logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumapili, 27 Januari 2008
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
sp.l_icon sp.r_icon
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1


Nikikutana na Spika Sitta!
Charles Mullinda


JUMANNE, Januari 29, mwaka huu, kikao cha kumi cha Bunge la Jamhuri kinaanza mjini Dodoma chini ya Spika Samuel Sitta. Nimepanga kusafiri kwenda huko nikakutane naye ‘mwishimiwa’ Sitta nizungumze naye machache.

Baada ya kukutana naye, kitu cha kwanza ni kuamkiana naye, huku uso wangu ukiwa umepambwa na tabasamu lenye bashasha ya hali ya juu. Wengi wa wanasiasa wa Tanzania wanapenda kuchekacheka wanapokutana na wapiga kura wao, na kwa sababu Spika Sitta ni mwanasiasa, basi nitamsabahi kwa staili hiyo.

Nimepanga hivyo kumsabahi kwa kuchekacheka ili tu nimlainishe, hata kama atakuwa na mipango yake mingine aiahirishe kwa muda, anisikilize.

Kisha, nitampongeza kwa kazi nzuri anayoifanya bungeni. Nitamsifia kwa mafanikio aliyoyapata ya kuweza kuenenda katika kaulimbiu yake ya kuliongoza bunge kwa Standard and Speed.

Sitamficha. Nitamweleza jinsi wabunge wa CCM wanavyomsifia kwa kuliongoza Bunge kwa jinsi walivyotarajia, pia nitatumia fursa hiyo kumweleza namna wapinzani wanavyolalama kwa kuminywa na kutishwa, wanapokuwa wakichangia hoja za msingi ndani ya ‘jumba’ hilo linalotumika kutunga sheria za nchi yetu kiranja mkuu akiwa yeye mwishimiwa Sitta.

Katika hili la wabunge wa upinzani kupiga yowe kuhusu staili yake ya kuongoza vikao vya Bunge, nitampongoza kwa kumshika mkono kwa sababu anaonekana kulinda maslahi ya chama zaidi kuliko taifa.

Sitampa nafasi ya kujibu pongezi zangu kwa sababu nafahamu akipata nafasi hiyo, anaweza kubadili mwelekeo wa mazungumzo yetu. Nitazungumza haraka haraka kwa kuunganisha maneno, huku nikiwa nimeung’ang’ania mkono wake, ‘nikuitingishatingisha’ kwa kumpongeza.

Najua hatachoka kwa sababu hatujaonana kwa siku nyingi, ‘tumemisiana’ kwa miezi zaidi ya sita sasa.

Aidha, nitamkumbusha mbali, miaka takriban miwili iliyopita, wakati wa semina ya kwanza ya wabunge iliyofanyikia kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, wabunge kadhaa walikoeleza kile kilichowafanya wagombee wabunge, jinsi walivyojipanga kulilia maslahi makubwa kuliko yale waliyokuwa yakiyapa wakati ule!

Nitamkumbusha jinsi alivyowaunga mkono. Nitamweleza namna alivyotoa mfano wa maslahi manono wanayopewa wabunge wa nchi nyingine zilizoendelea, zenye maslahi makubwa yasiyolingana kabisa na ya wabunge wa hapa bongo.

Nitamkumbusha jinsi alivyosisitiza kuongezwa kwa maslahi ya wabunge bila kujali matatizo ya kiuchumi yaliyokuwa yakilikabili taifa hili.

Hapa nitaongeza kasi ya kuutikisa mkono wake kama ishara ya kumpongeza kwa dhati kwa jinsi alivyoweka pamba masikioni, wakati wananchi wakipiga kelele kupinga azma hiyo ya wabunge kujiongezea marupurupu, wakati taifa likiwa katika baa la njaa na ukosefu wa nishati muhimu ya umeme.

Nitampongeza kwa kuwa mweledi kwa kufanikiwa kuwahadaa na kuwashawishi wananchi na wabunge wa kambi ya upinzani waliokuwa wakimpamba kutokana na mbwembwe zake za kuliongoza Bunge kwa kasi na viwango, kinyume chake akaanza mapema kuonyesha uroho wa kutaka vinono.

Nitampongeza kwa kuamua kushughulikia suala hilo kimya kimya hadi akafanikiwa. Nitampa mfano wa mbunge wa kwetu alivyofurahi baada ya masurufu yake kuongezwa, ingawa siku hizi hatoi sana ‘mshiko’, kama wakati ule alipokuwa akiomba kura.

Hapo nitajichekesha kidogo ili maneno yangu haya ya mwisho yasimuudhi!

Kitakachofuatia, nitamwambia jinsi wananchi walivyomsifia kwa kufanikiwa kumaliza mgogoro wake na Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima, bila kuufikisha ngazi za juu kabisa za chama.

Nitamkumbusha kuwa hata mimi niliwahi kumsifia kwa hili, nilimsifia kupitia waraka wangu gazetini uliokuwa ukieleza jinsi nilivyopendezwa naye kutokana na staili yake ya kipekee ya kuliongoza Bunge!

Nina hakika atatabasamu kwa furaha kupewa sifa za kweli, za jinsi alivyo, kwa sababu ni yeye tu aliyeweza kufanya jambo hilo kati ya Maspika wote tuliowahi kuwa nao katika Bunge letu.

Mtangulizi wake, Pius Msekwa, hakufanya na asingeweza kufanya hivyo, na waliomtangulia Msekwa hali kadhalika. Yeye anajua, Malima anajua na wabunge wote wanajua!

Nitamuunga mkono kwa udhaifu aliouonyesha kama Spika baada ya kukubali zaidi ya sh. milioni 100 za walipakodi ziteketee katika shauri la Malima na mfanyabiashara maarufu nchini, Reginald Mengi.

Nitamtoa wasiwasi kuwa ingawa kuna watu walimcheka, lakini uamuzi wake wa kulimaliza suala hilo kwa njia ya kile alichokiita kuwapatanisha watu hao, hata baada ya Kamati ya Bunge kubaini kuwa Malima alikuwa amesema uongo bungeni wakati akimtuhumu Mengi, ulikuwa safi kwa sababu alikuwa akilinda heshima ya chama chake.

Nitamwambia asiwe na wasiwasi kabisa kwa sababu Watanzania wanaofahamu utendaji wa CCM na msingi mkuu wa chama hicho kumfanya Spika anayetokana na chama chao kuwa mjumbe wa Kamati Kuu yake, wanafahamu sababu za yeye kufanya hivyo.

Nitabadilika kidogo kutoka kwenye uso wa tabasamu ili ninachokusudia kumwambia hapa kimuingie. Nitamtaka awe makini na ile kambi ya wabunge vijana inayoongozwa na kale kakijana kutoka Kigoma.

Nitamuonya asiiamini kabisa kambi hiyo licha ya kwamba ilimsaidia sana wakati wakubwa wenzake walipoamua kumshughulikia, wakitaka kumpoka madaraka yake ya uspika alipotofautiana nao katika sakata lile lile la Malima!

Nitamwambia awe makini sana na vijana wale, kwa sababu kama waliweza kupambana na vigogo wa chama tawala na kuwashinda kwa hoja, kama waliweza kukaa chini na kuandaa hoja walizoziwasilisha bungeni na kulifanya Bunge liwe kimya, kabla hajatoa uamuzi wa kumpa ushauri nasaha Malima, basi awe makini na vijana hao.

Asijali kwamba hoja za vijana hao ndizo zilizomsaidia yeye kutobanwa na chama chake na kuwapiga mweleka waliokuwa wamedhamiria kumwangusha.

Awe makini na hoja za vijana hao kwa sababu hawachoki kusoma, nitamnong’oneza kuwa mmoja wa vijana hao sasa yuko kwa Mandela ananoa ubongo, ili awe ‘gwiji’ wa sheria kuliko hata yeye Spika!

Nitamtaka apunguze tabia ya kuwabania sana, wala asigombane nao kwa sababu wanaweza kumfanyia mambo asiyoyatarajia na kukiona kiti cha Uspika kichungu.

Halafu, nitarudi katika hali yangu ya mwanzo ya kummiminia sifa, nitamsifia kwa jinsi alivyoweza kumbana yule yule kijana kutoka Kigoma pale alipotaka kuivua nguo serikali kuhusu sakata la Buzwagi!

Nitacheka kidogo, najua na yeye atacheka. Lakini kabla hajamaliza kucheka nitaendelea kumwambia kuwa mtu yeyote mwenye akili timamu, atakuwa ameona waziwazi namna yeye Spika Sitta alivyojaribu kujenga mazingira ya hoja hiyo kuchukua mtazamo wa kivyama zaidi hadi yule kijana wa Kigoma akasimamishwa ubunge, lakini watu wengi hawakulijiua hilo!

Nitabadilika tena, nitauachia mkono wake na usoni nitakunja ‘ndita’ kidogo, kwa umakini wa kutosha nitamwambia awe mwangalifu sana na hatua zinazochukuliwa na Rais Kikwete kwa sababu zinaonekana kupingana kabisa na maamuzi yake.

Nitampa mfano wa hilo sakata la kijana wa Kigoma aliyekuwa aking’ang’ania kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kwa ajili ya kuchunguza mkataba wa Buzwagi, jambo ambalo yeye Spika pamoja na wabunge wenzake wa CCM walilipinga, lakini Rais Kikwete akaunda ya kamati yake ya kupitia upya mikataba ya madini nchini akiwa amemshirikisha huyo kijana wa Kigoma.

Mfano mwingine nitakaompa ni huu wa karibuni wa Rais Kikwete kutengua ugavana wa Dk. Daudi Ballali kwa tuhuma za kuwapo kwa ufisadi wa kutisha katika Benki Kuu, jambo Spika Sitta alilolipinga kwa nguvu zake zote bungeni, na hata kutishia kumchukulia hatua za kisheria mwanzilishi wa hoja hiyo, Dk. Willbroad Slaa, kuwa vielelezo vyake kuhusu tuhuma hizo ni vya kughushi.

Nitamtahadharisha awe makini na maamuzi haya ya Rais kwa sababu yanaonekana kupingana na maamuzi yake, jambo ambalo ni hatari sana katika uhai wa pumzi zake kisiasa na linaweza sababisha watu kumcheka mwaka 2010.

Kama hiyo haitoshi, nitamweleza pia jinsi wananchi walivyoanza kuingiwa na wasiwasi kuhusu uwezo wake wa kimaamuzi na kimatendo, hasa pale alipoonyesha dhahiri kushindwa kuwaruhusu wabunge kuikagua Kampuni ya Richmond, baada ya kilio dhidi yake kuonekana kikiongezeka kila kukicha.

Hapa nitamwambia asiwe na shaka sana kwa sababu sasa Richmond imekwishachunguzwa na kamati ya bunge.

Kabla sijamuaga, nitamtaka awe makini sana katika kuongoza kikao hiki cha kumi cha Bunge kwa vile Watanzania sasa wanaokana kufuatilia sana nyendo zake na hata kuwa na mashaka na maamuzi yake kama Spika.

Nitamtaka katika kikao hicho ajidhihirishe tofauti na wanavyodhania wengi kuwa kwa mara nyingine tena Bunge lina Spika asiyefaa.

Kisha, nitamshika mkono na kumuaga huku nikimtakia kila la kheri katika kazi zake za Uspika. Nitamuahidi kumtembelea tena Julai, mwaka huu, wakati wa kikao cha Bunge la Bajeti na kwamba nitaendelea kufuatilia utendaji kazi wake katika wadhifa huo ‘mnene’ wa Uspika.

cmullinda@yahoo.com
0782 698386


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2008 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570