na Mwandishi
Wetu
MWENYEKITI wa Kamati ya Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Musa Kundecha, amesema ndoa za utotoni zitapungua au kwisha kabisa iwapo serikali itaweka sheria, sera na mipango itakayowezesha watoto wote wa kike na wa kiume kupata elimu bure angalau hadi kidato cha nne.
Alisema azma hiyo itafanikiwa iwapo pia serikali itaweka sheria kali na kusimamia kikamilifu utekelezaji wake, ili kuhakikisha kila atakayebainika kumpa mimba mtoto wa shule anaadhibiwa kikamilifu.
Sheikh Kundecha, alisema hayo mwishoni mwa wiki ofisini kwake Magomeni, Dar es Salaam katika mahojiano maalum na mwandishi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA).
Alisema anaamini kukiwa na utaratibu wa kumwezesha kila mtoto wa kike na wa kiume kusoma bure angalao hadi kidato cha nne, kutapunguza au kuondoa kabisa tatizo la ndoa za utotoni nchini.
Kiongozi huyo wa dini, alisema hivi sasa wasichana wengi hasa wa familia maskini ndio wanaoathirika zaidi na tatizo la ndoa za utotoni kwa sababu wanapoishia darasa la saba au chini yake, wanakuwa hawana shughuli ya kufanya kwa manufaa yao, hivyo hushawishika au kulazimishwa kuolewa.
“Azma ya kutokomeza ndoa za utotoni nchini itafanikiwa kwa kiwango kikubwa iwapo pia kila mwanajamii atajiepusha na mambo yanayosababisha watoto wa kike kukatisha masomo,” alisema.