AJALI za barabrani wilayani hapa zimepungua kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miezi minne iliyopita, hali inayoelezwa kuchangiwa na semina maalumu ya usalama barabarani iliyofanyika kwa wakazi husika chini ya udhamini wa mgodi wa Resolute uliopo wilayani hapa.
Akizungumza wilayani hapa hivi karibuni, Meneja wa kitengo cha Maendeleo ya Jamii cha mgodi, Mariamu Mavura, alisema wakazi wengi wamepoteza maisha katika wilaya hiyo tangu barabara ya Nzega – Kahama ilipokamilika Juni mwaka jana.
Alisema kutokana na uelewa mdogo wa sheria za usalama barabarani waliokuwa nao wakazi wengi, ajali za barabarani zilikuwa zikiua kati ya watu watatu hadi sita kila wiki.
Alisema kwa miaka mingi usafiri mkubwa kwa wakazi husika ni baiskeli na kwamba kutokuwepo kwa barabara ya uhakika inayopita katika makazi yao kuliwafanya wawe nyuma kujua sheria za matumizi ya barabara.
“Kama unavyojua usafiri mkubwa wa watu wa huku ni baiskeli na kutokana na kutokuwepo kwa barabara za uhakika kwa muda mrefu wakazi wa wilaya hii na vitongoji vinavyotuzunguka walikuwa nyuma sana kisheria,” alisema meneja huyo.
Alisema kutokana na hali hiyo, uongozi wa mgodi ulifanya mazungumzo na kikosi cha polisi cha usalama barabarani wilayani hapa na kufanya semina maalumu kwa wakazi kuhusiana na sheria za barabarani.
Alisema semina hizo zilizokuwa zikiendeshwa kwa awamu kutoka kitongoji kimoja hadi kingine sasa zimeonyesha mafanikio makubwa, kwani vifo vinavyotokana na ajali za barabara vimepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba sasa yaweza kupita hata miezi mitatu bila kutokea.
“Pamoja na jitihada za polisi kudhibiti mwendo wa magari lakini semina tuliyoifanya kwa pamoja na polisi kwa wakazi husika inaonyesha kusaidia kwa kiasi kikubwa katika hili, kwani tangu semina hiyo ilipoendeshwa ajali zimepungua sana,” alisema Mavura.