KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), imemteua Mkurugenzi wa Wazee wa chama hicho, Victor Kimesera, kumenyana na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kinyang’anyiro cha ubunge katika Jimbo la Kiteto.
Katika kamati hiyo iliyokutana mwishoni mwa wiki Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, ilimteua Kimesera kuwa ndiye mgombea pekee aliyependekezwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji cha Wilaya ya Kiteto kilichofanyika Januari 20.
Kimesera, kiongozi wa muda mrefu wa CHADEMA, amekuwa akigombea kiti hicho katika chaguzi kwa muda wa takriban miaka 15 iliyopita. Mwaka 2005 alipata asilimia 42 ya kura zote.
Mbali ya kamati hiyo kumteua Kimesera, pia ilipitisha mkakati wa kampeni ya uchaguzi katika jimbo hilo pamoja na mwongozo kuhusu utekelezaji wa maadili, itifaki na kanuni za chama juu ya utendaji wa kampeni za uchaguzi ndani ya chama.
Mkurugenzi wa Mahusiano na Uenezi wa CHADEMA, Erasto Tumbo, alipoulizwa kwa nini CHADEMA imeamua kumsimamisha mgombea kupitia chama hicho wakati kipo katika ushirikiano na vyama vingine vitatu vya upinzani, alisema vyama hivyo vimeridhia CHADEMA itoe mgombea wa nafasi hiyo.
Tumbo alisema kuwa CHADEMA imeamua kuteua mgombea baada ya kupata baraka za kufanya hivyo kutoka kwa vyama washirika, vikiwamo CUF, TLP na NCCR-Mageuzi.
“Tulishafanya internal consultations (mawasiliano ya ndani) na washirika wenzetu na tukakubaliana kuwa CHADEMA iteue mgombea na wote watatuunga mkono.
“Hapa ninapozungumza na wewe tayari tuna barua zao (vyama vingine) ofisini vikitupa baraka ya kuteua mgombea ambaye wao watamuunga mkono,” alisema Tumbo.
Juzi CCM ilimtangaza, Benedict ole Nangoro, kuwa mgombea wake baada ya jina lake kupitishwa na kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho.
Mgombea huyo aliwashinda Paulo Lemunyo, Ali Juma Lugendo, Benedict Ngarama ole Nangoro, Dann Meng’orick Mollel, Meshark ole Lutikise na Luteni Lepilal ole Moleiment.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), uchaguzi katika jimbo hilo utafanyika Februari 24, mwaka huu, wakati uteuzi wa wagombea utafanyika leo, na kampeni za uchaguzi zitaanza kesho hadi Februari 23.