FAINALI za soka za Mataifa ya Afrika zilizoanza kutimua vumbi Januari 20 nchini Ghana kwa kushirikisha miamba 16, zimeanza kutoa sura ya timu gani zitakazotinga robo fainali.
Tangu kuanza kwa fainali hizi, kila mpenzi na shabiki wa soka kama si michezo kwa ujumla, amejionea au kusikia namna nyota wanavyoonyesha uwezo wao katika kusakata soka.
Watanzania tukiwa sehemu ya wadau wa soka katika Bara la Afrika, nasi hatuko mbali katika kufuatilia fainali hizi, si kupata uhondo wa mchezo huo tu, pia kujifunza mengi.
Nimekuwa nikifuatilia na kubaini mambo mengi, ambayo kwetu Tanzania tukiwa miongoni mwa wanachama wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), tunapaswa kujifunza pia.
Watanzania tumekuwa na kiu ya maendeleo ya soka na michezo kwa ujumla, lakini kiu hiyo, bado haijapata jibu licha ya kuwapo kwa juhudi nyingi tu.
Kutokana na juhudi hizo kugonga mwamba, tukajikuta tukilaumiana wenyewe kwa wenyewe kwamba, mmojawapo ni chanzo cha hali hiyo.
Katika mazingira haya, makocha wazalendo wakajikuta wakibebeshwa zigo la lawama kwamba, hawafai hivyo wenye kufaa zaidi, ni makocha wa kigeni.
Hao makocha wa kigeni wakaja nchini na kufundisha timu mbalimbali, hasa za Ligi Kuu, lakini hata hivyo klabu zetu zikawa bado kichwa cha mwendawazimu katika mashindano ya kimataifa.
Achilia mbali klabu, hata timu ya taifa, Taifa Stars tumeshuhudia makocha kadhaa (wazalendo na hata wageni) wakibadilishana bila mafanikio yoyote.
Kabla ya ujio wa Mbrazil Marcio Maximo aliyeanza kuinoa Stars, Agosti 19 mwaka jana, Stars iliwahi kuwa chini ya makocha kadhaa wa kigeni na kizalendo, bila mafanikio.
Stars iliwahi kuwa chini ya makocha kadhaa wa kigeni, kama Mromania Prof. Victor Stanculescu na baadaye Mjerumani, Burkhad Pape, lakini haikuwa dawa.
Julai mwaka jana, Kocha Maximo akatua nchini kwa msaada wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Agosti 19, alianza kazi ya kuinoa Stars.
Kazi ya kwanza ya Maximo, ikawa ni kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Ghana, fainali ambazo kwa mara ya kwanza na mwisho kushiriki ni mwaka1980.
Stars ikiwa katika kundi la saba pamoja na timu za Senegal, Msumbiji na Burkina Faso, ilimaliza ikiwa ya tatu nyuma ya Senegal na Msumbiji.
Hata hivyo, tangu kuja kwa Maximo walau dalili za mafanikio zimeanza kuonekana kwani Stars imetoka nafasi ya 165 hadi 101.
Kama ari hii itaendelea huku Watanzania kwa ujumla wakiunga mkono harakati hizi pamoja na kuwa na uvumilivu, hata kama itachukua muda, Tanzania itapiga hatua baada ya miaka kadhaa.
Hili liliwekwa wazi hata na Maximo siku anawasili (Julai 26 mwaka jana) kwamba, anajua Watanzania wana kiu ya maendeleo ya soka, lakini mafanikio hayawezi kuja haraka.
Kwa kusisitiza kauli yake, akafananisha na ujenzi wa msingi wa maendeleo ya soka kama ujenzi wa nyumba, ambayo ni vigumu kujengwa kwa siku moja.
Alichomaanisha ni kwamba, ni vigumu maendeleo hayo ya soka kuja haraka kama wengi ambavyo wangetaka iwe, bali ni baada ya jitihada za muda mrefu.
Kauli ya Maximo ilikuwa ikitoa jawabu la kwanini soka yetu, ilikuwa imedumaa kiasi cha timu zetu za klabu hata za taifa kushindwa kuhimili mashindano ya kimataifa.
Sababu kubwa ni kukosekana kwa maandalizi ya msingi katika kuwajenga na kuwaandaa vijana tangu hatua ya awali, hivyo kushindwa kufundishika hapo baadaye.
Hili ndilo tatizo kubwa analopambana nalo Maximo kwamba, wachezaji wengi aliowakuta, ni watu wazima, ambao ni kazi kubwa kufundishika.
Kwa vile wachezaji hao wasiofundishika ndio kipenzi cha mashabiki wa klabu maarufu za Simba na Yanga, kuwekwa kwao kando, inaonekana Stars kukosa wachezaji stahili.
Kutokana na dosari hiyo, ndiyo maana katika Mtazamo wangu wa leo, nimeamua kuzungumzia suala hili kwamba, siri ya mafanikio ya soka, ni timu za vijana.
Mifano ni mingi kwani nchi zinazoonekana kutamba katika soka ya Afrika kama Cameroon, Burkina Faso, Guinea, Nigeria, Benin, Ghana, Morocco, Tunisia, Misri, Ivory Coast na nyinginezo, ni baada ya kuwekeza katika vijana.
Nikirejea katika soka ya Tanzania, bila kuwekeza katika soka ya vijana, tutazidi kubadili makocha kila kukicha bila mafanikio kwa sababu wachezji wetu hawaandaliwi vema kuanzia ngazi ya awali.
Suluhisho pekee hapa ni kuwapo mkakati wa makusudi katika kuwezeka kwenye soka ya vijana kwa kuanzia ngazi ya awali hadi wanapokuwa watu wazima.
Sina maana ya kuwakusanya vijana tu, bali kuwapa mafunzo yatakayowaandaa kuwa nyota wa siku za usoni kwani hiyo ni njia pekee ya kupata wachezaji wasomi.
Ninaamini kupitia mfumo huo, suala la kutofundishika kwa wachezaji, halitakuwepo kwa sababu, wachezaji watakuwa wmeandaliwa vema kuanzia ngazi ya awali na wenye uelewa mkubwa kwa ujumla.
Binafsi, naungana na mkakati wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuagiza kila klabu ya Ligi Kuu kuwa na timu za vijana, kwa sababu hiyo ni siri kubwa ya maendeleo ya soka na michezo kwa ujumla.
Namaliza mtazamo wangu kwa kuitaka TFF kutolegeza msimamo wa kila klabu kuwa na timu za vijana, kwa sababu hiyo ni njia pekee ya kuwapata nyota wa kesho.