadala wa bajeti, alisema kuwa serikali iangalie uwezekano wa kuondoa ushuru kwenye mafuta ya taa na kwamba sh nne ambazo zimeongezwa kwenye mafuta ya taa zipelekwe kwenye mambo ya
anasa kama vile Cassino na vileo.
Alisema pia mafuta mazito yaongezwe kodi na alishauri kwamba fedha zilizoongezwa kwenye mafuta ya taa, zinaweza zikapatikana kwenye mishahara ya watu wenye mishahara mikubwa kwa kuongezea kodi ya P.A.Y.E.
Kidawa alisema kuwa, pamoja na bajeti ya serikali kuwa nzuri, bado nidhamu katika matumizi inapaswa kuzingatiwa ili wananchi waweze kunufaika nayo kwa kuona matunda waliyoyatarajia.
Naye Mbunge wa Magu Mjini, Dk. Festus Limbu (CCM), aliisifu bajeti hiyo kwamba imelenga kukuza
uchumi wa nchi, lakini aliiomba serikali kuangalia upya mapendekezo yake ya magari yenye cc 2000, ambapo alipendekeza kuwa kiwango cha sh 80,000 kianzie cc 1500 hadi cc 2000, kwa watu wengi wenye kipato cha chini ndiyo wanatumia magari hayo.
Alisema serikali itenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara na si maamuzi yaishie kwenye makabrasha.
Dk Limbu, ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha, aliiomba serikali itowe ruzuku ya mbegu na dawa kwa zao la pamba linalolimwa zaidi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Wakati huo huo, Mbunge wa Iramba Mashariki, Mgana Msindai (CCM), ameitaka serikali kueleza mikakati iliyoweka katika bajeti ya awamu hii ili kuhakikisha mikoa iliyopo chini ya pato la taifa inalingana na mikoa mingine.
Alisema mikoa hiyo si maskini kama inavyodhaniwa tatizo ni kutokuwepo kwa soko zuri la bidhaa zinazozalishwa katika mikoa hiyo.
Msindai, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, aliishauri serikali kuweka vipaumbele katika mikoa hiyo kwa kuitafutia soko la uhakika la mazao wanayozalisha.
Aidha, aliilalamikia serikali kwa kutougawa Mkoa wa Singida tangu uhuru upatikane hali inayosababisha makao makuu na wilaya kuwa mbali na wananchi walio wengi ambao wanaishi katika maeneo ya vijijini.
Alisema mwalimu anatumia siku tano kila mwezi kwa ajili ya kufuatilia mshahara na kuacha kazi ya kufundisha wakati wastaafu wanatumia fedha nyingi kufuata mafao yao, ambazo zinalingana na fedha wanayolipwa.