SOKA Zanzibar huenda ikaingia katika mtikisiko wa aina yake kutokana na Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Ali Ferej Tamim kujiandaa kung’atuka katika wadhifa huo.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa washauri wa karibu wa rais huyo, zinasema sababu za kutaka kuchukua uamuzi huo, ni tofauti zilizojitokeza katika uendeshaji wa soka kati ya ZFA na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo.
Mbali ya sababu hiyo, pia imeelezwa ni kuchelewa kuimarika kwa hali ya afya ya kiongozi huyo baada ya kushauriwa na daktari wake kutofanya kazi za kufikiria kwa muda mrefu pamoja na kutosoma magazeti, kusikiliza redio na kuangalia televisheni.
Ferej, hivi karibuni alinukuliwa akisema kuwa anakabiliwa na matatizo ya usahaulifu kutokana na matatizo ya kichwa yanayomkabili, ambayo yalimfanya mapema mwaka jana kuomba kupumzika kwa miezi mitatu.
Katika kipindi hicho, alikasimu madaraka yake kwa makamu wake, Alhajj Haji Ameir.
“Ali Ferej anafikiria kujiuzulu wadhifa wake kutokana na matatizo yanayoendelea kujitokeza kati ya ZFA na SMZ na kuchelewa kuimarika kwa afya yake,” kilisema chanzo cha karibu na kiongozi huyo siku chache kabla ya kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) uliofanyika Januari 19 nchini Ghana.
Taarifa za kiafya zinasema, kiongozi huyo alishauriwa na daktari wake kutumia muda mwingi kujipumzisha na kujiepusha na vikao vyenye mivutano na malumbano ili kuepuka matatizo ya kiafya.
Tanzania Daima ilipowasiliana na Makamu wa Rais wa ZFA, Alhaj Haji Ameir, alisema hadi jana, walikuwa hawajapokea barua yoyote ya kujiuzulu, isipokuwa alithibitisha Ferej kukabiliwa na matatizo ya kiafya kwa muda mrefu.
“Mimi sina taarifa hizo, isipokuwa kama atajiuzulu, basi ZFA itapata pigo kubwa ambalo halijawahi kulipata tangu kuanzishwa kwa chama hiki, lakini kwa nini watu wanapenda kuvumisha mambo yasiyokuwa na uhakika? Sasa jamani mambo yetu ya ZFA tuachieni wenyewe mbona mmekuwa hivyo? Tuachieni jamani tunakuombeni waandishi,” alisema makamu huyo kwa masikitiko makubwa.
Alisema, taarifa zinazoenezwa na baadhi ya wadau wa soka ambao wamekuwa wakihoji sababu za kiongozi huyo kudai kuwa anasumbuliwa na maradhi ya kichwa, lakini amekuwa mstari wa mbele kuhudhuria vikao vinavyofanyika nje ya Zanzibar na kutolea mfano vikao hivyo kuwa ni Mkutano Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) uliofanyika jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda Ghana.
Makamu huyo alisema, ZFA inaendelea kuthamini na kuujali mchango wa rais huyo mkongwe wa chama hicho na hasa katika masuala ya kimataifa, ambako amekuwa ni tegemeo kubwa katika kuwasilisha mapendekezo yanayohusu Zanzibar kimataifa.
Alisema, msimamo wa rais huyo wa kujiuzulu ama kuendelea na wadhifa wake utatolewa kesho (Jumanne) wakati atakapozungumza na waandishi wa habari, juu ya maazimio ya Mkutano Mkuu wa CAF uliomalizika nchini Ghana, ambako ZFA ilitakiwa na CAF kuunda bodi ya rufaa ambayo itakuwa chombo cha mwisho kitakachosikiliza rufaa mbalimbali za mchezo wa soka.
Hata hivyo, Ferej alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia madai hayo ya kutaka kujiuzulu, simu yake ilikuwa ikiita bila ya kupokelewa.
Kwa muda mrefu, ZFA imekumbwa na makundi yaliyotokana na uchaguzi mkuu na kusababisha kutokufahamiana kati ya viongozi wa chama hicho, Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) pamoja na Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo.