DIWANI wa Kata ya Usanda kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Abeid Ndaji, amesimamishwa uongozi kwa tuhuma za kukiuka kanuni za uongozi baada ya tume iliyoundwa kuchunguza tuhuma hizo kubaini kuwa alitafuna michango ya ujenzi wa shule za sekondari.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Mussa Homera alisema kamati ya siasa ya chama wilayani huko katika kikao chake cha Januari 24 mwaka huu ilimsimamisha uongozi diwani huyo na kumwamuru arejeshe kiasi cha fedha alizokula kwenye ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo.
Akifafanua, Homera alisema katika ziara aliyoifanya mwishoni mwa mwaka jana katika Jimbo la Solwa, Mbunge wa jimbo hilo, Salim Ahmed, alilalamikiwa na wananchi kuhusu kuzorota kwa kazi za ujenzi wa shule za sekondari katika kata hiyo baada ya wananchi kugoma kuendelea kuchanga kwa madai kuwa michango yao inaliwa na viongozi.
Kufuatia hali hiyo, mbunge huyo aliziomba kamati zote za ujenzi wa shule za sekondari katika jimbo hilo, kuwasomea wananchi taaarifa za mapato na matumizi na akaivunja kamati ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Usanda na kuunda tume maalumu kuchunguza tuhuma zinazomkabili diwani huyo.
Kamati hiyo ilibaini kasoro kadhaa na upotevu wa pesa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga akapeleka wakaguzi wa mahesabu, ambao nao walibaini upotevu wa kiasi cha sh 1,348,167 zilizochangwa na wananchi wa kata hiyo kwa ajili ya ujenzi wa sekondari ambazo inadaiwa Diwani Ndaji anahusika na upotevu huo.
Inadaiwa kuwa kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika kata hiyo umezorota, kutokana na mgomo wa wananchi kugoma kuendelea kuchangia ujenzi baada ya pesa walizochanga awali kuliwa na kiongozi wao na kutokusomewa taarifa za mapato na matumizi.
Homera alisema iwapo diwani huyo hatalipa kiasi cha pesa alichochukua katika muda wa siku 14, suala hilo litafikishwa kwa katibu wa CCM wa mkoa, ambako ndiko kwenye vikao vyenye maamuzi ya mwisho yatakayoamua hatima ya diwani huyo, ikiwa ni kutengua maamuzi ya kamati ya siasa ya wilaya au kumnyang’anya kadi ya uanachama diwani huyo.