WACHEZAJI Asamoah Gyan na Baffour Gyan, juzi waliamua kujiondoa katika timu ya taifa ya Ghana kufuatia kuibuka mzozo baada ya mechi dhidi ya Namibia.
Katika mechi hiyo ya Kundi A, wenyeji Ghana walishinda 1-0, hivyo kufikisha pointi sita.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la BBC, kutokana na mzozo huo, wachezaji hao ndugu waliamua kutwaa mabegi yao na kutaka kuondoka.
Hatua hiyo ya Asamoah mwenye miaka 22, ilitokana na baadhi ya vituo vya redio nchini Ghana kumlaumu nyota huyo kwamba, alikuwa ameikosesha mabao Ghana.
Baada ya kusikia kipindi cha majadiliano kwenye redio, Asamoah aliamua kuondoka akiungwa mkono na kaka yake Baffour.
Baadhi ya redio hazikuishia hapo, zilizidi kumlaumu mchezaji huyo hata asubuhi ya siku iliyofuata, hali ambayo ilimkasirisha nyota huyo.
Kabla ya tukio hilo, hata Asamoah mwenyewe alifadhaishwa baada ya kukosa mabao mengi katika mechi hiyo dhidi ya Namibia.
Msemaji wa Chama cha Soka cha Ghana (GFA), Randy Abbey, alikana kutokea kwa hali hiyo, lakini wachezaji wawili waliopo kambini, walithibitisha kutokea kwa suala hilo.
“Tulishangazwa kuona Asamoah na Baffour wakijiandaa kuondoka kambini kwa sababu Asamoah amekuwa akipondwa.
“Asamoah alikasirishwa na hatua ya baadhi ya redio kuzidi kumshambulia hadi asubuhi ya siku iliyofuata,” alisema mmoja wa wachezaji hao waliothibitisha tukio hilo.
Habari zinasema kocha wa timu hiyo, Claude Le Roy, alilazimika kuingilia kati kuwasihi nyota hao kusitisha uamuzi wao wa kuondoka kambini.
Asamoah alisema, akiwa mchezaji wa timu hiyo, wananchi wa Ghana wanajua nini anaweza kufanya kwa timu yake na kwamba, kukosesa ni kitu cha kawaida.
“Nimekasirishwa kwa sababu, wananchi wa Ghana wanajua uwezo wangu, hivyo kukosea, ni hali ya ubinadamu na kwamba, si mwisho wa mafanikio,” alisema na kuongeza:
“Nimecheza mechi 22 katika timu ya taifa na kufunga mabao 15, hivyo kama ninakosea, mashabiki wanapaswa kunipa moyo si kushutumiwa.”
Licha ya Ghana kushinda mechi zake mbili katika Kundi A, dhidi ya Guinea na Namibia, lakini imekuwa ikilaumiwa kwa kutocheza soka maridadi.