KITUO cha Uwekezaji nchini (TIC), kinatarajia kuwapeleka nchini Ujerumani wawekezaji wazalendo 67 kwa ajili ya kunadi miradi yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Emmanuel ole Naiko, alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa hafla fupi ya kuuaga mwaka 2007 na kuukaribisha mwaka 2008 iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Alisema huo utakuwa ni mwendelezo wa mikakati ya kituo chake kilichojiwekea katika mwaka huu wa 2008, kuhakikisha kuwa kwa kufuata sheria ya nchi, wajasiriamali wazalendo wanaanza kumiliki uchumi wa miradi yao hapa nchini.
“Tunataka kufanya jinsi tuwezavyo kuwapeleka nje wawekezaji wa Kitanzania 67 nchini Ujerumani kwenda kunadi miradi yao,” alisema.
Hafla hiyo fupi iliwakutanisha wafanyakazi wa kituo na familia zao pamoja na wageni mbalimbali akiwepo Rais wa Shirikisho la wenye Viwanda, Biashara na Kilimo nchini (TCCIA), Alloyce Mwamanga.
Akizungumzia mafanikio waliyoyapata katika mwaka wa 2007, Ole Naiko, alisema kituo chake kimefanikiwa kuvuka karibu malengo yote waliyojiwekea.
Alisema awali kituo chake kilijiwekea mikakati ya kupata miradi 650, ambapo lengo lao limevuka kwa kupata miradi 701, hivyo wamevuka lengo kwa miradi 51.
Katika upande mwingine, Mkurugenzi huyo wa kituo cha uwewekezaji alisema mwaka 2007 kituo kilivuka lengo kwa asilimia 51 ambapo kilisajili miradi 701 badala 650 waliyojipangia.
“Tuliweza pia kushughulikia maombi 12,918, ukilinganisha na maombi 10,637 kwa mwaka 2006,” alisema na kuongeza kuwa kitengo cha kodi kilishughulikia maombi 4,984.