na Ansbert Ngurumo
NIMEWAHI kusikia na kuona baadhi ya watu wanaokunywa pombe nyingi na kulewa kupita kiasi kwa kisingizio kwamba hiyo ni mbinu ya kuondoa matatizo.
Matatizo hayapungui wala hayaondoki. Kinachotokea ni kwamba wanapokuwa wamelewa ‘njwi’ wanayasahau kwa muda. Akili zao zinakuwa katika hali ya kudanganyika na kudhoofika.
Na mara nyingi, unywaji wa aina hii hukuza na kuongeza matatizo badala ya kuyapunguza au kuyaondoa.
Rafiki zangu wawili hawakubaliani na ‘ujinga’ huu. Mmoja kati ya hawa ninaowazungumzia, ana kawaida ya kunywa sana pale anapokuwa anataka kufurahia jambo fulani jema maishani mwake.
Anakunywa kuchangamka kwa sababu roho yake ina furaha; imechangamka.
Mwingine amejiwekea utaratibu kwamba anapokuwa na matatizo makubwa, ama hanywi kitu, au anakunya maji au kinywaji kingine chepesi (laini) ili aweze kutafakari vema namna ya kukabiliana na matatizo yaliyomsibu.
Ulevi hauondoi matatizo. Unadhoofisha nguvu ya akili kufikiri na kutafakari. Ulevi unaposababishwa na matatizo, huongeza nguvu na wigo wa matatizo kuliko ulevi wa kawaida, ambao pia hasara zake zinafahamika vema.
Nasikitika kwamba serikali yetu imeamua “kulewa ili kuondoa matatizo yanayowakabili wananchi wake.”
Katika tukio la hivi karibuni, ni juzi tu ilipoamua kuathiri mwenendo wa mjadala wa bajeti ya bungeni Dodoma kwa kisingizo cha kuipongeza timu ya soka ya taifa (Taifa Stars) kwa ushindi dhidi ya timu ya taifa ya Burkina Faso.
Iliamua kuwapangia nafasi ya kuwapongeza “mashujaa” katika sehemu ya muda ambao ulipangwa kwa ajili ya wapinzani kuwasilisha bajeti mbadala, ambayo ilikuwa inakosoa bajeti ya serikali na kuweka mapendekezo mbadala.
Haikutokea hivi hivi. Inaeleweka kuwa timu hiyo haikuwa imepanga kufika Dodoma, juzi. Ilikuwa imepangiwa kulakiwa kwa kishindo Dar es Salaam ikitokea Burkina Faso kupitia Mwanza.
Viongozi wa serikali wakapata wazo. Baada ya kuwa wamesikia malalamiko ya wananchi kuhudu bajeti ya serikali, na baada ya uongozi wa serikali bungeni kuwaita na kuwapa somo wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na waandishi na baadhi ya wahariri Dodoma, ulisukwa mkakati wa kupunguza makali ya wapinzani, na hasa kuzuia hoja zao zisitangazwe kama za serikali.
Stars ikawa kimbilio lililojitokeza kwa bahati. Ikabidi serikali ilazimishe waende Dodoma ghafla, wagawane muda na wapinzani, sherehe na shamrashamra zifunike changamoto na hoja za bajeti; wananchi wafunikwe na ushindi wa Stars na tambo za ilani ya CCM!
Watawala wetu walijua wananchi wanakerwa na bajeti, lakini ilijua pia kuwa furaha ya ushindi wa Stars ni dawa ya adha za Watanzania na ni jibu kwa hoja za wapinzani.
Wakatumia sanaa kufunika mjadala wa bajeti bungeni, masuala nyeti ya utawala na uongozi wa nchi.
Huu ndio ulevi wa muda ambao hauondoi shida. Tutakapozinduka tutazikuta pale pale.
Hekima ya viongozi wetu haikuwaruhusu watenganishe matukio haya. Umakini na umahiri wao umeonekana katika kupuuza na kukimbia changamoto, na kujenga mazingira ya kuzifunika kwa mbwembwe za ushindi wa Stars.
Naomba nieleweke vema. Ushindi wa Stars ni fahari yetu sote. Nami ni shabiki wa soka. Zaidi ya hayo, nafurahia ushindi wa nchi yangu. Naushangilia kama wananchi wengine, lakini si kipaumbele mbele ya mjadala wa bajeti.
Natambua kuwa soka ni jambo pekee ambalo Rais Jakaya Kikwete amelivalia njuga. Mashabiki wake wanasema amekuza ‘michezo.’ Ndiyo! Soka ni mchezo, lakini michezo si soka.
Michezo ni zaidi ya soka. Tukumbuke pia kwamba maendeleo ya soka hayaishii kwenye timu ya taifa.
Na hayatakuwapo kama hakuna maandalizi ya msingi kitaifa na bila mkakati uliozama ndani ya sera makini za kukuza soka katika miaka mingi ijayo. Mpango huo hatuna.
Kwa hiyo, tukiwa wakweli, tutasema kwamba Rais Kikwete amefanikiwa kuipa hamasa timu yetu ya taifa ya soka. Timu nyingine za soka ziko hoi. Michezo mingine, hata katika ngazi ya kitaifa, iko hoi.
Tumpe sifa yake kwa timu ya taifa ya soka, si kwa kukuza michezo. Huo ndio ukweli ambao hauwezi kutupeleka jehanamu.
Wakati huo huo, ni vema tujue kwamba timu yetu haijatwaa kombe, wala haijaingia fainali. Imesonga mbele.
Nasema hivi, inastahili pongezi, michango na maandalizi makubwa ili ipate ufanisi zaidi katika mechi zijazo.
Kitu ambacho haistahili kupewa ni umuhimu unaofunika mjadala wa bajeti ya serikali, ambayo inagusa maisha ya kila Mtanzania, inaboreshwa katika kuijadili, ili kupunguza makali yake na kuisaidia serikali kutuhudumia vema.
Nimeisoma bajeti mbadala ya wapinzani. Si bajeti ya kupuuzwa na kufunikwa na shamrashamra za soka.
Nimeona mengi ambayo serikali ilipaswa kuyapa kipaumbele na hata kuyabeba yalivyo na kuyatekeleza.
Ni bajeti makini, ya kizalendo, ambayo imejikita katika ubunifu wa njia mbadala za kuongeza pato la serikali na kuwapunguzia wananchi kero zilizoongezwa na bajeti ya serikali.
Wapinzani wameonyesha kwamba serikali ikiwa na viongozi na watendaji makini, inaweza kuachana na bajeti za bandua-bandika.
Viongozi makini wangeitumia kama fursa ya kujifunza kwa washindani wao na hata kuweka mkakati wa kuwapiku kwa kutumia hoja zao.
Wenzetu hawataki kusikiliza, hawataki kujifunza, bali kufunika mema ya wapinzani wao.
Sijui kwa nini wanapenda kukimbia midahalo, na kuchangamkia vitu vyepesi katika urembo, muziki na mpira.
Sijui kwa nini wanatamani kujenga taifa la ‘chereko,’ propaganda za kisiasa, udaku na soga za vijiweni, huku wakipuuza mambo yanayoweka misingi ya taifa. Sijaelewa kwa nini hawashtuki kwamba wananchi wamechoka tabia yao ya kupenda sifa, hata zinazowaponza.
Hebu tazama hata baadhi ya wizara ‘maskini’ zinazolialia kwa kunyimwa fungu la maana, ambazo zimetangaza kutokuwa na miradi mipya kwa sababu ya ukosefu wa pesa, nazo zinajitokeza kushindana kuandikwa magazetini kwa kutoa michango mikubwa ya dharura kwa timu ya taifa, na hivyo kuhatarisha utekelezaji wa miradi michache kadhaa iliyokwishapangwa.
Viongozi wetu wajue kwamba, si wao wa kwanza kupenda sifa. Miongoni mwa waliowatangulia katika hilo ni Rais wa kwanza wa Ghana, hayati Kwame Nkrumah.
Kwa kupenda utukufu binafsi na kupuuza umaskini wa nchi yake, alianzisha mradi mkubwa sana wa gharama za kutisha kujenga kile alichokiita Job 600, ukumbi mkubwa wa mikutano kwa ajili ya viongozi wenzake wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1965, ambao alikwishajitolea kuwa ‘kiongozi wao’.
Inasemekana kuwa gharama ya ukumbi huo ilikuwa pauni milioni 10 (kama sh 25,000,000,000), wakati huo uchumi wa nchi yake ukiwa unadidimia, viwanda havina bidhaa wala mitaji, maduka hayana bidhaa muhimu, wananchi wanakabiliwa na njaa kali nchi nzima, hospitali hazina dawa, huku mashirika ya serikali (umma) yanafilisika.
Kilichotawala dhamira yake ni fahari itakayotokana na jengo kubwa lisilo na mfano barani Afrika, kama vile serikali yetu inavyojivunia ndege ya rais yenye fahari ambazo hata wale wanaotupatia misaada na mikopo hawana.
Kwa mujibu wa mwanahistoria, mwandishi wa habari na mtunzi wa vitabu, Martin Meredith, jengo hilo kubwa lilikuwa na vyumba 60 vya fahari inayostahili chumba anamoweza kulala rais wa nchi; ukumbi mkubwa unaoweza kuwatosha wageni 2,000 kwa wakati mmoja wakiwa wameketi, chemchemi za maji zinazoendeshwa na ‘jeti’ 72, na mbwembwe nyingi za kuunakshi ukumbi na kuuongezea fahari.
Ulijengwa ukakamilika, lakini azima haikutimia. Haukuweza kuwa makao makuu ya Umoja wa Afrika.
Inasemekana hata viongozi wengi waliotarajiwa kuhudhuria katika mkutano waligomea mwaliko wa Nkrumah, wengine wakatuma maofisa wadogo. Mradi ukafa.
Fedha zikateketea katika kuridhisha sifa binafsi za Nkrumah, huku vyombo vya habari vya Ghana vikiimba sifa kemkem za ukumbi huo na utukufu wa kiongozi waliyebuni na kusimamia mradi huo.
Licha ya sifa hizo, mradi huo umebaki kuwa kituko cha kihistoria cha Nkrumah! Ndiyo gharama ya kupuuza mambo ya msingi na kuhangaikia sifa za leo bila kujenga misingi ya taifa kwa miaka mingi ijayo.
Tanzania hatuko mbali na huko alikokuwa Nkrumah. Rafiki yangu mmoja ameniambia kuwa “ukiona mtu asiyestahili hata kuosha viatu ndiye anakuwa mshona viatu, ujue tumekwisha.”
Sawa, serikali ihamasishe maendeleo ya soka na michezo mingine. Wananchi, wakiwamo viongozi wetu, tushangailie ushindi wa ‘mashujaa’ wetu katika mechi ya Jumamosi iliyopita. Wachezaji wapewe heshima na zawadi bungeni.
Yote haya ni mambo mema kama yanafanywa kwa utaratibu unaoonyesha vipaumbele; kama yanatenganishwa na masuala ya msingi, ya uhai kwa taifa.
Ushindi wa Stars ni mzuri kwetu kama viongozi wetu hawautumii kama ulevi wa kukwepea matatizo ya wananchi na makali ya bajeti.
Ni mzuri kama viongozi wetu hawautumii kufunika ushauri mzuri kutoka kwa wapinzani.
Wanafanya makosa pale wanapodhani kwamba hatuelewei ‘janja’ yao, na wanapotaka tukubali ulevi huo sasa kuficha udhaifu wao.
+447828696142
ansbertn@yahoo.com
www.ngurumo.blogspot.com