MKULIMA Athumani Muna (32), mkazi wa Kijiji cha Maswea, Tarafa ya Sepuka, Wilaya ya Singida, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi mtoto wake wa kufikia mwenye umri wa miaka tisa.
Hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini hapa, baada kuridhika na ushahidi uliowasishwa na upande wa mashitaka.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Chiganga Tengwa, alisema mahakama yake imeridhishwa na ushahidi uliotolewa kwani umethibitisha bila kuacha chembe ya shaka kuwa mshitakiwa anayo hatia.
“Mahakama hii inakutia hatiani kwa shitaka uliloshitakiwa nalo, hivyo inakupa adhabu ya kutumikia jela miaka 30 ili iwe fundisho kwako na watu wengine wanaotarajia kufanya kosa la aina hii,” alisema Hakimu Tengwa.
Awali, Mwendesha Mashitaka, Inspekta wa Polisi, Adamu Chasama, alidai Julai 18 mwaka jana, saa mbili usiku, katika Kijiji cha Masweya, mshitakiwa alimbaka mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi ya Masweya.
Alidai kuwa siku ya tukio mshitakiwa alirudi nyumbani kwake saa mbili usiku huku akiwa amelewa na kumkuta mkewe, Halima Selemani akiwa amelala na mtoto wake wa kike (aliyebakwa).
Alieleza baada ya kuingia mshitakiwa alianza kutoa lugha ya matusi huku akikataa kula ugali kwa kutumia mboga ya mlenda.
“Kutokana na hali hiyo, mkewe aliamua usiku huo kwenda dukani kununua dagaa ili aje kumpikia mume, hivyo mshitakiwa alitumia mwanya huo kumfanyia unyama huo mtoto wake wa kufikia na kumtisha asimwambie mama yake,” alisema.
Alisema mtoto huyo baada ya kutishwa na baba yake wa kambo, siku ya tukio hakuweza kumwambia mama yake hadi kesho yake alipozidiwa maumivu, ndipo akamweleza mama yake juu ya kitendo alichofanyiwa na baba yake.